Friday, April 12, 2013

LIBYA YAKATAA KUTUMWA WANAJESHI WA KULINDA USALAMA


Viongozi wa Libya wamesisitiza kuwa hawataruhusu kwa njia yoyote ile kutumwa nchini humo askari wa kulinda usalama kutoka nchi za kigeni. Msimamo huo umechukuliwa baada ya viongozi wa nchi za Magharibi kusikika wakisema kuwa wanatilia shaka uwezo wa serikali ya Libya wa kulinda usalama wa visima vya mafuta vya nchi hiyo. Kuhusiana na suala hilo ujumbe wa mashirika ya mafuta ya Uingereza ulikutana hivi karibuni na Nuri Balruin Mkuu wa Shirika la Mafuta la Kitaifa la Libya LOC na kumfahamisha wasiwasi wa mashirika hayo kuhusiana na usalama wa wafanyakazi wao. Wasiwasi wa Wamagharibi kuhusiana na suala la usalama nchini Libya ukiwemo usalama wa balozi zao, umepelekea viongozi wa serikali za Magharibi kufanya safari kadhaa nchini humo, ikiwemo safari ya hivi karibuni ya Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron, kwa lengo la kuchunguza usalama wa maslahi yao. Akiwa nchini Libya Cameron alitoa matamshi ya uingiliaji masuala ya ndani ya nchi hiyo kwa kuwataka viongozi wa Tripoli waimarishe sheria na usalama nchini. Kabla ya hapo Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza ilikuwa imewataka raia wake kuondoka nchini humo kutokana na vitisho vya kiusalama dhidi yao.
Kwa kuzingatia kuwa serikali ya Tripoli haijafanikiwa kudhibiti maeneo yote ya nchi hiyo, kuna uwezekano mkubwa wa makundi ya kigaidi na ya wanamgambo kuyadhibiti maeneo hayo. Licha ya kupita zaidi ya mwaka mmoja tokea kuangushwa kwa utawala wa dikteta Muammar Gaddafi serikali mpya ya nchi hiyo imeshindwa kabisa kudhibiti na kurejesha usalama katika maeneo yote ya nchi. Kwa kutumia vibaya hali hiyo, nchi za Magharibi zinafanya njama za kutuma nchini humo askari wa kigeni ili kuandaa uwanja wa kupora zaidi utajiri wa nchi hiyo ya Kiarabu. Hii ni katika hali ambayo wajuzi wa amambo wanasema kuwa ni uingiliaji wa nchi hizo ndio unaochochea na kuvuruga zaidi usalama wa Libya na eneo zima la kaskazini mwa Afrika. Uzoefu unaonyesha wazi kwamba machafuko na ghasia huongezeka katika kila eneo ambalo nchi za Magharibi huamua kutuma huko askari wao kwa kisingizio cha kulinda amani na usalama wa maeneo hayo. Hali hiyo inaonekana wazi huko kaskazini mwa Mali ambako ghasia na machafuko yameongezeka kufuatia kutumwa huko askari wa Ufaransa kwa kisingizio cha kupambana na makundi ya kigaidi. Hivi sasa upinzani mkubwa unatolewa dhidi ya uingiliaji wa kijeshi wa Ufaransa na Uingereza katika bara la Afrika, uingiliaji ambao kimsingi unafanywa kwa lengo la kulinda maslahi ya nchi hizo za kikoloni na wala sio kulinda maslahi ya mataifa ya Kiafrika.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO