Utawala wa Kizayuni wa Israel umeendelea kupuuza kabisa misingi ya sheria za kimataifa hususan azimio la mwezi Desemba mwaka jana la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na hivi sasa unaendelea na hatua zake za kubadilisha utambulisho wa maeneo ya Wapalestina huko Baytul Muqaddas katika fremu ya stratejia yake ya kuyayahudisha maeneo ya Wapalestina. Ripoti zinaonesha kuwa, Israel inaendelea na njama zake hizo za kuuyahudisha mji wa Baytul Muqaddas kwa kubadilisha majina ya mitaa na barabara za eneo hilo. Kwa msingi huo, Kamati ya Kutoa Majina ya Maeneo huko Baytul Muqaddas imetangaza kuwa, kuna majina mapya 43 ya Kiyahudi katika barabara za Wapalestina. Kabla ya hapo kamati hiyo ilikuwa imebadilisha majina 141 ya mitaa na barabara za Baytul Muqaddas Mashariki na kuyapa majina ya Kiibrania. Wataalamu wa mambo wanaamini kwamba, moja kati ya mikakati ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika miaka ya hivi karibuni ni kusukuma mbele gurudumu la miradi ya kuyayahudisha maeneo ya Wapalestina hususan Baytul Muqaddas. Kuupa mji wa Baytul Muqaddas sura ya Uyahudi imekuwa nguzo kuu na muhimu ya kisiasa ndani ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika miongo ya hivi karibuni; lakini mwenendo huo umechukua kasi zaidi katika kipindi cha serikali ya mrengo wa kulia na yenye kufurutu ada ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu. Hatua za Israel zinaonesha kuwa, kubadilisha muundo wa kijiografia wa Baytul Muqaddas na kuuonyesha kuwa ni wa Kiyahudi ni miongoni mwa mambo yanayopewa kipuambele kikubwa na utawala huo ghasibu. Njama hizo za Israel zimekuwa na lengo la kubadilisha utambulisho wa Kiislamu, muundo wa kijiografia, kijamii, majina, asasi na hata kubadilisha utambulisho wa misikiti; huku hatua hizo zikienda sambamba na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika makazi ya Wapalestina. Netanyahu na baraza lake la mawaziri wakiwa na lengo la kuongeza idadi ya Mayahudi, wameyafanya maisha ya Wapalestina kuwa magumu ili kuwalazimisha waondoka Baytul Muqaddas na kwa muktadha huo wawalete walowezi wa Kiyahudi katika maeneo hayo. Ukweli wa mambo ni kuwa, kubadilishwa majina ya Kiarabu na kuyafanya kuwa ya Kiibrania kwa upande mmoja hupelekea kubadilika muundo wa kidhahiri wa maeneo wanayoishi Wapalestina na kwa upande wa pili kuwafanya watoto wa Kipalestina kuwa mbali na utambulisho wao wa asili. Misikiti na maeneo ya kidini ambayo yanahesabiwa kuwa sehemu ya utambulisho wa Wapalestina yamehujumiwa na kuharibiwa mara kadhaa na Wazayuni na nafasi yake kuwekwa nembo na utambulisho wa Mayahudi yakiwemo mahekalu. Si hayo tu bali mkakati mwingine mkubwa wa Wazayuni ni kubomoa nyumba za Wapalestina kwa kisingizio cha kutokuwa na idhini ya kisheria ya ujenzi. Huku kilio cha walimwengu cha kulalamikia ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi huko Palestina kikiendelea, hivi karibuni Israel ilipasisha mpango mpya wa ujenzi wa vitongoji vipya katika maeneo ya Wapalestina. Hii ni katika hali ambayo, mbali na jamii ya kimataifa, ujenzi huo wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi umekuwa ukilalamikiwa hata na madola rafiki ya utawala huo ghasibu. Desemba mwaka jana Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha maazimio matano ambayo yalilaani miamala na hatua zisizo za kibinaadamu za utawala haramu wa Israel. Katika moja ya maazimio yake hayo, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa sambamba na kueleza wasi wasi wake kuhusiana na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi lilibainisha kuwa, hatua hizo za Tel Aviv ni misdaq na kielelezo cha wazi cha ukiukaji wa sheria za kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa. Ukweli wa mambo ni kuwa, himaya ya daima ya Marekani na baadhi ya madola ya Magharibi kwa Israel, imepelekea maazimio ya Umoja wa Mataifa na ukosoaji wa asasi za kieneo na kimataifa dhidi ya Israel kutokuwa na natija yoyote ile, ambapo hatua ya viongozi wa Tel Aviv ya kukiuka sheria za kimataifa imeendelea kuipa changamoto jamii ya kimataifa
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO