Friday, December 28, 2012

NJIA KUMI ZA KUHIFADHI QUR 'AN. Part 4.


4. HATUA YA NNE
KUCHAGUA WAKATI NA SEHEMU MUNAASIB KWA KUHIFADHI
Kuweka wakati munaasib kwa kuhifadhi ni njia muhimu inayosaidia kuhifadhi. Na wakati wa kuhifadhi inatofautiana kati ya mtu na mtu kuna anayefadhilisha wakati wa Alfajiri au wakati wa Sahar (kabla ya alfajiri) au baada ya Maghrib. Inapasa uchunge yafuatayo:


 1. Kupangilia muda maalum mfano saa moja au masaa mawili muhimu udumu na muda uliojipangia usipunguze.


 2. Kuwa na faragha kamili katika muda uliojipangia ukate mahusiano na wengine ushughulike na kuhifadhi tu bila ya kuathiriwa na chochote mfano simu makelele au sauti za juu. 3. Kuchagua sehemu maalum yenye utulivu na isiyokuwa na chenye kukushawiwishi mfano picha, vitabu, majarida na vinginevyo vinavyoathiri.
 
5. HATUA YA TANO
KUPANGILIA MWANZO WA HIFDHI (KUHIFADHI)
 Kusudio je mwanzo wa kuhifadhi utakuwa mwanzo wa Mus-haf (Al-Faatihah na Al-Baqarah) au mwisho wa Mus-haf (An-Naas), na hili linatofautiana kutokana na uwezo wa mtu ikiwa mtu ana uwezo mzuri wa kusoma bora aanze mwanzo na ikiwa yupo mwanzo katika kusoma bora aanze na Surat An-Naas.


 Natija ya wote wawili kwa Uwezo wa Allaah ni kufikia katika kuhifadhi Kitabu cha Allaah, wangapi wameanza na Surah ndogo na wamefanikiwa kufika mwisho.


 
6. HATUA YA SITA
KUWEKA IDADI YA AAYAH
Uwezo wa kuhifadhi ni Kipaji kutoka kwa Allaah na inatofautiana uwezo huu kati ya mtu na mtu kikubwa kinachonasihiwa mwanzo wa kuhifadhi ni kuweka idadi kamili hata kama una uwezo zaidi. Kuna mtu anaweza kuhifadhi katika kikao kimoja ukurasa mzima katika Mus-haf kisha siku ya pili ameshasahau baadhi ya Aayah alizohifadhi na kuna mwengine anahifadhi kila siku Aayah tano hazidishi na inakuwa Hifdhi yake ni yenye nguvu.


 Amepokea Abu ‘Umar Ad-Daaniy katika “Al-Bayaan” kutoka kwa ‘Uthmaan na Ibn Mas’uud na Ubay bin Ka’ab kwamba: “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam) alikuwa akiwafundisha Aayah kumi hazidishi zingine mpaka wajifundishe yaliyomo na kuifanyia kazi, Anawafundisha Qur-aan na kuifanyia kazi kwa wakati mmoja.”


 Kutoka kwa Abu ‘Abdir-Rahmaan As-Sulamiy anasema: “Tulikuwa tukijifundisha Aayah kumi katika Qur-aan hatuchukui zingine baada yake mpaka tujue halali yake na haramu yake, amri yake na makatazo.” Na katika kuweka idadi ya Aayah ni kutokana na kutofautiana urefu wake. Mfano tuchukulie “Aayatud-Dayn” ambayo ni Aayah ndefu kuliko zote katika hali hii inapendekezwa kuhifadhi Aayah kuendana na idadi ya mistari. Ama ikiwa Aayah ni ndogo ndogo mfano Suratul As-Swaaffaat, ‘Abasa, At-Takwiyr na zinginezo jiwekee Aayah kumi au tano katika kikao kimoja. Na ukisoma Tafsiyr kuhusu maana ya maneno ni jambo litakalokusaidia katika kuhifadhi. 


 itaendelea Ijumaa ijayo insha-Allah..............

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO