Friday, January 25, 2013

AHMED NEJAD ASISITIZA WAISLAM WOTE KUSHIKAMANA

Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewataka Waislamu kote duniani kuungana na kuzima njama za maadui. Rais Ahmadinejad ameyasema hayo leo, katika sherehe za kumalizika kwa mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya vikosi vya majeshi ya nchi za Kiislamu, yaliyofanyika mjini hapa Tehran kwa mnasaba wa kuwadia uzawa wa Mtukufu Mtume Muhammad (SAW) na wiki ya Umoja. Akizungumzia udharura wa kuimarishwa umoja kati ya Waislamu wote duniani Rais Mahmoud Ahmadinejad amesema kuwa, kuibua migongano na mizozo kati ya Waislamu ni mbinu zinazofanywa na maadui kwa ajili ya kuzusha mifarakano kati yao.
Amesema kuwa, maadui mara zote wamekuwa wakifanya njama za kuanzisha mivutano ya kikabila, kikaumu na kimadhehebu na kuongeza kuwa, pamoja na hayo Qur'ani na Mtume Muhammad ni thamani za Waislamu wote duniani bali pia ni kwa ajili ya watu wote wakiwemo wafuasi wa dini tofauti za mbinguni ikiwemo Uyahudi na Ukristo na walimwengu wote kwa ujumla. Kwa upande mwingine Rais Mahmoud Ahmadinejad amesema kuwa, moja ya sababu zinazopelekea kuzushwa mivutano, ni kutokufahamu tafsiri halisi ya Qur'ani na kwamba, suala hilo kwa muda mrefu limekuwa ndio chanzo cha matatizo kati ya Waislamu.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO