Saturday, April 06, 2013

RAIS WA MISRI NA SUDAN WAKUTANA

Rais Muhammad Mursi amefanya ziara rasmi ya kiserikali nchini Sudan ikiwa ni safari yake ya kwanza nchini humo tangu achaguliwe kuwa Rais wa Misri mwezi Juni mwaka 2012. Wakuu wa Misri wamesema kuwa lengo la safari hiyo ni kujenga upya uhusiano wa kisiasa baina ya nchi hizo jirani na kustawisha ushirikiano wa kiuchumi wa pande mbili. Kustawishwa uhusiano wa kisiasa, kiuchumi na kibiashara ndiyo ajenda kuu ya mazungumzo ya Marais wa nchi hizo mbili. Uhusiano wa  nchi hizo mbili ambazo wananchi wake wana udugu wa muda mrefu uliharibika mwaka 1995 baada ya dikteta wa zamani wa Misri, Hosni Mubarak kutoa tuhuma mbaya dhidi ya viongozi wa Sudan. Dikteta wa zamani wa Misri ambaye alipinduliwa na wananchi mwaka 2011 alidai kuwa viongozi wa Sudan walikuwa na nia ya kumuua katika kikao cha wakuu wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa Ethiopia. Hivi sasa karibu miongo miwili imepita na uhusiano wa nchi hizo mbili haujatengamaa. Ni kwa sababu hiyo ndio maana vyombo vya habari vya Sudan vikaitaja safari ya hivi sasa ya Rais wa Misri nchini Sudan kuwa ni ya kihistoria. Hata hivyo baadhi ya weledi wa mambo wanasema kuwa, bado ni mapema mno kuweza kuiita safari hiyo kuwa ni ya kihistoria. Swafwat Fanous, mmoja wa wachambuzi wa masuala ya kisiasa wa Chuo Kikuu cha Khartoum amesema kuwa, hatuwezi kusema kwamba Sudan inapewa kipaumbele cha kwanza na Rais Muhammad Mursi wa Misri kwani ametembelea nchi nyingine nyingi kabla ya kutembelea Sudan. Amesema, safari ya Rais wa Misri katika nchi jirani ya Sudan imechelewa sana. Muhammad Mursi kutoka kundi la Ikhwanul Muslimin amekuwa akisema mara kwa mara kuwa analipa umuhimu mkubwa suala la kustawisha uhusiano wa Misri na majirani zake. Wachambuzi wengine wa mambo wanaamini kwamba, kuwa na uhusiano mzuri na Sudan ni muhimu sana kwa Misri hasa linapofika suala la matumizi ya maji ya mto Nile. Hii ni kwa sababu sekta ya kilimo nchini Misri inategemea kikamilifu maji ya mto Nile. Si hayo tu, lakini pia mwaka jana Essam Sharaf, mmoja wa viongozi waandamizi wa kisiasa nchini Misri na ambaye alikuja kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo alisema kwamba Misri ni nchi ya tatu kwa kuwa na vitega uchumi vingi nchini Sudan. Alisema, uwekezaji wa kiuchumi wa Misri nchini Sudan unapindukia dola bilioni tatu na milioni 400. Vile vile nchi hizo mbili zina mzozo kuhusu umiliki wa eneo la mpakani la Halaib katika fukwe za Bahari Nyekundu, suala ambalo ni muhimu kufanyiwa mazungumzo. Ni kwa sababu hiyo ndio maana watambuzi wa mambo wakasema kuwa, safari ya Rais Muhammad Mursi wa Misri nchini Sudan ni uwanja mzuri sana wa kuweza kupanua uhusiano wa nchi hizo na kufikia mwafaka juu ya masuala ya pande mbili. Weledi hao wa mambo wanataja baadhi ya mambo muhimu ya kufikiwa mwafaka na pande hizo mbili kuwa ni pamoja na kuwa na mfumo unaofanana wa kiuchumi, kufungua njia za kuingia na kutoka kiurahisi wananchi wa nchi mbili hasa wafanyabiashara na masuala mengineyo. Vile vile viongozi wa Misri na Sudan wanaweza kuitumia vizuri fursa hiyo kuweza kuwa na misimamo ya pamoja katika majukwaa ya kimataifa hasa kwa vile wananchi wa Sudan na Misri ni ndugu na wana mfungamano mkubwa wa kidini, kikabila na kiutamaduni.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO