Habari kutoka mjini Istanbul, Uturuki zinasema kuwa polisi wa kuzima fujo wamekabiliana na waandamanaji usiku kucha na kufanikiwa kuwaondoa kabisa katika medani mashuhuri ya Taksim. Habari zaidi zinasema moshi umetanda karibu na medani hiyo huku taka zikiwa zimezagaa kote kufuatia fujo za usiku wa kuamkia leo. Hapo jana Waziri Mkuu, Reccep Tayyip Erdogan aliwataka waandamanaji kuondoka mara moja kwenye medani hiyo na kufanya maandamano yao katika bustani ya Gezi. Meya wa Istanbul amesema kupitia radio na televisheni kwamba, oparesheni ya kuwaondoa waandamanaji katika medani hiyo itaendelea. Waandamanaji wanamtaka Waziri Mkuu ajiuzulu. Erdogan anatarajiwa kukutana na waandamanaji hao leo Jumatano ili kusikiza kilio chao lakini baadhi ya watu wanadai kwamba, wajumbe watakaokutana na Waziri Mkuu huyo ni vibaraka wa serikali na wala si wawakilishi wa wale wanaoandamana.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO