Harakati ya Ikhwanul Muslimin ya nchini Misri imesema kuwa nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani ndizo zilizolishawishi jeshi kumpindua Rais Muhammad Morsi Jumatano iliyopita. Mohammad al-Beltagi, afisa wa ngazi za juu wa Ikhwanul Muslimin amesema Tayari baadhi ya nchi za Ulaya zimeanza kuutambua utawala wa mpito jambo linalodhihirisha kuwa nchi hizo zina mkono kwenye mapinduzi yaliyotokea. Al-Beltagi amesema hatua hiyo imezidi kuligawa taifa la Misri na kwamba huenda kusipatikane tena maridhiano ya kitaifa. Amesema kuwa machafuko yoyote yatakayotokea yatakuwa mikononi mwa Wamagharibi. Huku hayo yakijiri, ripoti zinasema kuwa Marekani ilikuwa imemtahadharisha Rais Mursi kwamba asipofanya mabadiliko kwenye baraza lake la mawaziri angepinduliwa. Gazeti la New York Times limeripoti kwamba, Bi. Susan Rice Mshauri wa Masuala ya Usalama wa Taifa wa Marekani alimpigia simu Dkt. Mursi saa moja kabla ya kupinduliwa na kumtaka atangaze mabadiliko makubwa. Kwa mujibu wa gazeti hilo, Rais Mursi hakutoa jibu lolote na badala yake alikata simu.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO