Wednesday, January 02, 2013

MAREKANI WAAFIKIANA MSWADA WAMATUMIZI


Wabunge nchini Marekani wameupitisha mswaada wa kuinusuru nchi hiyo kutumbukia kwenye mgogoro wa kiuchumi. Baada ya miezi kadhaa ya mijadala, Baraza la Wawakilishi limeuridhia mpango uliokwishaungwa mkono na Baraza la Seneti, kuzuia makato makubwa kwenye matumizi na kupanda kwa kodi. Sheria hiyo mpya itaruhusu kupandishwa kwa kodi kwa wale wenye kipato cha juu tu na kuchelewesha makato ya matumizi kwa miezi miwili.
Akizungumza muda mfupi baada ya makubaliano hayo kufikiwa, Rais Barack Obama aliwapongeza wajumbe wa Democrats na Republicans kwa kufikia muafaka. Hata hivyo, alionya kwamba mengi zaidi yanapaswa kufanyika kudhibiti matumizi. "Tunaweza kushirikiana kama Democrats na Republicans kukata matumizi na kuongeza mapato kwa namna ambayo inapunguza nakisi yetu, inalilinda tabaka letu la kati, inatoa fursa kwa kila mtu anayefanya kazi kwa nguvu kuingia kwenye tabaka hilo la kati." Amesema Rais Obama.
Wajumbe wa Republican walikuwa wametaka ukataji wa matumizi kuwa sehemu ya makubaliano hayo, lakini waliyaacha madai hayo baada ya kushindwa kupata uungwaji mkono wa kutosha. Rais Obama anatarajiwa kuusaini mswaada huo kuwa sheria hivi punde.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO