Monday, August 19, 2013

WAFUASI WA MORSI 38 WAUAWA GEREZANI

Kiongozi mmoja wa usalama nchini Misri ametangaza kuwa, wanachama 38 wa Harakati ya Ikhwanul Muslimin wameuawa, katika tukio la mapigano kati ya askari polisi na watu waliokuwa na silaha, waliotaka kuwatorosha watu hao kutoka gerezani. Habari zinasema kuwa, mapigano hayo yalitokea karibu na jela ya Abu Zaabal katika mkoa wa al-Qalyubiyah. Aidha wafungwa hao walikuwa wamemteka polisi mmoja katika mapambano hayo. Wizara ya Mambo ya Ndani nchini Misri imetangaza kuwa, polisi walifanikiwa kumuokoa polisi huyo ambaye alikuwa amejeruhiwa vibaya. Jana wafuasi wa Ikhwanul Muslimin walisitisha maandamano mjini Cairo kwa kile walichosema kuwa ni kuepusha umwagikaji damu zaidi dhidi yao.  Ripoti iliyotolewa na harakati hiyo, ilisema kuwa, Ikhwan wameamua kusitisha maandamano yao, kutokana na kuwepo hali tete nchini humo. Kabla ya hapo, ilikuwa imepangwa kufanyika maandamano ya nchi nzima, kwa ajili ya kutaka kurejeshwa Muhammad Mursi, Rais halali wa Misri aliyepinduliwa na jeshi la nchi hiyo.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO