Wednesday, April 10, 2013

BUNGE LA SUDAN LATAKA JESHI KUPAMBANA NA WAASI


Bunge la Sudan limelitaka jeshi la nchi hiyo kutumia mbinu za kisasa katika kukabiliana kikamilifu na hatimaye kuwaangamiza waasi wa Darfur, magharibi mwa nchi hiyo. Bunge la Sudan limesisitiza juu ya ulazima wa kukombolewa haraka maeneo kadhaa yanayokaliwa kwa mabavu na waasi. Taarifa ya bunge hilo imewatuhumu waasi kwa  kuwazuia wakaazi wa eneo hilo kuondoka kwenye  maeneo wanayoyadhibitiwa. Taarifa hiyo imetolewa baada ya AbdulRahim Muhammad Hussein Waziri wa Ulinzi wa Sudan leo kulihutubia bunge na kutoa taarifa inayohusiana na hali ya kiusalama katika eneo hilo.
Eneo la Darfur lililoko magharibi mwa Sudan, tokea mwaka 2003 limekuwa likikabiliwa na machafuko ya makundi ya waasi yanayoungwa mkono kisilaha na kifedha na nchi kama Sudan Kusini na Uganda dhidi ya serikali ya Sudan. Imeelezwa kuwa, maelfu ya watu wameuawa na mamia ya maelfu ya wengine kuyakimbia makazi yao katika eneo hilo. Wakati huohuo, Taasisi ya Kukagua Silaha Ndogondogo 'SAS' yenye makao yake Geneva, imeeleza kuwa, Sudan Kusini inawaunga mkono kifedha, kisilaha na kisiasa waasi wa Sudan.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO