Tuesday, May 28, 2013

WAKIMBIZI LAKI NNE WA MALI WANA HALI MBAYA

Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu nchini Mali limetangaza kuwa, tangu mwezi Januari mwaka jana hadi sasa, karibu raia laki nne wa nchi hiyo, wamelazimika kukimbilia maeneo yenye amani baada ya maeneo yao kukumbwa na machafuko. Mkurugenzi wa Shirika hilo PeterMoorer amewambia waandishi wa habari kuwa, karibu raia wa Mali wapatao laki nne, ni wakimbizi wa ndani ya nchi yao. Ameongeza kuwa, wakimbizi hao wanaishi katika kambi za wakimbizi huku wengine wakilazimika kuishi kwa ndugu zao. Amesema kuwa wale ambao ndugu zao hawana uwezo wa kifedha wanaishi hali mbaya sana ya kibinaadamu. Moorer amesisitiza kuwa, Shirika la Msalaba Mwekundu, limekuwa likishindwa kufikisha misaada kwa wakimbizi hao, kutokana na sababu za ukosefu wa usalama, uthabiti na kuongezeka vitendo vya utumiaji mabavu katika maeneo ya kaskazini mwa Mali. Aidha amesema kuwa, ukiachilia mbali idadi hiyo ya wakimbizi wa ndani, idadi kubwa nyingine ya wakimbizi wa nchi hiyo, wamekimbilia nchi za jirani zikiwemo za Mauritania, Niger, Burkina Faso na Algeria.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO