Mafuriko katika eneo la kusini mwa Ujerumani katika mto Danube yanaanza kupungua, ikiwa ni taarifa nzuri kwa maafisa wanaoendelea kufanya usafi wa mazingira baada ya mvua kubwa kunyesha katika eneo la Ulaya ya kati. Hata hivyo maji ya mto Elbe , ambayo yalivunja tuta la kuzuwia maji mapema siku ya Jumatatu mashariki mwa mji wa Magdenburg, yanaelekea katika mji wa Hamburg. Hali inaangaliwa katika mji wa Lauenberg katika jimbo la kaskazini la Schleswig-Holstein, ambako mto Elbe unatarajiwa kujaa kuanzia kesho.
Katika wiki chache zilizopita , mvua imesababisha mito mikubwa kufurika , na uharibifu mkubwa katikati na kusini mwa Ujerumani, Jamhuri ya Czech , Austria, Slovakia na Hungary. Gharama za uharibifu zinakadiriwa na shirika la viwango la Fitch kufikia kiasi ya euro bilioni 12 nchini Ujerumani pekee, wakati mashirika ya bima yatapata hasara ya kiasi cha kati ya euro bilioni mbili na bilioni tatu na nusu. Waziri wa mazingira wa Ujerumani Peter Altmeier ametoa wito wa kuwa na mtazamo mpya juu ya ulinzi dhidi ya mafuriko.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO