Sunday, January 06, 2013

WANANCHI WA IRELAND WAWAJERUHI POLISI

Raia watiifu kwa serikali ya Uingereza kaskazini mwa Ireland wamewajeruhi askari polisi kadhaa wakati wa maandamano ya kupinga uamuzi wa Halmashauri ya Mji wa Belfast kupunguza siku za kupeperusha bendera ya muungano wa nchi hiyo na Uingereza. Kundi la watu 300 mashariki mwa Belfast waliwashambulia maafisa wa polisi kwa kuwarushia mabomu ya petroli na mawe jioni ya siku ya Ijumaa. Polisi walitumia maji ya kuwasha kuwatawanya waandamanaji hao pamoja na kuwakamata baadhi yao. Maandamano ya waumini wa madhehebu ya Protestanti wenye hasira yamekuwa yakiukumba mji huo mara kwa mara tangu tarehe 3 mwezi Desemba baada ya Halmashauri ya mji huo kupitisha uamuzi wa kupunguza siku ambazo bendera ya Uingereza nchini humo itapepea katika mlingoti wa jengo kuu la ofisi hiyo. Waprotestanti wanadai kuwa uamuzi huo wa kupunguza siku ni dalili ya masharti mengi yanayotolewa na watu wa madhehebu ya Katoliki katika mchakato wa kutafuta mapatano ya amani baina yao. Bendera hiyo ambayo inaungwa mkono na Uingereza imekuwa ikipepea katika jengo la Halmashauri ya mji wa Belfast tangu mwaka 1906 ikiwa ni alama ya uhusiano baina ya Uingereza na na jimbo la Ireland Kaskazini.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO