Tuesday, April 09, 2013

KAMPENI ZA UCHAGUZI VENEZUELA ZAPAMBA MOTO

Kampeni za uchaguzi zimepamba moto nchini Venezuela sambamba na kukaribia tarehe ya uchaguzi wa rais nchini humo. Uchaguzi huo wa Rais unaotarajiwa kufanyika baada ya wiki moja yaani tarehe 14 Aprili umepelekea Venezuela ishuhudie vuta ni kuvute kati ya wagombea wawili wa uchaguzi huo. Henrique Capriles, kiongozi wa upinzani nchini humo anayefuata siasa za Wamagharibi, ameshadidisha mashambulizi ya maneno dhidi ya hasimu wake Nicolas Maduro, aliyekuwa Makamu wa Rais wa hayati Hugo Chavez wa Venezuela, na ambaye kwa sasa ni rais wa mpito wa nchi hiyo. Capriles amesema kuwa, ikiwa atachaguliwa kuwa Rais wa Venezuela, atakata ruzuku ya mafuta inayotolewa na Venezuela kwa Cuba kama ambavyo pia atakata uhusiano na nchi alizodai kuwa haziheshimu haki za binaadamu. Aidha mgombea huyo anayeungwa mkono na Marekani amedai kuwa, ataimarisha uchumi wa Venezuela kupitia mabilioni ya dola yanayotumwa na nchi hiyo kwenda kwa nchi za kisosholisti. Kadhalika Capriles amezidi kufichua kufungamana kwake na Wamagharibi kwa kusema kuwa, ataimarisha uhusiano wake na viongozi wa Marekani. Wakati huo huo mgombea huyo wa urais ametabiri kwamba, ikiwa Nicolas Maduro, mgombea wa chama tawala na rais wa muda wa Venezuela atashinda katika uchaguzi wa April 14, basi chi hiyo itakabiliwa na kipindi kigumu. Amedai kuwa Maduro ameshindwa kuiongoza nchi na kwamba, kishindo cha matatizo ya kiuchumi yatakayoikabili Venezuela ikiwa atachaguliwa kuwa rais, kitamlazimu kiongozi huyo ajiuzulu na kuachia madaraka. Amma katika upande wa pili, Nicolas Maduro sambamba na kukanusha madai yote hayo ya Capriles amesisitiza kuwa ataendelea kufuata siasa zile zile za kimapinduzi za rais aliyemtangulia hayati Hugo Chavez wa Venezuela. Maduro mwenye umri wa miaka 50, alianza harakati zake za kisiasa wakati akiwa kijana mdogo na kwa uungaji mkono wa harakati ya kimapinduzi inayofahamika kwa jina la Bolivari huku akiwa dereva wa basi na kuwakilisha wafanyakazi wa jumuiya ya usafirishaji ya mjini Caracas. Aidha Maduro ni mmoja wa waasisi wa chama ambacho baadaye kilikuja kufahamika kama chama cha Chavez. Kiongozi huyo ameonya kuwa, huduma zote za kijamii nchini Venezuela zitasimama ikiwa Henrique Capriles atachaguliwa kuiongoza nchi hiyo ya America ya Latini.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO