Thursday, January 31, 2013

MAOMBI YA NAFASI ZA MAFUNZO MWAKA WA MASOMO 2013/14


JAMHURI YA MUUNGANO YA TANZANIA
WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII

MAOMBI YA NAFASI ZA MAFUNZO MWAKA WA MASOMO 2013/14

Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii anakaribisha maombi ya kujiunga na kozi mbalimbali zinazotolewa na Wizara kwa mwaka wa masomo 2013/2014.

1.      Kozi zinazotangazwa ni:  

A.    Ngazi ya Stashahada:
(i)             Afisa Afya ya Mazingira (Assistant Health Officer)
(ii)           Fiziotherapia (Physiotherapy)
(iii)          Fundi Sanifu Meno (Dental Laboratory Technologist)
(iv)          Mteknolojia Maabara (Laboratory Technician)
(v)           Optometria (Optometry)
(vi)          Tabibu (Clinical Officer)
(vii)        Tabibu Meno (Dental Therapist)
(viii)       Uuguzi Daraja ‘’A’’ (Diploma in Nursing)

B.    Ngazi ya Cheti

(i)             Fundi Sanifu Maabara Msaidizi (Laboratory Assistants)
(ii)           Mtunza kumbukumbu za Afya (Health Record Technicians)
(iii)          Tabibu Msaidizi (Clinical Assistants)
(iv)          Uuguzi Daraja ‘’B’’ (Certificate in Nursing)

C.    Mafunzo ya Tabibu kwa njia ya masafa (Distance Learning) kwa wale waliohitimu mafunzo ya Tabibu Msaidizi mwaka 2009.

2.     Muda wa Mafunzo:
(i)             Miaka mitatu kwa kozi za Stashahada
(ii)           Miaka miwili kwa kozi za Ngazi ya cheti

3.     Sifa za Muombaji:
Waombaji watarajali (Pre-service):
(i)             Awe raia wa Tanzania
(ii)           Awe amemaliza kidato cha nne au sita kati ya mwaka 2008 na kuendelea
(iii)          Ufaulu wa kidato cha nne uwe wa kiwango kisichopungua alama ya ‘C’,  katika  masomo ya Biologia na Kemia , na alama ‘D’ kwa somo la Fizikia kwa kozi za Stashahada . Alama hizi zipatikane katika kikao kimoja tu cha mitihani.
(iv)          Cheti chake cha kidato cha nne, kionyeshe ufaulu usiopungua point 28 kwa kozi za cheti. Aidha ni lazima awe na ufaulu usiopungua (minimum) alama ‘D’, kwa masomo ya Biologia, Kemia na Fizikia. Alama hizi zipatikane katika kikao kimoja tu cha mtihani.
(v)           Kwa wale waliomaliza kidato cha sita na wanaohitaji kujiunga na mafunzo ya stashahada, wawe na alama isiyopungua ‘E’,  kwa masomo ya Biologia, Kemia na Fizikia. Ufaulu huu uwe umepatikana katika kikao kimoja tu cha  mtihani.
(vi)          Kufaulu somo la Kiingereza na Hisabati ni sifa ya nyongeza.


Waombaji wa Mafunzo ya Masafa (Distance learning:
A.    Wanaotakiwa kujiunga na Bridging course kabla ya kuendelea na masomo ya NTA 6 (Clinical Officer)
               i.         Awe amemaliza kidato cha nne na kupata ufaulu wa angalau alama “D” katika masomo manne
              ii.         Awe na cheti cha kuhitimu mafunzo ya waganga wasaidizi vijijini mwaka 1999 na kurudi nyuma.
B.     Tabibu wasaidizi (NTA 5) Wanaotakiwa kuendelea na masomo ya NTA 6 (Clinical Officer)
               i.         Awe amemaliza kidato cha nne na kupata ufaulu wa angalau alama “D” katika masomo manne.
              ii.         Awe na cheti cha kuhitimu mafunzo ya Tabibu wasaidizi (NTA 5) mwaka 2009.
4.     Utaratibu wa kutuma maombi:
(i)    Fomu za maombi zitapatikana kwa wakuu wa kanda za mafunzo zilizoainishwa hapo chini (rejea kipengele Na. viii) chini, Waganga Wakuu wa wilaya na wakuu wa vyuo vya afya vilivyo chini ya Wizara.
(ii)  Waombaji wote watalipia fomu kwa sh. 15, 000/=. Risiti halisi ya Benki kwa ajili ya malipo haya, iwasilishwe pamoja na fomu za maombi. Kiasi hiki cha fedha hakitarejeshwa (Non refundable).
(iii)Malipo  yaingizwe kwenye akaunti ,Health Service fund’, Account No. 0111-030-12059 NBC – CORPORATE BRANCH.
(iv)Maombi yatakayopokelewa na kufanyiwa kazi, ni yale yatakayoambatanishwa na risiti halisi ya malipo ya Benki,  inayoonyesha kiwango cha malipo kilichotajwa hapo juu.
(v)  Maombi ambayo hayataambatanishwa na hati ya malipo ya Benki(Pay  in Slip) na kivuli cha cheti cha Baraza la Mitihani cha kuhitimu Elimu ya Sekondari, hayatafanyiwa kazi.
(vi)Maombi yote yatapokelewa kupititia kanda za mafunzo baada ya malipo kufanyika kwenye akaunti iliyotajwa hapo juu.
(vii)      Fomu za maombi zijazwe na zitumwe kwa Katibu Mkuu,  wizara ya afya na ustawi wa jamii,kupitia anwani za wakuu wa kanda kulingana na eneo muombaji alipo.
(viii)    Anwani za Wakuu wa Kanda ni kama zilivyoainishwa hapa chini:-
a)      Mratibu wa Kanda ya Mashariki (Mikoa ya Morogoro na Pwani) - Chuo cha Mafunzo ya Afya ya Jamii – S.L.P. 1060, Morogoro.
b)     Mratibu wa Kanda ya Magharibi (Mikoa ya Kigoma na Tabora) – Chuo cha Tabibu Wasaidizi, S.L.P. 458, Kigoma
c)      Mratibu wa Kanda ya Kusini (Mikoa ya Lindi na Mtwara)– Chuo cha Tabibu, S.L.P. 86, Mtwara.
d)     Mratibu wa Kanda ya Kaskazini (Mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga)– Chuo cha CEDHA, S.L.P.1162, Arusha..
e)      Mratibu wa Kanda ya Nyanda za Juu kusini Magharibi (Mikoa ya Rukwa na Mbeya) – Chuo cha Madaktari Waasaidizi, S.L.P. 1142, Mbeya.
f)       Mratibu wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mikoa ya Ruvuma na Iringa)– Chuo cha Afya ya Jamii, S.L.P. 235, Iringa.
g)     Mratibu wa Kanda ya Kati (Mikoa ya Singida na Dodoma) – Chuo cha Uuguzi Mirembe, S.L.P. 595, Dodoma.
h)     Mratibu wa Kanda ya Ziwa (Mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera na Shinyanga) – Chuo cha Madaktari Wasaidizi, S.L.P. 11351, Mwanza.
i)      Mkurugenzi wa Taasisi za Sayansi Shiriki za Afya Muhimbili, S.L.P 65005, Dar-es-salaam.

5.     Utaratibu wa kutoa taarifa kwa waliochaguliwa:
a)     Wizara itakuwa na wajibu wa kuwataarifu wale wote watakaofanikiwa kuchaguliwa kujiunga na kozi mbalimbali kupitia magazeti, ‘website’ ya Wizara na mbao za matangazo Wizarani.  
b)     Taarifa hizo zitatumwa pia kwenye kanda za mafunzo kama zilivyoainishwa hapo juu.

6.     Mwisho wa kupokea maombi ni tarehe 30 Aprili, 2013.
7.     Muhula wa masomo unatarajiwa kuanza tarehe 1 Oktoba, 2013.

Imetolewa na:
Katibu Mkuu,
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,
S.L.P. 9083,
Dar es Salaam

BREAKING NEWS

Jahazi la SUNRISE lililobeba abiria wapatao 35 limezama Nungwi Visiwani Zanzibar. Watu wapatao 20 wameokolewa na wengine wapatao 15 hawajulikani walipo. Jahazi hilo lilitokea kutokea Tanga, na lilikuwa ni la mizigo
Chanzo ITV breaking news, saa 3:37 jioni, leo tar.31/01/2013

 sOURCE: http://www.jamiiforums.com/jukwaa-la-siasa/393678-jahazi-lazama-nungwi-zanzibar-leo.html

DAVID CAMERON ZIARANI LIBYA

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, amefanya ziara ya kushitukiza nchini  Libya hivi leo, ziara  inayokuja  siku chache  baada  ya  Uingereza  kutoa  tahadhari  kuhusu vitisho  vinavyoukabili  ubalozi  wake  mjini  Tripoli. Cameron amewasili  mchana  wa  leo huku  kukiwa  na ulinzi  mkali. Akiongozana  na   waziri  wa  mambo  ya ndani  wa  Libya  Ashur Shwayel, Cameron  alikwenda moja  kwa  moja  katika  chuo  cha  mafunzo  ya  polisi kusini  mwa  mji  mkuu  Tripoli, ambako  alihudhuria sherehe  ya kupandishwa  vyeo kwa maafisa wa polisi. Maafisa  wa  serikali  ya  Libya wameliambia  shirika  la habari  la  AFP  kuwa  ushirikiano  katika  nyanja  ya usalama  utakuwa  katika  ajenda  ya  juu  katika mazungumzo  baina  ya  Cameron  na  maafisa  wa  Libya. Ofisi  ya  waziri  mkuu  mjini  London  imesema  kuwa Cameron  amekwenda  nchini  Libya  kujadiliana  juu  ya namna Uingereza  inavyoweza  kuendelea kusaidia  ujenzi wa  Libya imara, yenye  maendeleo  na  demokrasia.

ISRAEL HAIWEZI KUSIMAMISHA MPANGO WA NYUKLIA WA IRAN


Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa Utawala wa Kizayuni wa Israel amekiri kuwa utawala huo hauna uwezo wa kusimamisha mpango wa nyuklia wa Iran wenye malengo ya amani. Akizungumza Jumatano mjini Tel Aviv katika mkutano na ujumbe wa lobi ya Kizayuni Marekani, Netanyahu amekiri kuwa hata Israel ikitumia mbinu za kijeshi haiwezi kusimamisha mpango wa nyuklia wa Iran wenye malengo ya amani. Ikumbukwe kuwa katika uchaguzi wa hivi karibuni wa bunge katika utawala huo, Netanyahu alitumia kadhia  ia ya nyuklia ya Iran kujaribu kupata viti vingi lakini  hakufaulu bali alipata pigo kubwa kuliko uchaguzi uliopita.

Netanyahu ameutaja mwaka wa 2013 kuwa nyeti kuhusu kadhia ya nyuklia ya Iran na ameitaka lobi ya Kizayuni Marekani kutumia ushawishi wake kuishinikiza Marekani izuie mpango wa nyuklia wa Iran wenye malengo ya amani.

WATU 80 WAFARIKI MAFURIKO MSUMBIJI


Mafuriko mapya yameripotiwa nchini Msumbuji ambapo watu saba wameuawa na hivyo kupelekea idadi ya watu waliouawa katika mafurko ya hivi karibuni nchini humo kufika 80 na wengine 250,000 kuachwa bila makao.
Ripoti zinasema kuwa mvua kali jana Jumatano zilipelekea karibu watu 17 elfu kuondoka makwao kati kati mwa jimbo la Zambezia na mji wa Nampula kaskazini mwa nchi hiyo. Imearifiwa kuwa mwanamke mmoja mjamzito amejifungua juu ya paa la nyumba. Mama huyo aliyetambulika kwa jina la Hortensia ni mkazi wa wilaya ya Chokwe nchini Msumbiji, moja ya maeneo yaliyoathirika zaidi na mafuriko hayo. Ripoti zinasema Hortensia alijifungua salama mtoto wa Kike akiwa juu ya paa. Maafisa wa hali ya hewa wameonya uwezekano wa kutokea mvua kubwa zaidi na wamewataka wakazi wa maeneo yaliyokumbwa na maafa kuchukua tahadhari.

UINGEREZA YATUMA JESHI NCHINI MALI


Serikali ya London imethibitisha kwamba imetuma askari wasiopungua 350 nchini Mali na katika nchi jirani na nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika. Waziri wa Ulinzi wa Uingereza Philip Hommond amesisitiza tena bungeni juu ya uungaji mkono kikamilifu wa serikali ya London kwa mashambulizi ya Ufaransa nchini Mali. Awali viongozi wa Uingereza walisema kuwa watatoa msaada wa kilojistiki tu kwa Ufaransa katika mashambulizi yake kijeshi huko Mali. Kupanuliwa ushiriki wa Uingereza katika mashambulizi ya kijeshi nchini Mali kunafanyika katika hali ambayo, wanaharakati wanaopinga vita wanalaani mashambulizi ya kijeshi ya Ufaransa nchini humo na kusema kuwa ni vita vya kikoloni. Vilevile wameitaka serikali ya London iache kuunga mkono vita hivyo. Waziri wa Ulinzi wa Uingereza anajitahidi kuhalalisha hatua ya nchi hiyo ya kutuma majeshi huko magharibi mwa Afrika kwa kuhusisha usalama wa Mali na amani ya nchi za Ulaya. Hammond pia amesisitiza kwamba, Ufaransa tangu ilipoanza mashambulizi ya kijeshi huko Mali Januari 11 haijaungwa mkono na nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.
Waziri wa Ulinzi wa Uingereza alitoa matamshi hayo bungeni baada ya kuzungumza kwa simu na Rais François Hollande wa Ufaransa, ili kujaribu kuisaidia serikali ya Paris ambayo inaonekana kuwa imetengwa na nchi nyingine katika suala hilo. Kabla ya kuishambulia Mali, Ufaransa pia ilijitahidi kuonyesha kuwa eneo la magharibi mwa Afrika la nchi za Mali, Algeria, Mauritania na Niger limekuwa kituo na hifadhi ya makundi yaliyofurutu ada ya kigaidi kama lile la waasi wa Kituareg. Hatua ya Poland ya kutuma wataalamu wa kijeshi nchini Mali pia imetekelezwa kwa kisingizio hicho.
Kwa mujibu wa azimio lililopasishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu uingiliaji wa kijeshi nchini Mali, operesheni hiyo ilipaswa kutekelezwa chini ya usimamizi wa jumuiya ya kieneo ya Ecowas na Umoja wa Afrika kwa mwongozo wa jeshi la Mali. Licha ya hayo, Ufaransa ambayo inakabiliwa na matatizo ya kiuchumi iliingilia kijeshi mgogoro wa Mali, bila ya kuwasiliana na viongozi wa AU na nchi jirani na Mali. Mwezi Disemba mwaka jana baadhi ya duru zilieleza kuwa kumefanyika mazungumzo ya siri kati ya Marekani na Ufaransa kuhusu hali ya Mali na kuna uwezekano mkubwa ndio yaliyoratibu mashambulizi ya kijeshi ya Paris nchini Mali.
Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron amefanya safari nchini Algeria ili kuratibu ushirikiano zaidi na serikali ya Algiers katika kuwasaidia askari wa Ufaransa nchini Mali. Hata hivyo huenda serikali ya Algiers isikubali suala hilo hasa baada ya tukio la utekeaji nyara katika kiwanda cha gesi cha In Amenas uliochochewa na mashambulizi hayo ya Ufaransa nchini Mali.

ARGENTINA YAKATAA OMBI LA ISRAEL KUHUSU IRAN


Argentina imekataa ombi la Israel la kutaka ipewe maelezo juu ya makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni kati ya nchi hiyo na Iran ya kuchunguza mlipuko wa mwaka 1994 huko Buenos Aires ulioua watu 85. Wizara ya Mambo ya Nje ya Argentina imesema, ombi hilo la Israel si sawa na linapingwa vikali. Taarifa ya wizara hiyo imesema, shambulio la kigaidi la Julai 18, 1994 halikumhusu hata raia mmoja wa Israel kwani wahanga wote walikuwa raia wa Argentina, Bolivia, Poland na Chile.
Jumapili iliyopita Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Ali Akbar Salehi na mwenzake wa Argentina walisaini makubaliano ya maelewano kati ya pande mbili kuhusiana na kuchunguzwa zaidi mashambulizi hayo ya kigaidi yaliyotokea huko Buenos Aires mwaka 1994. Huko nyuma na chini ya mashinikizo ya Marekani na Israel Argentina iliituhumu Iran kuhusika katika mashambulizi hayo, madai ambayo yalikanushwa vikali na Tehran.

NIGERIA KUPOKEA NDEGE ZA KUJASUSI TOKA MAREKANI


Waziri wa Ulinzi wa Niger ametangaza kwamba, nchi yake ipo tayari kuanzisha kituo cha ndege zisizo na rubani za Marekani ili kuisaidia Washington kufanya ujasusi barani Afrika. Karidjo Mahamadou amesema, nchi hiyo pia itakubali msaada wa ndege kwa ajili ya kusimamia harakati zinazotia shaka nchini Mali. Hata hivyo amesema kuwa, hana taarifa juu ya makubaliano yoyote kati ya nchi yake na Marekani kwa ajili ya kupelekwa ndege kama hizo nchini Niger.
Iwapo mpango huo utatekelezwa, utadhihirisha hatua nyingine ya Marekani ya kutaka kujiimarisha kijeshi barani Afrika.
Marekani hivi karibuni ilitangaza mpango wa kupeleka vikosi maalumu vya jeshi katika nchi 35 za Kiafrika.  Marekani ina kituo cha kudumu cha kijeshi nchini Djibouti.

ISRAEL YASHAMBULIA KITUO CHA UTAFITI CHA SYRIA


Jeshi la Syria limetangaza kuwa watu wawili wameuawa na wengine watano kujeruhiwa baada ya ndege za kijeshi za utawala wa Kizayuni wa Israel kushambulia kituo cha utafiti wa sayansi cha Jamraya karibu na mji mkuu Damascus.
Taarifa ya jeshi la Syria imeeleza kuwa, ndege za Israel zilikiuka anga ya Syria jioni ya Jumatano na kushambulia moja kwa moja kituo cha utafiti wa sayansi ambacho kinaisaidia Damascus kuimarisha muqawamma na kujilinda. Utawala wa Kizayuni umedai kwamba ulilenga msafara uliokuwa umebeba silaha za kemikali nchini Syria. Jeshi la Syria limesema, mashambulizi hayo ni mfano mwingine wa jinai za Israel na utumiaji mabavu dhidi ya Waarabu na Waislamu.

WAPINZANI MISRI WATAKA MAZUNGUMZO NA MURSI


Muhammad al Baradei shakhsia wa upinzani nchini Misri ametaka kufanyike mazungumzo ya haraka kati ya makundi ya kisiasa na Rais Muhammad Mursi wa nchi hiyo ili kuhitimisha mgogoro wa kisiasa nchini humo. Al Baradei amesema kuwa harakati ya upinzani ya National Salvation Front inataka kufanyike mazungumzo ya haraka na Rais, pamoja na Mawaziri wa Ulinzi na Mambo ya Ndani ili kukomesha machafuko na kuanza mazungumzo ya kitaifa.
Wito huo umetolewa siku mbili baada ya kundi hilo la upinzani kukataa mwaliko wa Rais wa Misri wa mazungumzo ya kutatua matatitizo ya kisiasa na machafuko. Machafuko yalianza tena hivi karibuni katika miji kadhaa ya Misri baada ya mahakama ya nchi hiyo kutoa hukumu ya kunyongwa watu 21 waliohusika na tukio lililopelekea kupoteza maisha watu 74 baada ya mechi ya soka mwaka jana katika mji wa Port Said.

Wednesday, January 30, 2013

WATU SITA WAUAWA NA WAZIRI ANUSURIKA SOMALIA


Watu wasiopungua sita wameuawa kufuatia mlipuko wa bomu nje kidogo ya ofisi ya Waziri Mkuu wa Somalia mjini Mogadishu.
Hujuma hiyo imejiri leo Jumanne mchana ambapo kati ya waliouawa ni maafisa wa usalama. Imearifiwa kuwa mtu aliyekuwa amejifunga mshipi wa bomu alijiripua karibu na ofiisi ya Waziri Mkuu Abdi Farah Shirdon katika eneo la kati kati mwa Mogadishu. Maafisa wa usalama wanasema waziri mkuu alikuwa ofisi wakati wa tukio hilo lakini hakujeruhiwa. Hakuna kundi lolote lililodai kuhusika na mripuko huo lakini kundi la kigaidi la al-Shabab limeapa kuipundua serikali ya Somalia.

WANAMGAMBO WA ALQAEDA WAUAWA YEMEN

Jeshi la Yemen limefanya mashambulizi kwenye maficho ya mtandao wa al Qaeda na kuwaua wanamgambo 16 wa kundi hilo. Jeshi la Yemen jana liliwaua wanachama 16 wa al Qaeda baada ya kushambulia maficho ya kundi hilo katika eneo la Manaseh katika mkoa wa Bayda. Katika mashambulizi hayo wanajeshi wawili wa Yemen pia waliuliwa. Jeshi la Yemen lilifanya shambulio hilo dhidi ya maficho ya wapiganaji wa al Qaeda katika mkoa wa bayda kwa lengo la kuwakomboa raia wa nchi za Ulaya waliokuwa wametekwa nyara na kundi hilo.  Jana hiyo hiyo askari polisi usalama wa Yemen wasiopungua 11 waliuawa baada ya gari lililokuwa limetegwa bomu kulipuka karibu na kituo kimoja cha kijeshi cha upekuzi  katika mji wa Rida'a umbali wa kilomita 160 kusini mwa Sana'a mji mkuu wa Yemen.

JESHI LA SEPAH LAFANYA MAZOEZI GHUBA YA UAJEMI


Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC kimeanza maneva ijulikanayo kama 'Fat'h 91' katika Ghuba ya Uajemi. Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars, mazoezi hayo yameanza leo Jumatano na yataendelea kwa siku tatu kwa lengo la kuimarisha mipango ya kujihami na kukabiliana na vitisho kwa kutumia mbinu zisizo za kawaida.
Aidha katika luteka hiyo maafisa wenye uzoefu IRGC watatoa mafunzo kwa kizazi kipya. Kamanda wa Eneo la Tatu la Kitengo cha Wanamaji cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu Admeli Seifullah Bakhtiarivan amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina uwezo mkubwa wa kijeshi. Amesema Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu wanatumia stratijia ya kujihami ya pande zote kwa kuzingatia hali hatari zaidi inayoweza kujitokeza. Hivi karibuni pia Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lilifanya mazoezi makubwa katika eneo pana la fukweni, baharini na angani kwenye lango la Hormuz, Bahari ya Oman, kaskazini mwa Bahari ya Hindi, Ghuba ya Aden na lango la Babul Mandab. Wakuu wa vikosi vya kijeshi vya Iran wanasisitiza mara kwa mara kuwa mazoezi ya jeshi la Iran yana ujumbe wa urafiki na udugu kwa mataifa rafiki na onyo kali kwa maadui.

BOKO HARAM WATAKA USITISHAJI VITA


Mmoja kati ya makamanda wa kundi la Boko Haram nchini Nigeria ametaka kusitishwa vita na serikali ya nchi hiyo. Akizungumza kwa niaba ya kiongozi wa kundi la Boko Haram Abubakar Shikau, Sheikh Abu Muhammad bin Abdulaziz amesema kuwa, uamuzi huo umechukuliwa kufuatia uharibifu mkubwa na maafa wanayopata wananchi wasio na hatia. Ameongeza kuwa, uamuzi huo pia unatokana na mazungumzo yaliyofanyika hivi karibuni kati ya kundi hilo na viongozi wa jimbo la Borno ambalo ni chimbuko la kundi hilo. Kundi la Boko Haram limetoa ujumbe likiwataka wafuasi wake waweke chini silaha zao.
Kwa upande mwingine, serikali ya Nigeria imekataa kuzungumza chochote kuhusiana na taarifa hiyo iliyotolewa na kundi la Boko Haram la kusitisha mapigano. Mashirika ya Kutetea Haki za Binadamu yanasema kuwa, maelfu ya watu wameuawa na majengo kadhaa ya serikali kama vile, mashule, mahospitali na vituo vya polisi kubomolewa tokea yalipoanza mashambulizi ya kundi la Boko Haram mwaka 2009.

WAMAGHARIBI WAZUSHA HITILAFU BAINA YA WAISLAM


Mjumbe wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Kigeni katika Bunge la Iran amesema kuwa, nchi za Magharibi zinazusha hitilafu baina ya Waislamu kwa lengo la kuvuruga na kutokomeza umoja na mshikamano wa Waislamu.
Akielezea njama zinazofanywa na  nchi za Magharibi kwa lengo la kuzusha mifarakano kati ya Waislamu ulimwenguni, Ahmad Bakhshayesh Ardistani ameongeza kuwa, awali Marekani ilikuwa ikiyaunga mkono makundi ya kigaidi kama al Qaeda na hivi sasa inatuma majeshi yake kwenye nchi mbalimbali duniani kwa kisingizio eti cha kupambana na makundi hayo. Ardistani ameongeza kuwa, mifarakano mingi inayojitokeza katika ulimwengu wa Kiislamu, inasababishwa na umasikini wa kiutamaduni wa baadhi ya jamii ya Waislamu unaowatumbukiza Waislamu kwenye mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

Sunday, January 27, 2013

MATEKA WAACHILIWA HURU NIGER DELTA

Jeshi la Nigeria likipiga doria katika Niger Delta


Mabaharia watano wa India waliotekwa nyara mwezi uliopita nje ya mwambao wa Nigeria wameachiliwa huru, kwa mujibu wa kampuni yao. Mabaharia hao wa meli ya mafuta walitekwa wakati watu waliojihami na silaha tele walipoingia kwa nguvu ndani ya meli yao, SP Brussels, katika eneo la mafuta la Niger Delta kusini mwa Nigeria.
Taarifa ya kampuni ya meli hiyo, Medallion Marine, ilieleza kuwa mabaharia hao ni wazima lakini haikueleza iwapo ililipa kikombozi.

IRAN KUTOZIUZIA MAFUTA NA GESI BAADHI YA NCHI

Msemaji wa Wizara ya Mafuta nchini Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeamua kusimamisha kuziuzia mafuta ghafi na gesi baadhi ya nchi za Ulaya baada ya nchi hizo kuchukua hatua za kindumakuwili dhidi ya taifa hili. Ali Nikzad amesema kuwa, vikwazo hivyo vya Tehran dhidi ya nchi hizo za Ulaya, vinakuja sambamba na kuongezeka usafirishaji wa mafuta na gesi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuelekea nchi tofauti  za dunia na kwamba, nchi 27 ambazo ni wanachama wa Umoja wa Ulaya zimepigwa marufuku na Tehran kununua bidhaa hiyo muhimu. Aidha akiashiria kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mzalishaji wa pili wa mafuta katika Jumuiya ya Nchi Zinazozalisha Mafuta kwa Wingi Duniani OPEC Nikzad amesema, Iran imechukua hatua hiyo dhidi ya baadhi ya nchi za Ulaya kufuatia kupitishwa kwa duru ya pili ya vikwazo vya mafuta na gesi dhidi yake. Amesema kuwa, vikwazo hivyo vya Tehran dhidi ya nchi hizo za Ulaya vitaendelea hadi pale umoja huo utakapoachana na siasa zake za kiuadui na kubadilisha miamala yake ya kijuba dhidi Iran.

VITONGOJI VINAZUIA KUUNDWA TAIFA LA PALESTINA

Balozi wa Jordan nchini Marekani amesema kuwa, kuendelea ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi huko katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, kunazuia kuundwa kwa taifa huru la Palestina. Mwana mfalme Zaid bin Ra'ad aliyasema hayo jana katika mahojiano aliyofanyiwa na televisheni ya Bloomberg na kusisitiza kuwa, kuendelea kwa ujenzi huo wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, kunalifanya suala la kuundwa taifa la Palestina kuwa lisilowezekana. Amesema, kuongezeka nafasi ya haki ya taifa la Palestina katika Umoja wa Mataifa, kunaonyesha mustakbali mzuri kwa Wapalestina na kwamba, kwa hatua hiyo Wapalestina wataweza kuiweka Israel katika mashinikizo. Aidha kiongozi huyo wa Jordan amesema kuwa, Wapalestina sasa wanaweza kuuburuza utawala bandia wa Kizayuni katikaMahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC. Hivi karibuni Mjumbe mwandamizi wa Harakati ya Palestina Fat'h anayeshughulikia masuala ya utungaji sheria alikosoa vikali hatua ya kuendelea ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na kuitaka Kamisheni ya siasa za Mambo ya Nje ya Umoja wa Ulaya kuitisha kikao mwezi Machi na kujadili kwa kina suala hilo.

SHIRIKA LA MAFUTA LA UFARANSA KUNUNUA MAFUTA TOKA IRAN

Shirika la mafuta la Ufaransa na Korea Kusini lijulikanalo lama Samsung Total limeanza tena kununua mafuta ghafi ya petroli ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, baada ya kupata hasara kubwa iliyotokana na vikwazo vya upande mmoja vya nchi za Magharibi hasa Marekani dhidi ya Iran. Ripoti hiyo imeongeza kwa mashirika hayo yalipata hasara baada ya kuzuiwa kununua mafuta ya Iran. Hasara hiyo inayokadiriwa kufikia kiasi cha zaidi ya dola milioni 6.5, hali iliyoyalazimu kuachana na mashinikizo ya Marekani na Magharibi na hivyo kuanza tena shughuli za ununuzi wa mafuta ya nchi hii. Hatua hiyo inahesabiwa kuwa moja ya hatua za kususia vikwazo dhidi ya mafuta ya Iran kwa wateja wa mafuta hayo, sambamba na kuendelea mbinyo wa Wamagharibi kwa wateja wa Tehran. Baada ya kusimamishwa bidhaa ya mafuta ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwenda kwa wateja wake kama vile Japan na Korea Kusini, wateja mbalimbali wa bidhaa hiyo muhimu wameanza kufuatilia njia za ununuzi wa mafuta ya Iran mbali na vikwazo hivyo vya maadui wa Tehran.

WATU KADHAA WAUAWA MISRI BAADA YA MAANDAMANO YA KUPINGA HUKUMU YA KIFO KWA WENZAO

Wizara ya Afya ya nchini Misri imetangaza kuwa, watu 40 wameuawa na wengine 277 wamejeruhiwa kufuatia ghasia zilizoibuka jana nchini humo. Machafuko hayo yalijiri baada ya Mahakama ya Jinai ya nchi hiyo kutoa hukumu ya kifo kwa watu 21 waliopatikana na hatia ya kushiriki katika ghasia za Februari mwaka jana mjini Port Said katika uwanja wa soka baada ya mechi iliyozikutanisha klabu mbili za al Ahly na al Masry. Jeshi la Misri limeimarisha doria Port Said ili kurejesha hali ya amani na usalama. Waandamanaji waliokuwa na hasira kali walishambulia na kuteketeza moto ofisi kadhaa mjini hapo ikiwemo jela na jengo la shirika la umeme. Ghasia hizo zilizuka baada ya kundi moja la waandamanaji kuvamia gereza linalosadikiwa kuwa na watuhumiwa hao na kuanza kuwafyatulia risasi askari wa usalama. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri imetangaza kuwa, askari kadhaa wameuawa na wengine 150 wamejeruhiwa katika tukio hilo. Ghasia hizo zimempelekea Rais Muhammad Mursi wa nchi hiyo kufuta safari yake mjini Addis Ababa Ethiopia kwa ajili ya kushiriki mkutano wa wakuu wa Umoja wa Afrika.

Saturday, January 26, 2013

GAZETI LA ANNUUR

MAANDAMANO YA KUPINGA UTOAJI MIMBA YAFANYIKA MAREKANI


Maelfu ya wanaharakati wa haki za kuishi nchini Marekani jana Ijumaa wamekusanyika kwenye Mahakama Kuu nchini humo kupinga uamuzi wa kihistoria wa miaka 40 iliyopita wiki hii ambao umehalalisha utoaji mimba. Waandaaji wa matembezi ya mwaka kuhamasisha haki ya kuishi,huko Washington kwenye jengo la taifa la manunuzi,walitarajia umati mkubwa kupita ule uliojitokeza mwaka jana wa watu wapatao laki nne pamoja na uwepo wa baridi kali kwa sasa.
Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Benedicto wa 16 ameunga mkono maandamano hayo kwa kutuma ujumbe mfupi kupitia anwani yake ya mtandao wa twiter akiwatakia kila la heri wanaharakati hao na kusema kuwa anawaombea viongozi wa kisiasa ili walinde maisha ya watoto ambao bado hawajazaliwa na kuhamasisha utamaduni wa maisha.

VIKOSI VYA UFARANSA VYASONGA MBELE MALI

Vikosi vya Ufaransa na Mali vimesonga mbele kuelekea ngome muhimu ya waasi wenye itikadi kali za Kiislamu ya Gao, baada ya kuudhibiti tena mji wa kaskazini wa Hombori. Duru za vikosi vya usalama zimeeleza kuwa wanajeshi hao wataelekea Gao, moja ya miji mikubwa mitatu iliyopo eneo la kaskazini, ambako waasi wenye mafungamano na Al-Qaeda wameanzisha sheria ya Kiislamu ya Sharia kwa miezi kumi. Kwa mujibu wa duru hizo, katika eneo la magharibi mwa Mali, vikosi vinavyoongozwa na Ufaransa vinaelekea kwenye mji wa Lere kwa lengo la kuudhibiti mji wa Timbuktu uliopo kaskazini. Wakati huo huo, wakuu wa majeshi wa nchi za Afrika Magharibi wanakutana leo mjini Abidjan, Cote d'Ivoire katika kikao cha dharura kujadili operesheni za kijeshi nchini Mali zenye lengo la kuwaondoa waasi hao, ambapo watatathmini mchakato unaoendelea wa kupeleka vikosi vya kimataifa nchini Mali vinavyoongozwa na Afrika vya AFISMA. Aidha, viongozi wa Umoja wa Afrika wanatarajia kukutana Jumanne ijayo katika mkutano wa wafadhili ili kujadiliana kuhusu suala la kuongeza fedha katika operesheni za Mali. Mkutano huo utawajumuisha wawakilishi kutoka Umoja wa Ulaya na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

WATANO WAUAWA MISRI KWENYE MAANDAMANO


Taarifa kutoka nchini Misri zinaeleza kuwa watu watano wameuawa na wengine kwa mamia wamejeruhiwa wakati wa maandamano ya kuadhimisha miaka miwili ya mapinduzi yaliyouondoa madarakani utawala wa Hosni Mubarak. Polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi dhidi ya waandamanaji waliokuwa nje ya makaazi ya rais mjini Cairo. Ghasia zilizosababisha vifo na majeruhi hao zimetokea mjini Cairo na Alexandria pamoja na miji mingine ya Misri. Rais Mohammed Morsi ametoa wito wa kuwepo utulivu baada ya ghasia kati ya wapinzani na askari polisi.
Maandamano hayo yaliyoitishwa na viongozi wa upinzani yanaipinga serikali ya Rais Morsi aliyechaguliwa kwa kuzingatia demokrasia na anayeungwa mkono na vyama vya itikadi kali za Kiislamu. Upinzani unamshutumu Rais Morsi kwa kusaliti mapinduzi hayo.

MMAREKANI AHUKUMIWA MIAKA 494 JELA

Mahakama katika jimbo la Pennsylvania nchini Marekani imemuhukumu Walter Meyerle mwenye umri wa miaka 36 adhabu ya kifungo cha miaka 494 jela, baada ya kupatikana na kosa la kubaka na kuwadhalilisha kijinsia watoto 15 nchini humo. Mahakama hiyo imeeleza kuwa, kuanzia mwaka 1997 hadi 2010 Walter Meyerle aliwabaka watoto wavulana na wasichana wenye umri wa kati ya miaka  4 na 17. Mwendesha mashtaka wa kesi hiyo amesema kuwa, idadi kubwa ya watoto hao waliofanyiwa unyama huo walikuwa ni watoto wa marafiki zake. Wakati huohuo, Mahakama ya Chicago imempiga faini ya dola laki tano  mwalimu Kevin Jones baada ya kupatikana na hatia ya kuwadhalilisha wanafunzi wake. Mmoja kati ya mwanafunzi aliyekuwa mhanga wa kutumiwa vibaya kijinsia na mwalimu Kevin Jones alitoa ushadidi wake huo kwenye mahakama hiyo.

HATUA YA KOREA KASKAZINI KUJARIBU SILAHA ZAKE YATIA KIWEWE NCHI ZA MAGHARIBI

Hatua ya jana ya Korea Kaskazini ya kutangaza nia yake ya kufanyia majaribio ya nyuklia kama hatua ya kukabiliana na vitisho vya Marekani, imeutia kiwewe na woga mkubwa Umoja wa Ulaya na Marekani. Bi. Catherine Ashton, Mkuu wa Siasa za Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya, ameitaka Korea Kaskazini kuachana na nia yake hiyo na kufuata mkondo wa kisiasa na kufanya mazungumzo na jamii za kimataifa. Jana ikulu ya Marekani pia ilitangaza kuwa, mpango wa Korea Kaskazini wa kufanya majaribio ya nyuklia, unatia wasiwasi mkubwa na kwamba, hatua hiyo itapelekea kutengwa kimataifa nchi hiyo. Msemaji wa Ikulu ya Marekani Jay Carney aliwaambia waandishi wa habari kuwa, hatua ya Pyongyang ya kutangaza nia yake kufanya majaribio ya nyuklia, inapingana na azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Kwa upande wake Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Hung Lee, amezitaka nchi husika kukaa kwenye meza ya mazungumzo na Korea Kaskazini na kusisitiza kuwa, hiyo ndio njia pekee ya kumaliza mzozo uliopo. Hii ni katika hali ambayo, hivi karibuni Washington ilifanya jaribio la silaha za maangamizi ya umati chini ya ardhi huku jamii ya kimataifa ikiendelea kuwa bubu mbele ya hatua kama hizo za Marekani.

MAREKANI HAWAJAAFIKIANA KUHUSU SILAHA


Duru za habari kutoka Marekani zinaarifu kuwa, wapingaji na waungaji mkono wa uuzwaji silaha za moto nchini humo wameshindwa kuafikiana kuhusiana na kadhia ya kupiga marufuku uuzaji wa silaha hizo nchini humo. Duru za habari kutoka Congress ya Marekani zinasema kuwa bunge hilo Marekani linajadili muswada wa marufuku ya uuzwaji silaha unaofahamika kwa jina la Fainstein, ambao kama utapitishwa utapiga marufuku uuzwaji wa aina 160 ya silaha kwa raia nchini humo. Mkuu wa Kamisheni ya Wananchi mjini New York anayehusika na mpango wa kukabiliana na vitendo vya jinai Richard Aybom amesema kuwa, muswada wa huo wa Fainstein ni moja ya juhudi za Rais Barack Obama wa Marekani za kupunguza vitendo vya mauaji vilivyoshika kasi zaidi katika siku za hivi karibuni nchini humo. Wakati huo huo Eric Pratt Kiongozi Mkuu wa Mahusiano ya Umma katika Taasisi inayohusika na watu wanaomiliki silaha nchini Marekani amesema kuwa, kwa uzoefu wake muswada huo hauwezi kumaliza vitendo vya jinai na mauaji vinavyotokana na silaha zinazomilikiwa na raia nchini Marekani.

NAFASI YA WAISLAM NA KATIBA MPYA TANZANIA - USTADH ILUNGA


Friday, January 25, 2013

MAJESHI YA CHAD YAWASILI NIGER KUELEKEA MALI

Kundi kubwa la magari ya deraya na magari mengine yaliyobeba askari wa Chad kuelekea nchini Mali, limewasili mji mkuu wa Niamey nchini Niger. Vikosi hivyo vya Chad vinaelekea nchini Mali kwa ajili ya kushiriki katika oparesheni za kijeshi dhidi ya waasi wa nchi hiyo wanaoyadhibiti maeneo ya kaskazini. Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na serikali ya Chad, vikosi hivyo vitaweka kambi katika mji wa Ouallam uliopo umbali wa kilometa 100 kaskazini mwa mji mkuu wa Niger, Niamey. Askari wa Niger wapatao 500 wapo katika eneo la mpakani. Hii ni katika hali ambayo, hadi sasa Chad ina wanajeshi wapatao 400 huko Niger. Hatimaye askari wa Chad na Niger wataelekea nchini Mali na kupiga kambi katika mji wa Gao kaskazini mwa nchi hiyo. Utumwaji wa askari hao unafanyika chini ya mwamvuli wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika (Ecowas) iliyopitisha azimio la kutumwa askari wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo wapatao 3300 huko nchini Mali kwa ajili ya kuwatokomeza waasi wa kaskazini mwa nchi hiyo.

UFARANSA YAHARIBU VITUO VYA WAASI WA MALI

Ndege za kivita za Ufaransa zimeviharibu vituo viwili vya wapiganaji wa Kiislamu kaskazini mwa Mali, wakati ambapo kuna ripoti kuwa waasi hao wamegawanyika katika makundi mawili, moja likitaka kufanya mazungumzo ili kukomesha mashambulizi dhidi yao. Pia kumekuwepo na taarifa za majeshi ya Mali kufanya mauaji ya kinyama, ambapo kundi moja la haki za binaadamu limesema kuwa watu wasiyopungua 31 waliuawa katika mji wa kati wa Sevare, na maiti zao kutupwa katika visima. Chanzo kutoka duru za jeshi kimesema kuwa mashambulizi ya ndege yaliyofanyika usiku yamelenga vituo vilivyoko Ansongo, kilomita 80 kutoka mji wa Gao, na vituo vya kijeshi vya waasi vilivyoko katika kijiji jirani cha Seyna Sonrai. Jana Alhamisi, kundi jipya lililojitenga na Ansar Deen la Islamic Movement for Azawad, lilisema katika taarifa yake kuwa linapinga itikadi kali na ugaidi, na kwamba limedhamiria kupambana navyo, na kuongeza kuwa linataka suluhu ya muafaka ya mgogoro huo.

AHMED NEJAD ASISITIZA WAISLAM WOTE KUSHIKAMANA

Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewataka Waislamu kote duniani kuungana na kuzima njama za maadui. Rais Ahmadinejad ameyasema hayo leo, katika sherehe za kumalizika kwa mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya vikosi vya majeshi ya nchi za Kiislamu, yaliyofanyika mjini hapa Tehran kwa mnasaba wa kuwadia uzawa wa Mtukufu Mtume Muhammad (SAW) na wiki ya Umoja. Akizungumzia udharura wa kuimarishwa umoja kati ya Waislamu wote duniani Rais Mahmoud Ahmadinejad amesema kuwa, kuibua migongano na mizozo kati ya Waislamu ni mbinu zinazofanywa na maadui kwa ajili ya kuzusha mifarakano kati yao.
Amesema kuwa, maadui mara zote wamekuwa wakifanya njama za kuanzisha mivutano ya kikabila, kikaumu na kimadhehebu na kuongeza kuwa, pamoja na hayo Qur'ani na Mtume Muhammad ni thamani za Waislamu wote duniani bali pia ni kwa ajili ya watu wote wakiwemo wafuasi wa dini tofauti za mbinguni ikiwemo Uyahudi na Ukristo na walimwengu wote kwa ujumla. Kwa upande mwingine Rais Mahmoud Ahmadinejad amesema kuwa, moja ya sababu zinazopelekea kuzushwa mivutano, ni kutokufahamu tafsiri halisi ya Qur'ani na kwamba, suala hilo kwa muda mrefu limekuwa ndio chanzo cha matatizo kati ya Waislamu.

MATAIFA YA MAGHARIBI YATAKA RAIA WAKE KUONDOKA BENGHAZI

Uingereza, Ujerumani, Uholanzi na Australi zimewataka raia wake kuondoka katika mji wa Benghazi mashariki mwa Libya, kutokana na kitisho dhidi ya raia wa nchi za Magharibi, kinachohusishwa na kuingilia kijeshi kwa Ufaransa katika mgogoro wa Mali. Onyo la Uingereza lililotolewa jana Alhamisi liliikasirisha serikali ya Libya, iliyosema kuwa hakukuwa na taarifa mpya za uchunguzi kuhalalisha wasi wasi huo mjini Benghazi. Idara ya mambo ya nje ya Australia imesema kuwa wanatambua tishio maalumu kwa raia wa nchi za Magharibi mjini Benghazi, na kuwataka raia wake kuondoka huko mara moja. Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron alionya wiki iliyopita kuwa kilichotoekea nchini Algeria katika kiwanda cha gesi ni sehemu tu ya vita virefu dhidi ya magaidi wauaji duniani kote. Jana Alhamisi, Ujerumani na Uholanzi pia ziliwaonya raia wake na kuwataka waondoke mara moja kutoka Benghazi. Lakini naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Libya, Abdullah Massoud alielezwa kusikitisha kwake juu ya onyo hizo, na kusema kuwa serikali mjini Tripoli itahitaji maelezo.

MISRI YAUPINGA MKATABA WA AMANI WA CAMP DAVID

Duru za kidiplomasia kutoka Cairo zinaeleza kuwa, serikali ya Misri imetupilia mbali takwa la Marekani la kuitaka serikali hiyo ifungamane kikamilifu na makubaliano ya amani ya Camp David yaliyotiwa saini kati ya Misri na utawala wa Kizayuni wa Israel. Hatua ya serikali ya Misri ya kukataa pendekezo hilo, hivi karibuni ilipelekea hata Washington kutuma ujumbe maalumu ulioongozwa na Seneta John Mc Cain kuwashawishi viongozi wa Cairo kufungamana na makubaliano ya Camp David. Baadhi ya viongozi wa Misri wamesikika wakisema kuwa, siyo jambo la kimantiki kwa Cairo kufungamana na makubaliano hayo.
Makubaliano ya amani ya Camp David yalitiwa saini kati ya Anwar Sadat Rais wa zamani wa Misri na Menachem Begin Waziri Mkuu wa zamani wa utawala wa Kizayuni wa Israel tarehe 17 Septemba 1978, chini ya usimamizi wa Jimmy Carter Rais wa zamani wa Marekani.

UN YARIDHIA DRONE KUTUMWA KONGO

Baraza la Umoja wa Mataifa limeidhinisha matumizi ya ndege zisizo na rubani, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, baada wiki kadhaa za ucheleweshwaji kufuatia wasi wasi wa Urusi, China na Rwanda juu ya matumizi ya ndege hizo za uchunguzi. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ban Ki-Moon aliliandikia Baraza hilo mwishoni mwa mwezi uliyopita, kushauri kuwa walinda amani nchini Kongo wanapanga kutumia ndege hizo kuboresha uwelewa wa hali ya huko na kuharakisha mchakato wa maamuzi katika kushughulikia uasi wa kundi la M23. Rais wa baraza hilo kwa mwezi huu wa Januari, balozi wa Pakistan katika Umoja wa Mataifa Masood Khan amemjibu Katibu Mkuu Ban kuwa wamepokea maombi hayo na kuyaridhia. Lakini baraza hilo limesema ndege hizuo zitatumika tu kwa majaribio.
 

KOREA KASKAZINI YATISHIA KUISHAMBULIA KUSINI

Korea Kaskazini imetishia kuishambulia Korea Kusini, kama utawala mjini Seoul utaunga mkono vikwazo vipya vya Umoja wa Mataifa dhidi ya nchi hiyo. Onyo hilo la Korea Kaskazini limetolewa wakati ambapo Marekani imetangaza vikwazo zaidi vya kiuchumi dhidi ya Korea Kaskazini, kufuatia hatua ya nchi hiyo kutuma roketi ya setilaiti angani mwezi uliyopita. Korea Kaskazini imemuonya jirani wa kusini kuwa vikwazo vinamanisha kutangaza vita dhidi yao. Korea Kaskazini ilitangaza wiki hii kususia mazungumzo yote yanayolenga kusitisha mpango wake wa nyuklia, na kuapa kufanya majaribio zaidi ya roketi na nyuklia, baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuituhumu kwa jaribio la kombora la masafa marefu Desemba mwaka jana.

WAZAYUNI WAMECHOCHEA MARUFUKU YA KANALI ZA IRAN

Wabunge kadhaa nchini Uhispania wameikosoa vikali serikali ya nchi hiyo kwa kupiga marufuku matangazo ya kanali za Televisheni za Press TV na Hispan TV kutokana na mashinikizo ya lobi za Kizayuni na Marekani. Katika barua yao, wabunge wa chama cha United Left wameitaka serikali ya Uhispania kutoa maelezo iwapo Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania Jose Manuel Garcia-Margallo alijadili suala la kupiga marufuku kanali za Iran wakati alipokutana na lobi za Kizayuni Oktoba mwaka 2012. Wabunge hao wamesema mmiliki wa shirika la satalaiti ya Eutelsat ana uraia wa Israel na kwamba amekuwa akiongoza njama dhidi ya vyombo vya habari vya Iran barani Ulaya.
Televisheni ya Iran ya Hispan TV hurusha matangazo kwa lugha ya Kihispania kwa masaa 24 nayo Press TV hurusha matangazo yake kwa lugha ya Kiingereza. Hivi karibuni televisheni za kimataifa za Iran Hispan TV pamoja na Press TV zilipigwa marufuku kurusha matangazo yao kupitia satalaiti za Ulaya za Eutelsat na Hotbird. Aidha Shirika la Intelsat limepiga marufuku matangazo ya radio na televisheni kadhaa za kimataifa za Iran kufuatia mashinikizo ya Umoja wa Ulaya. Maamuzi hayo ya kupiga marufu vyombo vya habari vya Iran ni ishara ya wazi ya undumakuwili wa nchi za Magharibi zinazodai kutetea uhuru wa maoni. Nchi za Ulaya na Marekani zikishirikiana na utawala wa Kizayuni wa Israel zinajaribu kuzima sauti ya haki ya vyombo vya habari vya Iran.