Wednesday, April 03, 2013

SHAMBUIO LA TALIBAN LAUA 44 AFGHANISTAN

Wanamgambo waasi waliokuwa wamevalia sare za jeshi la taifa la Afghanistan wameua watu 44 na kuwajeruhi wengine 100 baada ya kufanya shambulio dhidi ya majengo ya serikali katika jimbo la Farah. Gavana wa Jimbo la Farah Mohammad Akram Ekhpelwak amesema kuwa, kwa uchache washambuliaji wanane waliuawa kwenye shambulio hilo. Amesema kuwa, shambulio hilo lililofanywa na kundi la wanamgambo wa Taleban lilikuwa na lengo la kuwakomboa wapiganaji wenzao waliokuwa wamefikishwa mahakamani. Amesema kuwa, raia 34, wanajeshi sita na askari wanne wameuawa kwenye shambulio hilo. Ekhpelwak ameongeza kuwa, shambulio hilo lililenga majengo ya serikali zikiwemo ofisi ya mahakama na ile ya Mwanasheria Mkuu. 

IRAN YASEMA MKATABA WA SILAHA NI WA KIBAGUZI


Mwanadiplomasia mwandamizi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amelaani Mkataba Mpya wa Biashara ya Silaha (ATT) uliopasishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kusema mkabata huo una malengo ya kisiasa na ni wa kibaguzi.
Akihutubu mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa siku ya Jumanne, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa Bw. Gholam-Hossein Dehqani amesisitiza kuwa katika hali ambayo lengo kuu la ATT ni kudhibiti biashara ya silaha duniani lakini rasimu ya mwisho ya mkataba huo bado inaruhusu kupelekewa silaha vikosi ambavyo haviko katika nchi zao. Mwanadiplomasia huyo wa Iran amesema kutumwa silaha Mashariki ya Kati na eneo la Ghuba ya Uajemi ni jambo ambalo limeathiri vibaya usalama na maisha ya watu wa eneo hilo na kusababisha idadi kubwa ya watu kupoteza maisha. Dehqani amebainisha kuwa Jamhuri ya Kiislamu ilijaribu kurekebisha makosa ya kisheria katika rasimu ya mkataba huo kwani ulitayarishwa 'kwa malengo ya kisiasa'. Mwanadiplomasia huyo wa Iran amesema mkataba huo umeandikwa ili kukidhi matakwa ya Marekani na muitifaki wake mkuu, Israel. Iran imekosoa mkataba huo kwa sababu hauzuii nchi vamizi kuuziwa silaha. Nchi zilizopiga kura dhidi ya ATT ni pamoja na Iran, Syria na Korea Kaskazini huku wauzaji wakubwa wa silaha kama Russia na China zikijizuia kupiga kura pamoja na nchi zingine 20 duniani.

WAZIRI MKUU WA MALAYSIA AVUNJA BUNGE

Waziri Mkuu wa Malaysia, Najib Razak ametangaza kulivunja bunge ili kutoa fursa ya kufanyika uchaguzi mkuu baadaye mwezi huu. Razak amewaambia waandishi wa habari kwamba ana imani muungano anaouongoza wa National Front ambao umekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 55, utaibuka na ushindi kwenye uchaguzi huo. Hata hivyo, weledi wa siasa za Malaysia wanaamini kuwa, kiongozi huyo atakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa kiongozi wa upinzani, Anwar Ibrahim. Kiongozi huyo wa upinzani aliwahi kukabiliwa na mashtaka ya ulawiti mwaka 2011 ingawa baadaye korti ilimpata bila hatia na kumuachilia huru. Baadaye Ibrahim alidai kuwa serikali ilipanga njama ya kumtupia kesi ya ulawiti ili kumvunja kisiasa. Malaysia ni miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa zaidi ya Waislamu duniani na tuhuma kama hiyo inachukuliwa kwa uzito mkubwa.  Itakumbukwa kuwa, Muungano wa Najib Razak ulipata pigo kubwa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2008 ambapo upinzani ulishinda viti 75 kati ya 222 na hivyo kuunyima muungano huo nafasi ya kuwa na thuluthi 2 ya viti inayohitajika kupitisha muswada bila tabu yoyote.

MULLAH OMAR RUKSA KUGOMBEA URAIS AFGHANISTAN


Rais Hamid Karzai wa Afghanistan amesema kuwa kiongozi wa kundi la Taliban Mullah Mohammad Omar anaweza kugombea katika uchaguzi ujao wa rais uliopangwa kufanyika nchini humo mwezi Aprili mwakani. Rais Karzai amesema kuwa kiongozi huyo wa kundi la Taliban anaweza kuwa mgombea wa kiti cha urais na kuwapa fursa raia wa Kiafghani ya kumpigia kura ya ndio au hapana. Rais wa Afghanistan amesema kuwa katiba ya Afghanistan ni yenye uhalali kwa raia wote wa nchi hiyo na kwamba kundi la Taliban pia linapasa kunufaika na katiba hiyo. Rais Hamid Karzai ameyasema hayo siku chache baada ya kurejea kutoka safari ya kiserikali ya siku mbili huko Qatar ambako alijadiliana na viongozi wa nchi hiyo kuhusu uwezekano wa kufungua ofisi ya Taliban nchini humo kwa ajili ya mazungumzo ya kusaka amani. Mullah Omar amekuwa mafichoni tangu Marekani iishambulie kijeshi Afghanistan mwaka 2001. Hii ni katika hali ambayo mwezi Januari mwaka jana vyombvo vya habari vya Pakistan viliripoti kuwa polisi ya upelelezi ya Marekani FBI imeliondoa jina la kiongozi huyo wa Taliban katika orodha ya magaidi wanaosakwa kwa udi na uvumba na nchi hiyo. Washington ililiondoa jina la Mullah Omar katika orodha hiyo licha ya kulituhumu kundi la Taliban na kiongozi wa zamani wa Al Qaeda Osama bin Laden kuwa ndio waliohusika na mashambulio ya Septemba 11 nchini Marekani.  

ISRAEL YAANZISHA MSHAMBULIZI MAPYA YA ANGA UKANDA WA GHAZA


Ndege za kivita za Israel zimeanzisha mashambulio katika Ukanda wa Gaza, ambayo ni ya kwanza ya aina hiyo tangu utawala huo wa kizayuni ulipofikia makubaliano ya kusimamisha vita na Hamas mwezi Novemba mwaka jana. Waziri wa Mambo ya Ndani wa serikali ya Hamas amesema kuwa ndege za kivita za Israel jana jioni zilishambulia eneo la wazi huko kaskazini mwa Ukanda wa Gaza lakini hakuna mtu aliyejeruhiwa.
Maafisa wa kijeshi wa Israel wamethibitisha kutekelezwa shambulizi hilo huko Gaza hata hivyo hawakutoa maelezo zaidi. Raia wa Palestina zaidi ya 160 wakiwemo wanawake na watoto waliuliwa na wengine wasiopungua 1,200 kujeruhiwa  katika mashambulizi ya siku nane yaliyoanzishwa na Israel kuanzia Novemba 14 hadi 21 mwaka jana huko Ukanda wa Gaza, Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Tuesday, April 02, 2013

VIONGOZI WA UAMSHO WAFUTIWA KESI


MAHAKAMA ya Mwanakwerekwe, Zanzibar imefuta kesi iliyokuwa ikiwakabili viongozi kumi wa Jumuiya ya Uamsho, visiwani Zanzibar. Mahakama hiyo, imefikia uwamuzi huo leo, wakati viongozi hao walipofikishwa Mahakamani hapo. Hii ni kwa mujibu wa taarifa fupi niliyoibandua kutoka ukurasa wa ‘facebook’ iliyowekwa na Hamed Mazrui. Haikufafanua kwanini mahakama imefikia uamuzi huo. Kwa hivyo: Kutokana na hatua hio, viongozi hao sasa watakuwa wanakabiliwa na kesi inayoendelea katika mahakama kuu ya Vuga, mjini Zanzibar. Mara ya mwisho viongozi hao wa Dini, walipofikishwa mahakama kuu, chini ya Jaji Fatma Hamid, kesi yao ilipangwa kusikilizwa tena Aprili 11, mwaka huu.
Jaji Fatma, aliuagiza upande wa mashtaka kupeleka mahakamani kwa maandishi, ombi la kuzuia kutolewa kwa dhamana kwa washtakiwa hao. Jaji huyo aliongeza: Licha ya kwamba upande wa mashtaka umekata rufaa kuzuia kusikilizwa kwa ombi la dhamana, mahakama itaendelea kusikiliza kesi ya msingi pamoja na dhamana inayohusu viongozi hao. Upande wa Mashtaka katika kesi hiyo unaongozwa Ramadhan Nassibu na Raya Msellem, huku upande wa utetezi unaongozwa na wakili, Salim Towfiq na wenzake.

KARZAI ZIARANI MAREKANI


Rais Hamid Karzai wa Afghanistan anajaribu kuimarisha msimamo wa serikali yake kabla ya vikosi vya kimataifa kuondoka Afghanistan mwishoni mwa mwaka 2014. Rais Hamid Karzai wa Afghanistan ameondoka Kabul kuelekea Marekani ambako anatazamiwa kusalia kwa siku kadhaa.Amepangiwa kuzungumza na kiongozi mwenzake wa Marekani,Barack Obama kuhusu hali ya utulivu nchini mwake baada ya shughuli za kijeshi za vikosi vya kimataifa vinavyoongozwa na jumuia ya kujihami ya NATO zitakapomalizika mwishoni mwa mwaka 2014 na pia uchaguzi wa rais nchini Afghanistan.
Mada zote hizo mbili zina umuhimu mkubwa kwa mustakbali wa nchi hiyo.Idadi ya wanajeshi watakaosalia ni muhimu kwa usalama na uchaguzi utabainisha njia gani itafuatwa na nchi hiyo inayozongwa na mizozo. Mada nyengine zitahusiana na uchumi,uhusiano pamoja na nchi jirani na Afghanistan na hasa Pakistan na mazungumzo kuhusu uwezekano wa kufikiwa makubaliano ya usalama kati ya Marekani na Afghanistan.
Wataalam wanakadiria vikosi vya Marekani na jumuia ya kujihami ya NATO vitakavyosalia Afghanistan baada ya mwaka 2014,vinaweza kufikia wanajeshi elfu 30. Hata hivyo raia wengi wa afghanistan wanahofia,maeneo ya kusini na mashariki ya nchi hiyo yanayopakana na Pakistan,yanaweza kuangukia mikononi mwa waasi,mara baada ya vikosi vya kimataifa vinavyoongozwa na NATO-ISAF vitakapoihama nchi hiyo.

MSHAURI WA WAZIRI MKUU WA LIBYA ATEKWA NYARA


Duru za habari zimeripoti kwamba mshauri wa Waziri Mkuu wa Libya ametekwa nyara. Mfanyakazi mmoja wa ofisi ya Waziri Mkuu wa Libya amefichua kuwa Muhammad Ali Al Qatus ambaye ni Mshauri wa Waziri Mkuu wa Libya, Ali Zaidan ametekwa nyara na gari lake limepatikana katika mtaa wa Tajura katika viunga vya mji wa Tripoli. Tukio hilo limetokea baada ya Waziri Mkuu wa Libya mwenyewe na baadhi ya mawaziri wa serikali yake kutishiwa kifo. Ishara zinaonesha kuwa hali ya usalama nchini Libya imeingia katika awamu mpya na tata hususan baada ya kuanza mashambulizi ya waasi dhidi ya viongozi na taasisi za serikali ya Tripoli.
Vyombo rasmi vya habari vya Libya wiki iliyopita pia viliripoti kuwa maafisa kadhaa wa polisi wa jiji la Tripoli walikuwa wametekwa nyara na kundi la wanamgambo na wafuasi wa makundi yenye misimamo mikali. Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Ndani pia walikuwa miongoni ma waliotekwa nyara na kundi hilo. Ingawa Tripoli ilikanusha habari hiyo lakini baadhi ya maafisa wa Congresi ya Taifa la Libya walithibitisha kuwa makundi ya waasi yameanzisha wimbi la mauaji ya kigaidi na kuwateka nyara askari wa serikali. Siku chache zilizopita makundi ya wanamgambo ya Libya yalivamia ofisi ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo mjini Tripoli na Jumapili iliyopita wafuasi wa makundi hayo walishambulia jengo la Wizara ya Sheria.
Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Usalama ya Tripoli Hashim Bashir anasema kuwa shambulizi hilo lilifanyika baada ya Waziri wa Sheria Salah Mirghani kutangaza kuwa, si halali kwa makundi ya wanamapinduzi kudhibiti baadhi ya jela za Tripoli. Baadhi ya jela na magereza za miji ya Tripoli, Misrata, Zawira na Jabal al Gharbi zingali zinadhibitiwa na makundi ya wafanyamapinduzi wa Libya licha ya kuundwa serikali ya mpito nchini humo. Mbali na jela miji kadhaa ya nchi hiyo pia inadhibitiwa ama na makundi ya wanamgambo walioshiriki kwenye mapinduzi ya Libya au wafuasi wa utawala uliong'olewa madarakani wa Muammar Gaddafi. Kwani hadi sasa viongozi wa serikali ya Libya hawajafanikiwa kudhibiti maeneo yote ya nchi hiyo. Suala hilo pamoja na vita vya kugombea madaraka baina ya makabila ya Libya kwa upande mmoja na baina ya serikali na wanamapinduzi wa zamani kwa upande mwingine vinaitumbukiza nchi hiyo katika lindi la ukosefu wa amani.
Majaribio ya kutaka kuuawa viongozi wa ngazi mbalimbali na serikali na jeshi la Libya yamekuwa yakifanyika karibu kila siku. Jaribio la hivi karibuni lilimlenga Kanali Waniis Bu Khmadah, kamanda wa jeshi la Libya kusini mwa nchi hiyo. Kanali Bu Khmadah aliokoka jaribio hilo. Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita maeneo ya kusini mwa Libya ikiwamo miji ya Sabha na al Kafara yamekuwa yakikumbwa na mashambulizi ya makundi ya kigaidi. Maafisa wa serikali ya Libya wanayahusisha mashambulizi hayo na wapiganaji kutoka Chad wanaoingia nchini humo au mapigano yanayojiri kati ya makabila ya Kiarabu na Kiafrika  kusini mwa Libya. Hapana shaka kuwa kuendelea hali hii ya ukosefu wa amani nchini Libya kunatishia mapinduzi ya wananchi na kufungua mlango wa madola ya kibeberu kuingia zaidi mambo ya ndani ya nchi hiyo. Hususan ikitiliwa maanani kwamba baadhi ya nchi za Magharibi zinakodolea macho kwa uroho maliasili na utajiri wa mafuta na gesi wa Libya.

MISRI YAKATAA KUREJESHA BALOZI WAKE TEL AVIV


Msemaji wa Rais Muhammad Mursi wa Misri amekadhibisha vikali uvumi wa kurejeshwa balozi wa Misri huko Tel Aviv, Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Ihab Fahmy amesema kuwa, hadi sasa hakuna mazungumzo yoyote yaliyofanyika juu kuanzishwa tena shughuli za kidiplomasia kati ya pande mbili. Mwezi mmoja uliopita, viongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel waliwataka viongozi wa Misri wamrejeshe Atif Salim balozi wa nchi hiyo mjini Tel Aviv. Misri iliamua kumuita nyumbani Atif Salim, ikilalamikia hatua ya kichokozi na isiyo ya kibinadamu ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kushambulia eneo la Ukanda wa Gaza mwezi Novemba mwaka jana.
Duru za Israel pia zimeeleza kusikitishwa kutokana na kukosekana kiunganishi cha mawasiliano kati ya Rais Mursi na viongozi wa utawala wa Israel.

MATEKA WA KIPALESTINA AUWAWA JELA ISRAEL

Atwaullah Abulsabah, waziri wa serikali halali ya Palestina anayeshughulikia masuala ya Wapalestina wanaoshikiliwa katika jela za Israel, ametangaza kuuawa shahidi mateka wa Kipalestina Maysra Abu Hamdiya katika jela za utawala huo wa Kizayuni. Hayo yamejiri baada ya utawala wa Israel kutangaza habari ya kufariki dunia kwa mateka huyo akiwa katika moja ya hospitali za Israel. Kufuatia habari hiyo, Abulsabah amewataka Wapalestina kuanzisha Intifadha ya Tatu na kuongeza kuwa, umewadia muda wa Israel kukosa amani. Aidha Atwaullah Abulsabah aliyekuwa akiongea na waandishi wa habari, ameonya kuhusiana na uwezekano wa kuongezeka idadi ya mashahidi katika mateka wanaoshikiliwa katika jela za kutisha za utawala wa Kizayuni. Waziri huyo wa Palestina, ameitaka Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuchukua hatua za dharura kwa ajili ya kuokoa maisha ya mateka wengine walio hai, sambamba na kukata mahusiano yao na utawala huo wa Kizayuni. Wakati huo huo Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS Sami Abu Zuhri amesema Israel itajuta kufuatia kuuawa shahidi Abu Hamdiya.

KOREA KUZINDUA MRADI MPYA WA NYKLIA


Korea Kaskazini imetangaza kuwa itazindua upya kituo chake kikuu cha nyuklia katika eneo la Yongbyon huku ngoma za vita zikiendelea kupigwa katika Peninsula ya Korea. Shirika rasmi la habari la nchi hiyo KCNA limesema kituo cha kurutubisha madini ya urani na tanuri nyuklia tano ambazo zilifungwa mwaka 2007 kama sehemu ya mkataba wa kuangamiza silaha, zitaanza kufanya kazi upya katika Taasisi ya Nyuklia ya Yongbyon.
Msemaji wa mirdai ya nishati ya nyuklia ya Korea Kaskazini amesema hatua hiyo ni katika fremu ya sera za kujiimarisha kwa zana za nyuklia na vile vile kutatua matatizo sugu ya ukosefu wa umeme. Jumatatu Korea Kaskazini ilitangaza kuwa sera zake kuu kitaifa ni kuwa na uchumi wenye nguvu na kuzalisha silaha za nyuklia. Siku hiyo hiyo Marekani ilitangaza kutuma meli zake za kivita katika Peninsula ya Korea kwa lengo la kukabiliana na makombora ya Korea Kaskazini. Aidha ndege za kivita za Marekani aina ya F-22 zenye uwezo wa kukwepa rada zimefanya mazoezi katika eneo hilo. Katika upande mwingine Rais wa Korea Kusini, Park Geun-hye amesema nchi yake itajibu haraka hujuma kutoka nchi jirani ya Korea Kaskazini. Korea Kusini na Korea Kaskazini ziliwahi kupigana vita vikali kati ya mwaka 1950 – 1953 na kisha kusaini makubaliano ya usitishaji vita kufuatia mashinikizo ya Umoja wa Mataifa.

RAIS AL-BASHIR KUWAACHIA HURU WAFUNGWA WA SIASA

Rais Omar Hassan al-Bashir wa Sudan amesema kuwa, serikali yake itawaachilia huru wafungwa wote wa kisiasa katika siku chache zijazo. Akizungumza mjini Khartoum wakati wa kuanza vikao vipya vya bunge mapema leo, Rais al-Bashir amesisitiza kwamba maandalizi kwa ajili ya kufanyika mazungumzo ya maridhiano ya kitaifa yanakaribia kukamilika na amewataka Wasudan wote kushiriki mchakato huo wa maridhiano ili taifa lifikie kilele cha saada na ufanisi kisiasa na kiuchumi. Rais wa Sudan pia amewataka waasi wanaopigana na serikali waweke silaha chini na kuja kwenye meza ya mazungumzo kwa maslahi ya nchi. Amekumbusha kuwa, ili Sudan ipate maendeleo ya kweli, watu wote wanapaswa kuwa kitu kimoja na kuzungumza kwa sauti moja. Kiongozi huyo anatarajiwa kuitembelea nchi jirani ya Sudan Kusini. Safari hiyo itakuwa ya kwanza tangu Sudan Kusini ilipojitenga na Sudan Julai 9 mwaka 2011.

VITA YA NYUKLIA INANUKIA KOREA MBILI

Rais wa Korea Kusini, Park Geun-hye amesema nchi yake itajibu haraka chokochoko zozote kutoka nchi jirani ya Korea Kaskazini na kuitaka Wizara ya Ulinzi kukaa ange huku hali ya taharuki ikiendelea kutanda katika Peninsula ya Korea. Bi. Geun-hye amesema Korea kaskazini ikijaribu kutupa hata jiwe katika ardhi ya nchi yake itakiona cha moto. Hii ni katika hali ambayo, Korea Kaskazini ilitangaza siku kadhaa zilizopita kwamba imeingia katika hali ya vita na kwamba iko tayari kuzima ngebe za Marekani na Korea Kusini. Tangazo hilo limewatia tumbojoto viongozi wa Washington na Seoul ambapo hapo jana, ndege za kivita za Marekani aina ya F-22 zenye uwezo wa kukwepa rada zilifanya mazoezi katika Peninsula ya Korea. Weledi wa masuala ya kijeshi wanaamini kuwa hatua hiyo ya Marekani ya kufanyia majaribio ndege hizo, ni onyo kwa Pyongyang kwamba itakiona cha mtemakuni ikithubuti kuishambulia Korea Kusini. Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi wake kuhusu hali ya mambo katika Peninsula ya Korea na kuzitaka Seoul na Pyongyang kukoma mara moja kupiga ngoma za vita katika eneo hilo. Pande mbili hizo ziliwahi kupigana vita vikali kati ya mwaka 1950 – 1953 na kisha kusaini makubaliano ya usitishaji vita kufuatia mashinikizo ya Umoja wa Mataifa.

HIZBULLAH YATANGAZA KUWA TAYARI KUIJIBU ISRAEL KWA LOLOTE


Harakati ya Mapambano ya Hizbullah kwa kushirikiana na Harakati ya Amal zote za Lebanon, zimetangaza kuwa tayari kikamilifu kukabiliana na hujuma yoyote ya kiuadui inayoweza kufanywa na utawala haramu wa Kizayuni dhidi ya taifa hilo. Viongozi wa harakati ya Amal na Hizbullah waliyasema hayo siku ya Jumamosi usiku, katika ripoti ya pamoja na kusisitiza kuwa, harakazi hizo zipo tayari kikamilifu kwa ajili ya kulinda taifa, ardhi na izza ya Lebanona kutokana na aina yoyote ya hatua ya kiuendawazimu ya Wazayuni na kwamba, ikiwa Israel itathubutu kuanzisha chokochoko dhidi ya taifa hilo, basi zitatoa jibu kali kwa vitisho vya utawala huo. Hayo yamejiri kufuatia hatua ya Israel ya kuongeza idadi ya askari wake katika mpaka wake wa pamoja na Lebanon sambamba na kuongeza vitisho dhidi ya taifa hilo la Kiarabu. Sambamba na ripoti ya kulaani hatua hiyo ya Israel ya kuongeza askari wake katika maeneo yaliyotajwa na kuongezeka kwa hatua za kichokozi za mara kwa mara kama vile kukiuka anga, ardhi na bahari ya Lebanon, harakati hizo zimeitaka pia serikali ya Bairut kuchukua hatua kali zitakazosaidia kukomesha uchokozi huo wa Wazayuni. Aidha jeshi la Lebanon pia limetoa ripoti ya kulaani hatua hizo za Wazayuni katika maeneo ya mpakani na kusisitiza kuwa, jeshi hilo limejiandaa vilivyo kwa ajili ya kukabiliana na uchokozi wowote wa Israel. Ripoti za vyombo vya kiintelijensia na usalama nchini Lebanon zinaonyesha kuwa, katika siku chache zilizopita utawala wa Kizayuni umeweka mamia ya askari wake na makumi ya magari ya deraya katika maeneo ya mpakani hususan katika eneo la Shab'aa huku helikopta na ndege za upelelezi za utawala huo zikionekana katika anga ya maeneo ya Jolan na Shab'aa. Hii ni katika hali ambayo Aizenberg kamanda wa usalama wa ndani wa jeshi la Israelamekiri kwamba, ikiwa kutazuka vita vipya kati ya utawala huo na Lebanon, basi vita hivyo vitailetea hasara kubwa Israel kuliko hasara iliyoipata katika vita vya mwaka 2006. Kamanda huyo ametabiri kuwa, ikiwa utawala huo utaingia katika vita vipya na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah nchini Lebanon, kuna uwezekano harakati hiyo ikavurumisha makombora yake kuelekea katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, mara kumi zaidi ya makombora yaliyovurumishwa katika vita vya mwaka 2006. Itakumbukwa kuwa, Israel ilishindwa vibaya na Hizbullah katika vita vya siku 33 mwaka mwaka huo na kulazimika kutoka katika maeneo ya kusini ya Lebanon baada ya kukubali azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lililoutaka utawala huo kuheshimu anga na ardhi ya Lebanona. Hata hivyo tokea wakati huo Israel imekuwa ikikiuka azimio hilo mara kwa mara kwa kudumisha hatua zake za kichochezi na kichokozi dhidi ya Lebanon.
Na Sudi Jaafar Shaaban

VITA VYA DUNIA DHIDI YA UISLAM VYAENDELEA MYANMAR


Imam wa msikiti wa al-Islam wa Washington Marekani amesema kuwa, nchini Myanmar kunaendelea kushuhudiwa vita vya dunia dhidi ya Waislamu huku Umoja wa Mataifa ukiendelea kunyamaza kimya. Sheikh Abdul Alim Mussa amesema katika mahojiano aliyofanyiwa na Kanali ya Televisheni ya Kimataifa ya Press TV kuwa, kuteswa Waislamu wa Myanmar ni sawa na "Vita vya Dunia Dhidi ya Uislamu" na kwamba, Umoja wa Mataifa umeendelea kunyamazia kimya jinai na mauaji dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo. Imamu wa Msikiti wa al-Islam wa Washington Marekani amesema kuwa, Vita vya Dunia dhidi ya Uislamu vinafanyika nchini Myanmar na kwamba, watu wasio na hatia yoyote wanauawa kiholela huku vyombo vya habari vya Kimagharibi vikinyamazia kimya jinai hizo dhidi ya binadamu. Tarehe 20 mwezi uliopita wa Machi, zaidi ya Waislamu 40 waliuawa na misikiti kadhaa kuchomwa moto katika miji kadhaa ya katikati mwa Myanmar. Weledi wa mambo wanaamini kuwa, siasa za kindumilakuwili za Wamagharibi kuhusu haki za binadamu na kulinda utu wa mwanadamu zimechangia katika mauaji ya Waislamu wa Myanmar.
Na Salum Bendera