Sunday, January 06, 2013

VIKWAZO VIPYA VYA MAREKANI VYAPINGWA NA CHINA

China imetangaza kuwa inapinga na inalaani vikali vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hua Chunying, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya China amesema kuwa, nchi yake haikubaliani na vikwazo hivyo vipya vya Marekani dhidi ya Iran. Amesisitiza kwamba, Beijing haiafiki vikwazo hivyo dhidi ya Iran kwa kisingizio cha miradi ya nyuklia inayofanyika kwa malengo ya amani na tena chini ya usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA. Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya China amesisitiza kuwa, Beijing inaamini kuwa, njia bora kabisa ya kupatiwa ufumbuzi kadhia ya miradi ya nyuklia ya Iran ni mazungumzo na ushirikiano. Hayo yanajiri katika hali ambayo, Saeed Jalili Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amenukuliwa akisema mjini New Delhi, India kwamba, mazungumzo kati ya Tehran na kundi la 5+1 yanatarajiwa kuanza hivi karibuni. Aidha Michael Mann, Msemaji wa Catherine Ashton, Mkuu wa Siasa za Nje za Umoja wa Ulaya alinukuliwa hivi karibuni akisema kwamba, duru nyingine ya mazungumzo baina ya Iran na kundi la 5+1 linalozijumuisha nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani itafanyika mwezi huu wa Januari, ingawa mahala na tarehe hasa ya kufanyika mazungumzo hayo bado haijaainishwa rasmi.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO