Wanaharakati nchini Misri wanaomuunga mkono Kiongozi aliyeondolewa madarakani Mohamed Morsi na wale wanaompinga wameahidi kufanya maandamano makubwa katika Ijumaa ya kwanza tangu kuanza mwezi Mtukufu wa Ramadhan kuonesha misimamo yao. Kambi hizo mbili ambazo zinatofautiana kwenye misimamo zimeahidi kufanya maandamano makubwa kwenye viunga vya Tahrir na Nasr kipindi hiki Waziri Mkuu wa Mpito Hazem Al Beblawi akisema serikali yao itashirikisha pande zote. Chama cha Muslim Brotherhood kimeendelea kusimama kidete kupinga kushiriki kwenye serikali kipindi hiki Marekani ikisema itaendelea kutoa msaada wa kijeshi kwa Misri.
Serikali ya Rais Barrack Obama imesema kuwa inatathimini kama kilichofanyika nchini Misri ni mapinduzi ya kijeshi,ambapo ni kinyume cha Sheri a za Marekani ikiwa itabainika hivyo, Marekani italazimika kusitisha misaada yake nchini Misri. Wizara ya ulinzi nayo imesema itaendelea kudumisha mahusiano ya kijeshi na Misri na kuwa Marekani imesema inataka kuona kuwa utawala wa kiraia na kidemokrasia unakuwepo nchini humo. Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amekemea kitendo cha kushikiliwa kwa aliyekuwa Rais wa Misri, Mohamed Morsi sambamba na Viongozi wengine wa Chama cha Muslim Brotherhood.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya nje ya Misri Badr Abelatty aliwaambia Waandishi wa Habari kuwa Morsi yuko mahali salama na kuwa wanahakikisha wanalinda usalama wake.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO