Tuesday, April 09, 2013

MRIPUKO WA BOMU WAUA 15 DAMASCUS


Habari kutoka Damascus, mji mkuu wa Syria zinasema kuwa zaidi ya watu 15 wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa kufuatia mlipuko mkubwa wa bomu karibu na Benki Kuu pamoja na Wizara ya Fedha ya nchi hiyo.
Habari zaidi zinasema bomu lililoripuka lilikuwa limetegwa kwenye gari. Televisheni ya taifa ya Syria imeonyesha uharibifu mkubwa katika eneo la tukio huku miili ya waliouawa ikiondolewa. Wanawake kadhaa ni miongoni mwa wahanga wa shambulio hilo ambalo serikali imesema limetekelezwa na makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Wamagharibi.
Ingawa hakuna kundi lolote lililodai kuhusika na tukio hilo, lakini baadhi ya wachambuzi wanaamini kuwa makundi ya waasi ndiyo yaliyohusika ili kuonyesha kuwa serikali ya Rais Bashar Asad ni dhaifu na imeshindwa kudhamini usalama wa raia wake. Makundi hayo yanayopata misaada ya kifedha na silaha kutoka katika baadhi ya nchi za Kiarabu na Magharibi zimekuwa zikitumia mbinu hiyo ya kuripua mabomu mjini Damascus kama njia ya kuipiga vita serikali. Majuma kadhaa yaliyopita, waasi waliripua bomu katika msikiti mmoja mjini humo na kusababisha vifo vya watu 42 akiwemo mwanachuoni mashuhuri, Mohammad Saad Al-Bouti.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO