Friday, January 25, 2013

ALSHABABA WATISHIA KUWAUA MATEKA WA KENYA

Waasi wa Somalia wa al Shabab wameitaka Kenya kuwaachilia huru Waislamu wote wanaoshikiliwa kwa tuhuma za ugaidi na kutishia kuwa takwa hilo lisipotekelezwa watawaua mateka wote wa Kenya wanaowashikilia. Waasi hao wametuma kwenye mtandao wa Tweeter video ya Wakenya wawili waliowateka nyara katika kaunti ya Wajir mwaka uliopita na kuiambia serikali ya Kenya kwamba maisha yao yapo hatarini.
Wiki iliyopita waasi wa al Shabab wa Somalia walisema kwamba wamemuua Denis Allex, jasusi wa Ufaransa waliokuwa wanamshikilia mateka, ili kulipiza kisasi kutokana na kile walichoeleza kuwa ni uadui wa Ufaransa kwa Waislamu na mashambulizi yake ya kijeshi nchini Mali. Kenya inawashikilia watu kadhaa wanaodaiwa kuwa na uhusiano na kundi la as Shabab na kuhusika katika mashambulizi ya kigaidi nchini humo.

WAPALESTINA KUISHITAKI ISRAEL ICC

Mamlaka ya Ndani ya Palestina imetishia kuichukulia Israel hatua za kisheria katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) iwapo Tel Aviv itajenga nyumba mpya katika maeneo ya Palestina inayoyakaliwa kwa mabavu. Riyad al Maliki Waziri wa Mambo ya Nje wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema hayo baada ya kushiriki kwenye mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York. Ameongeza kuwa, iwapo Israel itaendelea kujenga vitongoji vipya vya walowezi wa Kizayuni pamoja na mipango mingineyo katika mji wa Baitul Muqaddas, Palestina itaifungulia mashtaka katika mahakama ya ICC kwani haitakuwa na chaguo jingine.
Utawala wa Kizayuni wa Israel unapanga kupanua vitongozi vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Palestina unayoyakalia kwa mabavu pambizoni mwa Quds Mashariki, suala ambalo ni kinyume cha maazimio na sheria za kimataifa.

Wednesday, January 23, 2013

MTAMBO WA PATRIOT TAYARI KUANZA KAZI

Mtambo wa kwanza wa makombora ya ulinzi ya Patriot unatarajiwa kuwa tayari kwa ajili ya kuanza kutumika mnamo mwishoni mwa wiki hii. Mtambo huo umepelekwa na nchi za Jumuiya ya kujihami ya NATO nchini Uturuki kwa lengo la kuilinda nchi hiyo dhidi ya uwezekano wa mashambulio kutoka Syria. Marekani, Ujerumani na Uholanzi zimepeleka mtambo huo wa ulinzi wa Patriot baada ya serikali ya Uturuki kuiomba Jumuiya ya NATO kuisadia kuimarisha ulinzi katika anga yake. Kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Gary Deakin kutoka Uingereza, ambaye ni afisa wa ngazi ya juu wa NATO, jeshi la Uholanzi litakuwa la kwanza kuweka mtambo wake na ambao utakuwa tayari kuanza kutumika mwishoni mwa wiki hii. Aidha amesema mitambo yote ya Patriot inatarajiwa kuwa tayari kuanza kazi kufikia mwishoni mwa mwezi huu wa Januari.

MLEBANON ATIWA NGUVUNI KWA KUIFANYIA UJASUSI ISRAEL

Vikosi vya Kiitelijinsia vya Lebanon vimemtia mbaroni raia mmoja wa nchi hiyo kwa tuhuma za kushirikiana na shirika la ujasusi la Israel (Mossad) kwa zaidi ya miongo miwili. Mtu huyo aliyetambuliwa kwa jina la Ali Taufiq Yari anadaiwa kuwa alilipwa na Israel dola za Kimarekani laki sita kwa kuupatia utawala huo taarifa za siri kuhusu harakati ya Muqawama ya Lebanon Hizbullah na jeshi la nchi hiyo. Imeelezwa kuwa mwakilishi huyo wa zamani wa baraza la mji huko Baalbek aliwapatia maafisa wa ujasusi wa Israel taarifa nyingi muhimu wakati wa vita vilivyoanzishwa na utawala huo wa Kizayuni dhidi ya Lebanon mwaka 2006.

Yari ambaye imeelezwa kuwa alijiunga na Mossad mwaka 1990 ametajwa na maafisa wa Lebanon kuwa jasusi anayelipwa kitita kikubwa cha fedha kuwahi kutiwa mbaroni hadi sasa.

RUSSIA YAONYA KUHUSU VITA NA IRAN

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov ameonya kuwa hujuma yoyote ya kijeshi dhidi ya Iran itasababisha maafa makubwa. Akizungumza na waandishi habari mjini Moscow, Lavrov amesema kutatua kadhia ya nyuklia ya Iran kupitia nguvu za kijeshi ni jambo ambalo litasababisha maafa makubwa duniani.
Katika miaka ya hivi karibuni Marekani, Utawala wa Kizayuni na waitifaki wao wamekuwa wakitoa vitisho vya kuishambulia Iran kijeshi kwa sababu ya miradi yake ya kuzalisha nishati ya nyuklia. Iran imesisitiza kuwa shughuli zake za nyuklia zinafanyika kwa malengo ya amani katika fremu ya sheria za kimataifa. Kwingineko katika matamshi yake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema Iran ina nafasi muhimu sana katika kutatua matatizo ya Mashariki ya kati. Lavrov amesisitiza kuwa bila kuhusishwa Iran, matatizo mengi ya eneo hilo hayawezi kutatuliwa.

UFARANSA YATAKA TENA MAZUNGUMZO YA PALESTINA NA ISRAEL

Laurent Fabius Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ufaransa ameeleza matumaini ya kwamba mazungumzo ya amani kati ya Wapalestina na Wazayuni yataanza haraka iwezekanavyo. Akiashiria uchaguzi wa bunge la utawala wa Kizayuni wa Israel, Fabius amesisitiza kuwa, uongozi ujao wa utawala huo unapasa kuanzisha mazungumzo haraka iwezekanavyo ya kutatua mgogoro na Wapalestina. Ameongeza kuwa, mwaka wa 2013 unapasa kuwa mwaka wa kupatikana amani katika eneo la Mashariki ya Kati.
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ufaransa amesema moja kati ya masuala muhimu ya eneo la Mashariki ya Kati ni mapigano ya mara kwa mara kati ya Wazayuni na Wapalestina, jambo ambalo halikuzumgumzwa hata kidogo kwenye kampeni za uchaguzi wa Israel. Magazeti ya utawala wa Israel wiki zilizopita yalielezea mpango utakaosimamiwa na Ufaransa na Uingereza wenye shabaha ya kuanzishwa tena mazungumzo ya amani ambayo yalikwama miaka miwili iliyopita, baada ya utawala wa Israel kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina

MAREKANI KUTUMA WANAJESHI 3500 NCHI ZA AFRIKA

Serikali wa Marekani imeazimia kupeleka wanajeshi 3,500 katika nchi 35 za Kiafrika mwaka huu wa 2013. Gazeti la World Tribune linalochapishwa Marekani limeandika kuwa, hatua hiyo ya Washington ina shabaha ya kukabiliana na ongezeko la nguvu za kundi la al Qaeda na vitisho vya makundi mengine yenye mfungamano na kundi hilo. Gazeti hilo limeandika kuwa, Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon imesisitiza juu ya kutumwa majeshi hayo kwenye maeneo yaliyokumbwa na ghasia barani Afrika kwa lengo la kutokomeza ugaidi.
Jenerali Carter Ham Kamanda wa Majeshi ya Marekani barani Afrika AFRICOM amesema kuwa, hali iliyoko hivi sasa Afrika inatofautiana na ilivyokuwa hapo awali. Jenerali Ham ameongeza kuwa, kuna makundi mapya yanayobeba silaha ambayo hayana uhusiano na mtandao wa al Qaeda na kusisitiza kuwa, makundi hayo ni tishio kubwa kwa Marekani. Weledi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa, Marekani bado inatumia kisingizio cha kupambana na ugaidi kwa lengo la kuimarisha satua zake na kufikia malengo yake haramu katika maeneo mengi duniani

Tuesday, January 22, 2013

MICHEL SULEIMAN ASEMA MJI MKUU WA PALESTINA NI QUDS

Rais Michel Suleiman wa Lebanon amesema kuwa, nchi yake itaendelea na juhudi zake kwa shabaha ya kuhakikisha linaundwa taifa huru la Palestina, mji mkuu wake ukiwa Baytul Muqaddas. Akizungumzia mashinikizo yanayofanywa na utawala haramu wa Kizayuni kwa ajili ya kuzuia kuundwa kwa taifa hilo Michel Suleiman amesema, kuundwa kwa taifa la Palestina kutapelekea kuimarika demokrasia, uadilifu na kumaliza kabisa uvamizi wa Waisrael katika eneo. Aidha Rais huyo wa Lebanon amesisitiza juu ya haki ya kurejea wakimbizi wote wa Kipalestina katika ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni. Akizungumzia mgogoro wa nchi jirani ya Syria, Rais Michel Suleiman wa Lebanon amesema kuwa, lazima zifanyike juhudi za ziada zitakazosaidia kuanza kwa mazungumzo ya kisiasa na kumaliza hali mchafukoge inayoendelea katika nchi hiyo ya Kiarabu.

RUSSIA KUPANUA UHUSIANO WAKE NA IRAN

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia zimesema kuwa, zina azma ya kushirikiana katika uwanja wa kupambana na uhalifu wa kimataifa yakiwemo magendo ya madawa ya kulevya na ugaidi. Hayo yameelezwa na Ismail Ahmadi Muqaddam Mkuu wa Jeshi la Polisi la Iran na Vladimir Kolokoltsev Waziri wa Mambo ya Ndani ya Russia katika mazungumzo yao hapa mjini Tehran. Ismail Ahmadi Muqaddam Mkuu wa Jeshi la Polisi la Iran ameashiria katika mazungumzo hayo juu ya vitisho mbalimbali na vya pamoja na kubainisha kwamba, Iran na Russia zina uwezo wa kitaalamu, kielimu na kivitendo katika uwanja wa kupambana na madawa ya kulevya na ugaidi. Kwa upande wake Vladimir Kolokoltsev Waziri wa Mambo ya Ndani ya Russia amesisitiza katika mazungumzo hayo kwamba, kuna udharura wa kupanuliwa ushirikiano wa nchi mbili hizi katika uwanja wa usalama sambamba na kutekelezwa maafikiano ya Moscow na Tehran katika uwanja huo.

HAMAS YASEMA ROHO ZA MATEKA ZIKO MIKONONI MWA ISRAEL

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imetangaza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel ndio unaobeba dhima ya roho za wafungwa na mateka wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika magereza ya utawala huo katili. Taarifa ya Hamas sambamba na kutoa mkono wa pole kutokana na kuuawa shahidi Ashraf Abu Dhari' mateka wa Kipalestina aliyekuwa akishikiliwa katika moja ya magereza ya utawala huo ghasibu imesisitiza kwamba, askari magereza wa utawala huo wamekuwa wakiwatesa mateka na wafungwa wa Kipalestina kwa adhabu na mateso mbalimbali ya kiroho na kimwili. Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imelaani vitendo vya kinyama wanavyofanyiwa Wapalestina katika magereza ya Israel na kuitaka jamii ya kimataifa pamoja na asasi za kutetea haki za bninadamu ulimwenguni zichukue hatua za maana ili Wapalestina hao waachiliwe huru. Aidha Hamas imetoa wito kwa asasi za kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama la umoja huo ziushinikize utawala wa Kizayuni wa Israel ili uache kuwafanyia unyama wafungwa na mateka wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika magereza ya Israel.

EUTELSAT YAKATA MATANGAZO YA HISPANIA TV YA IRAN

Shirika la kutoa huduma za Satalaiti la Eutelsat limechukua hatua zisizo za kisheria za kukata matangazo yanayorushwa na Hispan TV ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Siku chache zilizopita, serikali ya Uhispania katika hatua inayokinzana na uhuru wa kujieleza ilitoa amri kwa shirika linalotoa huduma za satalaiti la Hispasat kukata matangazo yanayorushwa na Shirika la Utangazaji la Iran kwa lugha ya Kihispania na ile ya Kiingereza ya Press TV.
Hatua ya Hispasat ya kukata matangazo ya Televisheni za Iran imepokelewa kwa mikono miwili na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel. David A. Harris Mkurugenzi Mtendaji wa Kamati ya Mayahudi wa Marekani (AJC) amesifu na kuunga mkono uamuzi huo. David Harris ameongeza kuwa, miezi kadhaa iliyopita kulifanyika mazungumzo na viongozi wa Uhispania juu ya kukatwa matangazo ya kanali za televisheni za Iran katika satalaiti ya Hispasat.

WAPINZANI WA MALI WAAPA KULIPIZA KISASI

Wapinzani wa serikali ya Mali wametishia kulipiza kisasi kwa serikali ya Ufaransa na utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na mashambulizi wanayoyafanya nchini humo.
Taarifa iliyotolewa na wapinzani wa serikali ya Mali imeeleza kwamba, Ufaransa na utawala wa Kizayuni wa Israel zitakiona cha mtemakuni kutokana na hatua zao za kuwashambulia Waislamu wa maeneo ya kaskazini mwa Mali. Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kila mwanamgambo wa upinzani amekula kiapo cha kulipiza kisasi cha damu za Waislamu kutoka kwa majeshi vamizi ya Ufaransa na utawala wa Israel.
Rais Francois Hollande wa Ufaransa yapata siku kumi zilizopita alitoa amri ya kushambuliwa maeneo ya kaskazini mwa Mali, mashambulio ambayo yamelitumbukiza eneo lote la magharibi na kaskazini mwa Afrika katika machafuko. Serikali ya Paris imewapeleka wanajeshi wasiopungua 2,150 nchini Mali kwa lengo la kutekeleza operesheni ya kijeshi.

MATEKA WA KIFILIPINO WAULIWA ALGERIA

Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufilipino imetangaza kuwa watu wenye silaha wamewauwa wafanyakazi sita raia wa nchi hiyo huko katika kiwanda cha gesi asilia nchini Algeria. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufilipino Raul Fernandez amesema kuwa vifo vya wafanyakazi hao sita raia wa Ufilipino vilitokea baada ya kutekwa nyara kwenye kiwanda hicho cha gesi na zaidi vilisababishwa na majeraha ya risasi na athari za milipuko.
Wakati huo huo Algera imetahadharisha kuwa idadi ya vifo vya mateka katika kiwanda cha gesi nchini humo vitaongezeka. Hadi sasa mateka wasiopungua 48 wanakadiriwa kuwa wameuawa katika kituo cha gesi cha Sahara huku wengine wanaokaribia 20 wakiwa hawajulikani walipo. Vikosi vya jeshi la Algeria jana vilisema kuwa vimegundua viwiliwili vya mateka 25 na kuwatia nguvuni watekaji nyara watano katika kiwanda cha gesi cha In Amenas kilichopo katika jangwa la Sahara siku moja baada ya kulivamia eneo la kiwanda hicho linaloendelea kushikiliwa na waasi.

WALINGANIAJI WA MISRI WAILALAMIKIA UFARANSA

Jumuiya ya Walinganiaji wa Kiislamu wa Misri imetoa wito wa kufukuzwa mabalozi wa Ufaransa katika nchi za Kiislamu na Kiarabu. Jumuiya hiyo imetaka kufukuzwa mabalozi wa Ufaransa katika nchi hizo na kutoa wito wa kushinikizwa Paris ili isitishe mashambulizi yake ya kijeshi huko Mali. Jumuiya hiyo inapinga vikali uingiliaji kijeshi wa Ufaransa huko nchini humo.
Walinganiaji wa Kiislamu wa Misri pia wameutaka Umoja wa Mataifa kutekeleza majukumu yake mbele ya uingiliaji kijeshi wa Ufaransa huko Mali na kuishawishi Paris isimamishe mashambulizi yake dhidi ya nchi hiyo. Rais Francois Hollande wa Ufaransa siku kumi zilizopita alitoa amri ya kuanza vita dhidi ya makundi yanayobeba silaha huko kaskazini mwa Mali, mashambulizi yanayotajwa kuigharimu fedha nyingi Ufaransa. Eneo la kaskazini mwa Mali linakabiliwa na mashambulizi makubwa ya ndege za kivita za Ufaransa kwa siku kadhaa sasa.

HAMAS YATAKA MATEKA WAO WAACHIWE HURU NA ISRAEL

Afisa wa uhusiano wa kimataifa wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas ametangaza kuwa suala la kuachiwa huru mateka wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika jela za Israel ni moja ya vipaumbele vya Hamas na makundi mengine ya mapambano ya Palestina.
Usama Hamdani ameeleza kuwa mateka zaidi ya elfu tano wa Kipalestina wanashikiliwa katika jela za utawala wa Kizayuni na kwamba kuachiwa huru raia hao ni moja ya masuala yanayozingatiwa sana na Hamas na makundi mengine ya mapambano ya Palestina. Usama Hamdani pia amesema kuhusiana na kukusanyika kila wiki kwa Wapalestina mbele ya ofisi ya Shirika la Msalaba Mwekundu Duniani huko Ghaza kuwa, Hamas itatekeleza ahadi yake ya kuhakikisha kuwa Wapalestina walioko katika jela za Israel wanakuwa huru na kwamba faili la mateka hao litafungwa hivi karibuni.