Monday, July 08, 2013

KAMPENI ZAANZA NCHINI MALI KABLA YA UCHAGUZI WA JULY 28

Kampeni za kuelekea uchaguzi wa tarehe 28 Mwezi huu nchini Mali zilianza mwishoni mwa Juma lililopita, huku Taifa hilo likifanya jitihada za kulirejesha Taifa hilo katika hali ya utulivu baada ya mzozo wa Kisiasa uliodumu kwa Miezi 18. Kura hizo zitakuwa za kwanza tangu Mapinduzi ya kijeshi ya Mwezi Machi mwaka jana, Mapinduzi yaliyomuondoa madarakani Rais aliyechaguliwa kidemokrasia. Uchaguzi utakuwa wakwanza tangu mapinduzi yaliyomuondoa kiongozi aliyechaguliwa Kidemokrasia, ikiwa ni miezi kadhaa kabla ya muda wake wa kuondoka Madarakani kumaliza muhula wake wa uongozi.
 Mwishoni mwa Juma lililopita Serikali ya mpito iliondoa hali ya taadhari iliyodumu kwa miezi sita, hatua inayoelezwa na Maafisa nchini humo kuwa ni kiashiria kuwa nchi ya Mali inarejea katika hali ya utulivu wakati huu wakielekea katika uchaguzi Mkuu. Lakini Wachambuzi wa mambo wanadai kuwa Mchakato wa kuelekea uchaguzi umewahi sana, hivyo wameonesha wasiwasi wao kuwepo kwa uchaguzi wa kidemokrasia hali itakayohatarisha Taifa hilo na kuingia kwenye Machafuko zaidi. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,Ban Ki-Moon amesema kuwa hatua ya maandalizi ya Uchaguzi huo ni kubwa mno hivyo ni budi uchaguzi huu ukawa wa huru na haki wenye kukubaliwa na Raia wote wa Mali.
Jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa, lenye Wanajeshi 6,000 kutoka nchi za Magharibi mwa Afrika watakaokuwa na jukumu la kulinda usalama wakati na baada ya uchaguzi wanatarajiwa kuongezeka na kufikia Wanajeshi 11,200 , sambamba na Polisi 1,400, ifikapo mwishoni mwa Mwaka huu. Lakini Uchaguzi wa Mali umeelezwa kuwa na dosari kukiwa na Shuku kama nchi hiyo iko tayari kufanya uchaguzi tarehe 28 mwezi huu, huku Takriban Watu 500,000 wakiwa wameikimbia nchi hiyo kutokana na Mzozo wa kisiasa nchini Mali.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO