Sunday, April 07, 2013

MKUU WA MAJESHI YA MAREKANI AWASILI AFGHANISTAN

Jenerali Martin Dempsey Mkuu wa Jeshi la Marekani jana aliwasili nchini Afghanistan kwa ajili ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Kabul, na pia kamanda wa vikosi vya kigeni vilivyoko nchini humo Jenerali Joseph Dunford. Safari hiyo inafanyika katika hali ambayo, katika wiki zilizopita kulishuhudia wasiwasi katika uhusiano wa Kabul na Washington baada ya Rais Hamid Karzai wa Afghanistan kukosoa vikali utendaji wa nchi za Magharibi na hasa Marekani nchini kwake. Suitafahumu hizo zilijitokeza baada ya serikali ya Marekani kukataa kuikabidhi serikali ya Afghanistan usimamizi kamili wa jela ya Bagram, na pia kuondoa wanajeshi wake katika mkoa wa Ordak. Hata hivyo suitafahumu hizo zimepungua hivi karibuni baada ya Washington kukubali kukabidhi usimamizi kamili wa jela hiyo kwa askari wa Kiagfhani na kuanza mwenendo wa kuwaondoa askari wake katika mkoa wa Wardak. Kwa kuzingatia jendwali lililotangazwa na viongozi wa Jumuiya ya Kijeshi ya NATO la kuondoka kikamilifu askari wa kigeni nchini Afghanistan ifikapo mwishoni mwa mwaka 2014, safari ya Dampsey inatafsiriwa kuwa na umuhimu mkubwa. Hasa kwa kuwa, Washington katika fremu ya makubaliano ya kiusalama na Afghanistan na kwa kisingizio cha kulinda mafanikio ya kiusalama ya askari wa kigeni, inakusudia kuwabakisha baadhi ya wanajeshi wake nchini Afghanistan baada ya mwaka 2014. Hivi sasa viongozi wa White House wanahitilafiana juu ya kuainisha idadi ya askari wa Marekani watakaobakia Afghanistan baada ya kuondoka vikosi vya NATO. Jenerali John Allen kamanda wa zamani wa vikosi vya kigeni nchini Afghanistan alitoa mapendekezo kuhusiana na suala hilo ambayo White House haikuyaafiki. Baada ya wadhifa huo kushikwa na Dunford miezi miwili iliyopita, moja ya majukumu yake yalikuwa ni kuweka mipango ya kundoka vikosi vya kigeni nchini Afghanistan na wakati huo huo kuchunguza idadi ya wanajeshi wa Marekani wanaopaswa kubakia nchini humo baada ya mwaka 2014. Katika fremu ya senario hiyo White House inakusudia kutia saini makubaliano ya usalama na serikali ya Kabul ili iweze kuwapatia kinga ya kutoshtakiwa wanajeshi wa Marekani, suala ambalo linapingwa vikali na wananchi pamoja na makundi mbalimbali ya Afghanistan. Karzai ambaye anashinikizwa na Marekani ili akubali takwa la nchi hiyo la kupewa kinga ya kutoshtakiwa wanajeshi wake amesema kuwa, uamuzi juu ya suala hilo utachukuliwa katika mkutano ujao wa baraza la viongozi wa kikabila linalojulikana kama Loya Jirga. Hii ni katika hali ambayo vyama vinavyopinga serikali ya Afghanistan vinasema kuwa, baraza hilo halina haki ya kisheria ya kuamua suala hilo. Vyama hivyo vinasisitiza kuwa, suala hilo linapaswa kujadiliwa na kuamuliwa na Bunge la Afghanistan. Inaonekana kuwa, moja ya malengo ya Jenerali Dempsey katika safari yake nchini Afghanistan ni kuwashawishi viongozi wa nchi hiyo ili waweze kukubaliana na mpango huo. Wataalamu wa mambo wanasema kuwa, kwa kuzingatia msimamo mkali wa Karzai dhidi ya siasa za Marekani, hasa kutoridhishwa kwake na mpango wa White House wa kufanya mazungumzo na kundi la Taliban, ni jambo lililo mbali kuwa rais huyo wa Afghanistan atakubali uamuzi huo wa upande mmoja wa Washington wa kupewa kinga ya kutoshtakiwa wanajeshi wa Marekani, bila suala hilo kupitishwa na bunge.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO