Tuesday, June 11, 2013

JESHI LA SYRIA LAJIPANGA KUCHUKUA MJI WA ALLEPO

Majeshi ya serikali ya Syria yanajiandaa kuchukua uthibiti wa ngome nyingine ya wapiganaji wa upinzani mjini Allepo na viunga vyake. Duru kutoka ndani ya jeshi la Syria zinasema kuwa oparesheni hiyo itafanyika kwa saa au siku chache zijazo na tayari jeshi limeshajihami kukabiliana na waasi hao.
Mpango huu wa serikali ya Syria unakuja siku chache baada ya jeshi kufanikiwa kuchukua uthibiti wa mji wa kimkakati wa Qusair kwa usaidizi wa wapiganaji kutoka Lebanon wa Hezbolla. Jumapili iliyopita, jeshi lilifanikiwa kuchukua vijiji karibu na mpaka wa Lebabon na Homs.
Maeneo mengi ya Kaskazini mwa nchi hiyo yamekuwa yakithibitiwa na wapiganaji wa upinzani kuanzia mwaka uliopita lakini kuchukuliwa kwa mji wa Qusair kumewapa ushindi mkubwa wanajeshi la serikali. Wachambuzi wa siasa za Syria wanasema kuwa kuwasili kwa kundi la Hezbolla na usaidizi wa serikali wa serikali ya  Iran kumelisaidia sana jeshi la Syria ambalo awali lilionekana dhaifu.
Aidha, inaelezwa kuwa Hezbolla limesababisha mgawanyiko mkubwa kati ya Waislamu wa Kisuni na Kishia nchini humo suala ambalo  wachambuzi wanasema lisipoangaliwa vema linaweza kusababisha  kusambaa kwa mgogoro huo hadi katika nchi jirani. Mzozo wa Syria umekuwa ukiendelea kwa kipindi cha miaka miwili sasa na umesababisha zaidi ya watu elfu 90 kupoteza maisha yao na Mamilioni kukimbia makwao wengi wakikimbilia nchi jirani kama Lebanon, Jordan na Uturuki.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO