Sunday, March 31, 2013

WIZARA YA SHERIA YASHAMBULIWA LIBYA

Watu wenye silaha wameishambulia Wizara ya Sheria ya Libya baada ya wizara hiyo kukataa kuwalipa mishahara watu wenye silaha walioshiriki kwenye mapinduzi yaliyomng'oa madarakani Kanali Muammar Gaddafi. Ukurasa wa Intaneti wa al Yaumus Saabi'i umeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, leo watu wenye silaha wameishambulia Wizara ya Sheria ya Libya baada ya waziri wa wizara hiyo kukataa kulipa mishahara ya watu hao.

Mtandao huo umenukuu ripoti mbalimbali zilizotolewa nchini Libya zikimnukuu Waziri Sallah al Mirghani akisema kuwa serikali ya Tripoli italipa mishahara ya vikosi vya polisi na vikosi vilivyoko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani tu. Waziri huyo wa Sheria wa Libya ameongeza kuwa, si tu kwamba makundi ya watu wenye silaha yaliyoshiriki katika mapinduzi nchini Libya hayatalipwa mishahara likini pia serikali itashambulia maeneo yaliko makundi hayo na kuyapokonya silaha kwa nguvu. Taarifa kutoka Libya zinasema kuwa, milio ya risasi imesikika karibu na Wizara ya Sheria ya nchi hiyo.

MAREKANI ITABEBA LAWAMA VITA YA KOREA

Mchambuzi mmoja mwandamizi wa masuala ya kijeshi amesema kuwa, Marekani ndiyo itakayobeba lawama iwapo kutatokea vita kati ya Korea mbili zilizogawanyika. Jeff Steinberg wa jarida la kila wiki la Executive Intelligence Review (EIR) la nchini Marekani ameiambia televisheni ya Press TV kuwa, Marekani ambayo ni dola lenye nguvu duniani inataka kulisukuma mbele suala hilo hadi kuitumbukiza dunia katika vita ambavyo kuna uwezekano vikawa vya nyuklia. Amesema, mpira hauko katika uwanja wa Korea Kaskazini, bali uko kwenye uwanja wa Marekani. Korea Kaskazini imesema kuwa, kuanzia sasa uhusiano wake utakuwa ni wa zama za vita na masuala yote yanayohusiana na Korea mbili yatazingatiwa kwa protokali ya wakati wa vita. Vile vile imeonya kuwa, uchokozi wa aina yoyote ile wa kijeshi karibu na Korea Kaskazini, iwe ni ardhini au kwenye mpaka wa baharini, utashuhudia majibu makali sana na utakuwa mwanzo wa vita vya nyuklia. Hivi karibuni Marekani ilifanya manuva ya kijeshi karibu na Korea Kaskazini ikishirikiana na Korea Kusini hatua ambayo iliikasirisha sana Korea Kaskazini; nchi ambayo inaamini pia kuwa Marekani ilichochea vikwazo vipya vya Umoja wa Mataifa dhidi yake, baada ya Pyongyang kufanya majaribio ya nyuklia mwezi Februari mwaka huu.

MISRI KUPAMBANA NA WANAOVUNJIA HESHIMA UISLAM

Wizara ya Wakfu ya Misri ina mpango wa kuanzisha kitengo cha kukabiliana na vitendo vya kuivunjia heshima dini tukufu ya Kiislamu. Sheikh Ahmad Khalil anayehusika na masuala ya miongozo ya Kiislamu katika Wizara ya Wakfu ya Misri amesema kuwa, kuna udharura wa kuanzisha kitengo cha kukabiliana na vitendo vinavyoitovukia adabu dini ya Kiislamu ndani na nje ya Misri. Sheikh Khalil amesema kuwa, kitengo hicho kitafuatilia kila kitendo cha kuuvunjia heshima Uislamu kitakachofanywa ndani au nje ya Misri na kutoa majibu yanayotatikana kwa wale wote watakaoyatovukia adabu matukufu ya dini hiyo tukufu.

HARAAAAAM

KARZAI KUZUNGUMZIA KUFUNGULIWA OFISI YA TALIBAN QATAR

Rais Hamid Karzai wa Afghanistan leo anatazamiwa kuwa na mazungumzo nchini Qatar juu ya pendekezo la kufunguwa ofisi ya kundi la Taliban katika taifa hilo la Ghuba ikiwa kama ni hatua ya kwanza juu ya uwezekano wa kufanyika kwa mazungumzo ya kukomesha vita vilivyodumu zaidi ya muongo mmoja nchini Afghanistan. Karzai huko nyuma alikuwa amepinga kufunguliwa kwa ofisi hiyo akihofia kuwekwa kando kwa serikali yake katika mazungumzo yoyote yale yatakayowahusisha wanamgambo hao wa itikadi kali na Marekani. Wanamgambo hao wanagoma kuwa na mazungumzo ya moja kwa moja na rais huyo wa Afghanistan kwa kusema kwamba ni kibaraka wa Marekani ambayo ilisaidia kumuweka madarakani baada ya operesheni ya kijeshi ya kuu'gowa utawala wa Taliban kutoka Kabul hapo mwaka 2001. Kutokana na kwamba vikosi vya Jumuiya ya Kujihami ya NATO vinavyoongozwa na Marekani vinatarajiwa kuondoka nchini Afghanistan mwishoni mwa mwaka 2014 Karzai amekubali pendekezo la kuwepo kwa ofisi ya Taliban katika mji mkuu wa Qatar Doha na anatarajiwa kuutaja mpango huo wakati wa mazungumzo yake na Mfalme wa Qatar leo hii.

SAFARI ZA NDEGE ZAANZA TENA KATI YA IRAN NA MISRI


Safari ya kwanza ya ndege ya moja kwa moja kati ya Tehran na Cairo imeanza baada ya miongo mitatu. Ndege ya Shirika la Ndege la Memphis la Misri iliondoka Cairo mapema Jumamosi asubuhi na kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Imam Khomeini mjini Tehran.
Ndege hiyo ilikuwa na abiria kadhaa Wairani wakiwemo wanadiplomasia. Mapema mwezi huu Waziri wa Usafari wa Ndege Misri Wael El-Maadawi alisema safari za ndege kati ya Iran na Misri zitaunganisha miji ya kitalii ya Misri kama vile Luxor, Aswan na Abu Simbel na Jamhuri ya Kiislamu. Iran na Misri zimetilaiana saini makubaliano ya kuimarisha uhusiano wa kitalii baina ya pande mbili. Uhusiano wa Iran na Misri ulianza kuboreka baada ya dikteta kibaraka Husni Mubarak kutimuliwa madarakani mwaka 2011 na mahala pake kuchukuliwa na Rais Mohammad Mursi wa harakati ya Ikwanul Muslimin. Rais Mursi alitembelea Iran mwezi Agosti kushiriki katika kikao cha Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM. Rais Ahmadinejad wa Iran naye alitembelea Misri miezi miwili iliyopita kushiriki katika kikao cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu.

WANAOGOMBEA KITI CHA URAIS IRAN WAONGEZEKA


Waziri wa Barabara na Ustawi wa Miji Iran Ali Nikzad ametangaza rasmi uamuzi wake wa kugombea kiti cha urais katika uchaguzi ujao nchini na hivyo kufanya idadi ya waliotangaza azma ya kugombea kiti hicho kuwa tisa. Nikzad alitangaza uamuzi wake huo Jumamosi alipotembelea mji wa Ardebil ulio kaskazini magharibi mwa Tehran.
Uchaguzi wa 11 wa rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran utafanyika mwezi Juni na wagombea wote wanatakiwa kujiandikisha kati ya Mei 7 na 11. Rais Mahmoud Ahmadinejad anamaliza muhula wake wa pili na hivyo kikatiba hawezi kugombea. Kati ya waliotangaza kuwa tayari kugombea kiti cha urais Iran ni pamoja na waziri wa zamani wa mambo ya nje Manouchehr Mottaki, manaibu spika wawili wa bunge Sheikh Mohammad Hassan Aboutorabi-Fard na Mohammad Reza Bahonar. Wengine waliotangaza nia ya kuwania urais wa Iran ni pamoja na waziri wa zamano wa mambo ya ndani Sheikh Mostafa Pour-Mohammadi, mwanachama mwandamizi wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo, Sheikh Hassan Rohani, Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo Dkt. Mohsen Rezaei, waziri wa zamani wa usalama wa ndani Sheikh Minister Ali Fallahian na waziri wa zamani wa nyumba Mohammad Saeedi-Kia. Rais wa Iran huchaguliwa baada ya miaka minne na wagombea wote huidhinishwa baada ya kuchunguzwa na Baraza la Kulinda Katiba.

WAMISRI WATWANGANA KATIKA UUNDAJI WA SERIKALI


Miji ya Cairo na Alexandria jana ilikuwa uwanja wa mapigano na maandamano ya waungaji mkono na wapinzani wa serikali ya sasa ya Cairo. Mjini Cairo maandamano na mapigano ya pande hizo mbili yalisimamisha shughuli za biashara katika maeneo ya kandokando ya Medani ya Tahrir na kuwalazimisha wafanya biashara kutumia bunduki za kuwindia wanyama wakiwalenga waandamanaji. Watu kumi wamejeruhiwa katika mapigano hayo. Muungano wa wapinzani wa serikali ya Rais Muhammad Mursi hususan Harakati ya Uokovu wa Kitaifa ulikuwa umewataka wafuasi wake kushiriki kwa wingi katika maandamano hayo.
Mji wa Alexandria pia ulikumbwa na hali kama ile ya Cairo. Wafuasi wa kambi mbili za waungaji mkono na wapinzani wa serikali walitwangana na kushambuliana kwa kutumia silaha za aina mbalimbali. Kanali ya televisheni ya al Mayadeen ya Lebanon pia imeripoti kuwa mapigano ya silaha yameshuhudiwa mbele ya ofisi ya Harakati ya Ikhwanul Muslimin mjini humo.
Mapigano hayo yalianza wakati wa wafuasi wa kambi ya upinzani dhidi ya serikali ya Cairo walipotaka kuvamia ofisi za Harakati ya Ikhwanul Muslimin. Mapigano hayo yalishadidi zaidi baada ya wapinzani kuanza kutoa nara dhidi ya serikali ya Rais Muhammar Mursi na kusababisha ghasia kubwa katika mji mzima wa Alexandria.
Vyombo vya habari vimetangaza kuwa, machafuko ya sasa ya Misri yanahusiana na tukio la kuuzuliwa Mwendesha Mashtaka Mkuu Abdul Majiid Mahmoud. Mwezi Novemba mwaka jana Rais Mursi alimfuta kazi Abdul Majiid ambaye aliamua kufungua kesi mahakamani dhidi ya uamuzi huo. Baada ya kusikiliza kesi hiyo Mahakama ya Rufaa ya Misri ilimwamuru Rais wa nchi hiyo kufuta uamuzi wake na kumrejesha kazini Mwendesha Mashtaka Mkuu. Uamuzi huo umepongezwa na mrengo wa kiliberali nchini Misri ambao umeutaja kuwa ni ushindi wa utawala wa sheria na ishara ya uhuru wa mahakama za nchi hiyo. Hata hivyo duru za kieneo zinasema kuwa kufutwa uamuzi wa Rais wa Misri ulikuwa mwanzo wa mpambano mkali baina ya serikali ya Cairo na taasisi ya mahakama. Suala hilo hususan katika mazingira yanayotawala sasa nchini Misri, ni tishio kubwa kwa mapinduzi ya wananchi. Vilevile Waziri Mkuu wa Misri Hesham Qandil amesema kuwa nchi hiyo inakabiliwa na matatizo makubwa na kusema kuwa moja ya matatizo hayo ni ghasia na ukosefu wa amani.
Hali hiyo ya ukosefu wa amani imetumiwa vibaya na baadhi ya makundi yasiyokuwa na utambulisho wa kisiasa na kumlazimisha Rais Mursi kutahadharisha kwamba baadhi ya mirengo ya kisiasa na hata wanasiasa wa Misri wanatumia vyombo vya habari kuchochea wananchi. Mursi amesema kuna tofauti kubwa baina ya haki ya wananchi ya kufanya maandamano ya amani ya kudai haki zao na machafuko na ghasia zinazoharibu mali ya umma. Rais wa Misri amevitaka vyombo vya usalama kukabiliana na machafuko hayo.
Ghasia za sasa za Misri zimetoa dharba kubwa kwa uchumi wa nchi hiyo. takwimu zinaonesha kuwa, machafuko ya kisiasa na ghasia za Misri zimeisababishia nchi hiyo hususan sekta ya utalii hasara ya dola bilioni moja. Wachambuzi wa mambo wanasema hasara hiyo huenda ikaongezeka zaidi iwapo serikali ya Cairo itashindwa kudhibiti ghasia na machafuko yanayotatiza shughuli za utalii. 

Saturday, March 30, 2013

KIM JONG UN AAGIZA KUWEKWA TAYARI ROKETI ZA MASAFA MAREFU


Kiongozi wa Taifa la Korea Kaskazini Kim Jong-Un ameagiza roketi za nchi hizo ziwe tayari kwa mashambulizi kulenga kambi za kijeshi za Marekani pamoja na kuwashambulia washirika wao Korea Kusini. Tamko hilo limezidisha hofu ya usalama wa dunia kutokana na wengi kuhisi huenda mataifa hayo mawili ambayo yanamiliki silaha za maangamizi wakazitumia wakati wa vita na kuelta madhara si tu kwa wananchi lakini kwa mazingira.
Kim ametoa agizo hilo kutokana na kukerwa na kitendo cha majeshi ya marekani na yale ya Korea Kusini kuendelea na mazoezi yao ambayo Korea Kaskazini imeyaita yakichokozi na yanalengo la kutaka kuishambulia nchi yao. Agizo hilo limekuja kipindi hiki ambacho Waziri wa Ulinzi wa Marekani Chuck Hagel akiwa ziarani katika eneo la Peninsula na kusema Washington haiwezi ikawa muonga kutokana na vitisho vya Pyongyang. Mapema serikali ya Korea Kaskazini ilishatishia kufanya mashambulizi kulenga kambi za kijeshi za Marekani huko Japan kutokana na kukerwa na tabia ya nchi hiyo kuendelea kuifuatia kwenye shughuli zao za majaribio ya makombora ya nyuklia. Kwa upande wake Korea Kusini yenyewe imeendelea kusisitiza kuwa haiogopi vitisho hivyo na badala yake wametoa wito kwa Serikali ya Kim, kuachana na mpango wake wa Nyuklia ili kurudi karibu na jumuiya ya kimataifa. Juma hili pia Korea Kaskazini ilitangaza kukata njia zote za mawasiliano ya kijeshi na majirani zao ikiwa ni hatua za awali katika kutekeleza kile ambacho imeahidi kukitekeleza katika siku chache zijazo.

SYRIA, IRAN NA KOREA KIKWAZO CHA KUSAINI MKATABA WA KUDHIBITI SILAHA


Serikali ya Ufaransa imekumbwa na kizungumkuti iwapo itoe silaha kwa waasi nchini Syria au la na badala yake wanaendelea kusubiri maamuzi ya Umoja wa Ulaya EU ambao utaamua juu ya ombi lao na Uingereza kutaka kuondoa kizuizu cha kupeleka silaha Damascus. Rais wa Ufaransa Francois Hollande ameweka bayana kwa sasa hawana uhakika kama wataweza kuwasaidia Waasi wanaopambana na serikali ya Rais Bashar Al Assad kwa kuwapatia silaha ili waendelea na vita vyao. Hollande amesema kwa sasa hilo limebaki kuwa chini ya Umoja wa Ulaya EU licha ya Ufaransa na Uingereza kuwa tayari hapo kabla kuwasaidia waasi kwa kuwapatia silaha.Katika hatua nyingine rais Bashar al-Asad amelaani vikali shambulio la roketi lililotekelezwa kulenga wanafunzi wa chuo kikuu cha mjini Damascus, shambulio ambalo rais Asad amewatuhumu upinzani. Kwenye taarifa yake rais Asad amesema kuwa shambulio hilo linaendelea kudhihirisha ukatili ambao umekuwa ukifanywa na waasi wa Syria dhidi ya wananchi wasio na hatia na kwamba makundi ya kigaidi yameendelea kuwasaidia waasi kutekeleza mashambulizi zaidi dhidi ya Serikali na watu wake. Hata hivyo upande wa waasi umekanusha kutekeleza shambulio hilo ambalo lilishuhudia wanafunzi kumi na mbili wakipoteza maisha kwenye mgahawa wa chuo ambako walikuwa wakinywa chai kabla ya kuvurumishwa kwa roketi hiyo.Halikadhalika nchi za Iran, Korea Kaskazini na Syria zimepinga kutiwa saini mkataba maalumu wa kutazama biashra ya silaha duniani, mkataba ambao ulikuwa unahitaji baraka za nchi wanachama 193 ili uweze kufanya kazi. Balozi wa Australia Peter Woolcott amesema kuwa mkutano huo umeshindwa kutoka na maamuzi baada ya nchi hizo tatu kukataa kuunga mkono azimio hilo ambalo lililenga kuwepo uangalizi wa karibu wakati nchi zinapokuwa zinanunua silaha kwa matumizi ya kiusalama. Awali balozi huyo alilazimika kuahirisha kikao baada ya nchi za Iran, Korea Kaskazini na Syria kukataa kuendelea kujumuika kwenye mkutano huo ka madai kuwa baadhi ya mataifa yamekuwa yakiwaongelea vibaya kuhusu matumizi ya silaha ambazo nchi hizo imekuwa ikinunua.

IRAQ KUPEKUWA NDEGE ZA IRAN ZINAZOELEKEA SYRIA


Iraq imesema leo hii kwamba itaimarisha upekuzi wake wa ndege  za Iran zinazopitia anga yake kuelekea Syria ikiwa ni siku chache baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry kuishutumu hadharani serikali ya Iraq kwa kuzifumbia macho safari za ndege hizo.
Wakati msemaji wa Waziri Mkuu Nuri al-Maliki akizungumzia juu ya kuimarishwa kwa masharti mapya juu ya safari za ndege za Syria zinazoelekea Syria, mkuu wa mamlaka ya anga nchini Iraq amekiri kwamba hakuna ndege zilizopekuliwa tokea mwezi wa Oktoba. Ali Mussawi msemaji wa al-Maliki ameliambia shirika la habari la AFP kwamba kutokana na kuwepo kwa taarifa nyingi zenye kugusia usafirishaji wa silaha wameongeza harakati za kufanya upekuzi. Amesema hakuna mtu aliyawapatia ushahidi bali ni taarifa tu.Alipokuwa katika ziara ya ghafla nchini Iraq Jumapili iliopita Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry aliwaambia waandishi wa habari kwamba alimueleza wazi waziri mkuu kwamba safari za ndege za Iran kupitia anga ya Iraq zinasaidia kuendelea kumuweka madarakani Rais Bashar al Assad na utawala wake nchini Syria.

KOREA YA KASKAZINI YATANGAZA HALI YA VITA NA KUSINI


Korea Kaskazini leo imetangaza kuwa iko katika hali ya vita na Korea Kusini na kuzionya serikali ya Korea Kusini na Marekani kwamba uchokozi wowote ule utakuja kupamba moto na kuwa vita kamili vya nyuklia.
Marekani imesema inalichukulia tangazo hilo kwa makini wakati Korea Kusini kwa kiasi kikubwa imelipuuza kuwa kama ni tishio la zamani lililovalishwa nguo mpya. Huo ni mfululizo wa hivi karibuni kabisa wa matangazo makali kutoka serikali ya Korea Kaskazini ambao umekuwa ukijibiwa na onyo kali kutoka serikali za Korea Kusini na Marekani na hiyo kuzusha wasi wasi wa kimataifa kwamba hali hiyo yumkini ikaripuka na kuja kushindwa kudhibitiwa. Korea Kaskazini imesema katika taarifa kwamba kuanzia sasa uhusiano baina ya Korea hizo mbili utashughulikiwa kwa mujibu wa itifaki ya wakati wa vita.

CHINA NA RUSSIA YAITAHADHARISHA US KUHUSU KOREA

Russia na China zimeitahadharisha Marekani kutozidisha chokochoko za kijeshi katika Peninsula ya Korea na kwamba hali hiyo huenda ikalitumbukiza eneo hilo kwenye ukosefu wa amani. Taarifa iliyotolewa leo na Sergei Lavrov Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia imeeleza kuwa, hatua za kijeshi zinazochukuliwa na Marekani dhidi ya Korea Kaskazini huenda zikaleta maafa makubwa.  Wizara ya Mambo ya Nje ya China pia imezitaka pande mbili kufanya juhudi za kupunguza hali ya wasiwasi na kuimarisha amani na uthabiti katika Peninsula ya Korea. Hayo yamejiri baada ya Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un kutangaza kuwa nchi yake imeweka makombora yake tayari kushambulia Marekani, vituo vya kijeshi vya Pasifiki, vikiwemo vya Hawai na Guam pamoja na vya Korea Kusini. Pyongyang imetangaza hayo baada ya Marekani kupeleka jana huko Korea Kusini ndege mbili zenye kubebea vichwa vya nyuklia aina ya B2 kwa madai ya kufanya maneva ya kijeshi katika Peninsula ya Korea.  Vilevile Washington na Seoul jana zilisaini makubaliano ya kijeshi, yanayoziruhusu nchi hizo mbili kujibu hata vitisho vya kiwango cha chini vya Korea Kaskazini.

WAISLAM WA UJERUMANI WATAKA MAPUMZIKO SIKU YA EID

Baraza la Waislamu nchini Ujerumani limeitaka serikali ya nchi hiyo kutoa mapumziko ya sikukuu za Idul Fitr na Idul Adhha kwa Waislamu nchini humo. Ayman Mazyek Katibu  Mkuu wa Baraza la Waislamu nchini Ujerumani ametoa pendekezo hilo kwa serikali ya nchi hiyo. Amesema kuwa, iwapo pendekezo hilo litakubaliwa bila shaka  umoja na mshikamano  utazidi kuimarika kati ya jamii ya nchi hiyo. Hata hivyo Guntram Schneider mkuu  wa jimbo la Nordrhein - Westfalen amepinga takwa hilo la Baraza la Waislamu nchini Ujerumani kwa madai kuwa, kutaka kutolewe ruhusa ya siku mbili kwa Waislamu kusherehekea sikukuu za Idul Fitr na Idul Adhha eti kutazorotesha uchumi wa nchi hiyo.

TUNISIA YAKANUSHA KUANGAUKA KWA NDEGE YA LIBYA

Wizara ya Ulinzi ya Tunisia imekanusha taarifa kwamba ndege moja ya Libya isiyo na rubani imeanguka katika ardhi ya nchi hiyo. Mukhtar bin Nasr msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Tunisia amesea habari zilizotangazwa kuhusu kuanguka ndege ya Libya isiyo na rubani katika ardhi ya Tunisia ni za uwongo na zisizo na msingi wowote. Baadhi ya vyombo vya habari nchini Tunisia vimeripoti kuwa ndege ya Libya isiyo na rubani Jumatano iliyopita ilianguka katika eneo linaloungana na kitongoji cha Bin Qadran huko kusini mwa Tunisia karibu na mpaka wa Libya. Vyombo hivyo vya habari viliripoti kuwa, baadaye ilifahamika kuwa ndege hiyo isiyo na rubani mali ya Libya ilitengenezwa nchini Marekani  baada ya vikosi vya jeshi la Tunisia kuwasili mahali ndege hiyo ilipoanguka.   

GHAZA MWENYEJI WA MKUTANO WA KIMATAIFA WA USALAMA WA PALESTINA

Mkutano wa kimataifa wa usalama wa taifa la Palestina umeanza leo katika mji wa Ghaza kwa kuhudhuriwa na shakhsia wa kisiasa na kiusalama wa Kiarabu na wa nchi za kigeni. Mkutano huo umeanza leo na utaendelea hadi kesho Jumapili. Hani al Basusi Mkuu wa Kamati ya Mawasiliano ya Mkutano wa Kimataifa wa Usalama wa Taifa la Palestina ametangaza kuwa mkutano huo utachunguza mipango ya kitaifa ya Palestina, malengo ya Wapalestina na Quds, muqawama, serikali ya ndani ya Palestina na mustakbali wake na pia matukio ya kisasa ya kieneo na athari zake kwa malengo ya Palestina. Hani al Basusi amesema washiriki wa mkutano wa Ghaza watawasilisha mapendekezo na ushauri kuhusu mipango ya taifa ya Palestina na kwamba anataraji kuwa maafisa wa ngazi ya juu wa Palestina pia watachukua hatua katika uwanja huo.

UFARANSA KUBAKIZA ASKARI 1000 BAADA YA 2013


Rais Francois Hollande wa Ufaransa amesema kuwa nchi yake itabakiza askari wasiopungua 1,000 nchini Mali baada ya mwaka 2013. Hollande ameongeza kuwa, Ufaransa itaanza kuondoa wanajeshi wake nchini Mali mwishoni mwa mwezi huu wa Aprili na kwamba askari hao watapunguzwa na kufikia 2,000 ifikapo mwezi Julai.
Inafaa kukumbusha hapa kuwa, Januari 11 mwaka huu Ufaransa ilianzisha mashambulizi ya kijeshi nchini Mali kwa kisingizio cha kupambana na waasi kaskazini mwa nchi hiyo, mashambulizi ambayo hayakuidhinishwa na Umoja wa Mataifa. Mashambulizi hayo ya Ufaransa yamesababisha hali mbaya ya kibinadamu nchini Mali na kusababisha maelfu ya watu kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.

MAITI ZAPATIKANA MJI WA BANGUI

Shirika la Msalaba Mwekundu la Jamhuri ya Afrika ya Kati limetangaza kuwa, makumi ya maiti zimepatikana katika mji mkuu wa nchi hiyo Bangui tangu waasi wa Seleka walipoipindua serikali ya Francois Bozize mwishoni mwa juma lililopita. Albert Yomba Eyamo, afisa wa Shirika la Mlasaba Mwekundu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati amewaambia waandishi wa habari kwamba, hadi sasa wafanyakazi wa shirika hilo wameokota maiti 78 katika mitaa na barabara za mji mkuu Bangui na kuzihamishia katika vyumba vya kuhifadhia maiti. Habari ya kupatikana maiti hizo imetangazwa sambamba na maadhimisho ya sherehe za kitaifa za kujipatia uhuru nchi hiyo kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Wakati huo huo habari kutoka mji mkuu Bangui zinasema kuwa, hali ya kimaisha katika mji huo ni mbaya huku baadhi ya maeneo yakiwa hayana maji wala umeme. Ikumbukwe kuwa, tarehe 24 ya mwezi huu wa Machi, muungano wa waasi wa Seleka uliyadhibiti maeneo nyeti ya Jamhuri ya Afrika ya Kati ikiwemo ikulu ya Rais hali iliyomlazimisha Rais Francois Bozize wa nchi hiyo aikimbie nchi. Bozize kwa sasa yuko nchini Benin baada ya kuondoka Kongo na Cameron.

KANISA KATOLIKI LAONYA KUENEA UMASIKINI ULAYA


Makanisa Katoliki ya Ujerumani na Italia yametoa tahadhari ya kuenea umasikini barani Ulaya na kutoa wito wa kuchukuliwa hatua kwa minajili ya kukabiliana na wimbi la umasikini. Mtandao wa Habari wa al-Masri al-Yaum umeyanukuu makanisa ya Kikatoliki ya Ujerumani na Italia yakisisitiza kwamba, kuna haja kwa serikali barani Ulaya kuwazingatia wananchi wanaokabiliwa na umasikini barani humo. Robert Zollitsch, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki nchini Ujerumani ametangaza kuwa, serikali ya nchi hiyo inapaswa kushughulikia tatizo la umasikini linalowakabili wananchi na kwamba, itazame upya sera zake za ustawi na zile za masuala ya fedha.
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki nchini Ujerumani ameongeza kuwa, hali ya umasikini inayowakabili wananchi nchini humo haipasi kuachwa iendelee. Aidha Askofu Robert Zollitsch amevikosoa vyombo vya habari vya Ujerumani kutokana na kutoakisi kwa uwazi habari za umasikini katika nchi hiyo na kusisitiza kwamba, suala la umasikini nchini humo haliripotiwi kama inavyotakiwa. Aidha amesema, umasikini nchini Ujerumani hususan katika miji mikubwa upo katika hali ya kupanuka na kuenea.

Thursday, March 28, 2013

WAPIGAMBIZI WATATU WAKAMATWA WAKIKATA MKONGA WA INTERNET ULIO CHINI YA BAHARI


Maafisa wa utawala nchini Misri, wamewakamata wapigambizi watatu waliokuwa wanajaribu kuukata mkonga wa internet ulio chini ya bahari. Wanaume hao walikamatwa wakiwa katika boti walilokuwa wanatumia kwa shughuli za uvuvi, katika mji wa bandarini wa Alexandria. Hii ni kwa mujibu wa msemaji wa jeshi kanali, Ahmed Mohammed Ali. Mkonga huo ulioharibiwa, ulizuia kasi ya huduma za internet nchini Misri na katika nchi nyingine.
Hata hivyo haikubainika ikiwa kupungua kwa kasi ya internet ilihusika moja kwa moja na kitendo cha watatu hao kuuharibi mkonga ijumaa iliyopita. Wakati huo, kampuni inayomiliki mkonga huo, Seacom, ilisema kuwa mitandao kadhaa iliyounganisha Ulaya na Afrika , Mashariki ya kati na Asia ya Mashariki, iliathirika na hivyo kupunguza kasi ya huduma za internet. Mkonga uliovamiwa Jumatano ulikuwa ule uliounganisha huduma za internet katika nchi za Asia mashariki na Ulaya Magharibi.
Uvamizi ulitokea umbali wa mita 750 Kaskazini mwa Alexandria. Katika taarifa kwenye ukurasa wake wa Facebook Kanali Ali, alisema kuwa wapiga mbizi hao walikamatwa wakati wakivamia mkonga wa kampuni rasmi ya mawasiliano nchini Misri. Hata hivyo hakutoa maelezo yoyote kuhusu nia ya wapiga mbizi hao.

NZIGE WAVAMIA MADAGASCAR

Nzige wamevamia eneo kubwa la Madagascar na kutishia mimea pamoja na kuzua wasiwasi kuhusu upungufu wa chakula. Kwa mujibu wa shirika la chakula la umoja wa mataifa, (FAO) mabilioni ya mimea iliharabiwa na nzige hao na huenda asilimia sitini ya wananchi wakakumbwa na njaa. Takriban dola milioni 14.5 inahitajika kukabiliana na janga hilo katika nchi ambayo watu wake wengi ni maskini.
Ni janga mbaya zaidi kuwahi kukumba kisiwa hicho tangu mwaka 1950, kwa mujibu wa FAO. Mtaalamu wa kupambana na nzige, Annie Monard, aliambia BBC kuwa janga hilo ni tisho kubwa kwa kisiwa hicho cha bara hindi. "janga la mwisho kama hili kuwahi kutokea ilikuwa miaka ya hamsini na kudumu kwa miaka 17 kwa hivyo ikiwa hakuna hatua zitakazochukuliwa basi huenda ikachukua miaka mitano au kumi kukamilika,'' alisema mtaalamu huyo. Takriban asilimia 60,ya watu milioni 22 wa kisiwa hicho, huenda wakakumbwa na njaa.
Kwa sasa takriban nusu ya nchi imeathirika kutokana na nzige hao, kulingana na shirika la FAO. Shirika hilo linataka, wahisani kuchangisha takriban dola milioni 22 kama msaada wa dharura kwa kufikia mwezi Juni ili kunyunyizia nzige hao dawa. Janga hili la nzige limetishia mifugo na mchele shambani ambacho ni chakula rasmi cha raia wa Madagascar.

VIONGOZI WA KIISLAM MYANMAR WAMLILIA RAIS WAO

Viongozi wa Kiislamu nchini Myanmar wamemuomba Rais Thein Sein kuchukua hatua za haraka kukomesha vurugu, wakivituhumu vyombo vya usalama kwa kuangalia tu wakati waandamanaji wakifanya ghasia. Katika barua ya wazi waliyoituma kwa Rais Thein, makundi manne yakiwemo Baraza la Masuala ya Dini ya Kiislamu na Shirika la Kitaifa la Masuala ya Waislamu, yamesema mashambulizi hayo yanahusisha uhalifu kama vile uchomaji moto na mauaji, ambayo yanastahili adhabu kali, lakini mamlaka zilishindwa kuwachukulia hatua wahalifu ambao wametenda makosa hayo mbele ya macho yao. Watu wasiopungua 40 wameuawa na misikiti kuchomwa katika miji kadhaa katikati mwa Myanmar, tangu kuibuka kwa vurugu mpya za kidini tarehe 20 Machi. Machafuko ya sasa yalisababishwa na mzozo katika duka la kuuza dhahabu, na kugeuka ghasia ambapo misikiti na nyumba vilichomwa, huku miili ya watu iliyoungua ikizagaa barabarani. Lakini mashahidi wanasema vurugu hizo zinaonekana zilipangwa.

WAKOREA KUSINI WARUHISIWA KUINGIA KASKAZINI


Raia wa Korea Kusini wameruhusiwa kusafiri kwenda katika eneo la viwanda linalonedeshwa kwa pamoja nchini Korea Kaskazini, licha ya utawala mjini Pyongyang, kukata mawasiliano ya simu ya kijeshi ya mpakani siku ya Jumatano. Msemaji wa wizara ya muungano ya Korea Kusini amesema karibu watu 400 kutoka Korea Kusini walivuka mpaka pasipo kuchelewesha asubuhi ya leo.
Korea Kaskazini ilikata mawasiliano ya simu inayotumika kuratibu usafiri kwenda na kutoka eneo la viwanda la Kaesong, ambalo ni moja ya vyanzo vya mapato ya kigeni kwa taifa hilo lenye kiwango kikubwa cha umaskini. Karibu kampuni 120 za Korea Kusini zinaendesha shughuli zake katika eneo la Kaesong, na zinaajiri pia wafanyakazi wa Korea Kaskazini. Korea Kaskazini ilisema siku ya Jumatano kuwa ilikuwa inakata mawasiliano hayo, kutokana na tabia za kiuadui kutoka kwa Marekani na Korea Kusini, ambazo zilifanya mazoezi ya kijeshi mwezi huu.

WAPINZANI WA SYRIA WAFUNGUA UBALOZI WAO WA KWANZA QATAR

Upinzani wa Syria unaotambuliwa kama mwakilishi halali wa watu wa Syria na Jumuiya ya n´Nchi za Kiarabu, umefungua ubalozi wake wa kwanza nchini Qatar jana Jumatano, katika pigo la kidiplomasia kwa utawala wa rais Bashar al-Assad. Lakini kiongozi wa muungano wa upinzani huo, Ahmed Moazi al-Khatib, alitumia fursa ya kukata utepe wa kufungua ubalozi huo, ambao uko katika jengo tofauti na lile ulipo ubalozi wa serikali ya rais Assad,  kuelezea kukatishwa tamaa na kushindwa kwa mataifa makubwa kusaidia zaidi harakati za kumuondoa rais Bashar al-Assad. Al-Khatib ambaye alijiuzulu wiki hii kama kiongozi wa muungano wa taifa wa Syria, lakini anaendelea na wadhifa huo kama msimamizi, alizungumzia pia tofauti za ndani zinazoukabili muungano huo, na kusema kuwa njia pekee ya kusonga mbele ni kuwa kitu kimoja.

IRAN YATAKA KUDHIBITIWA UUZAJI WA SILAHA


Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Tehran inaunga mkono Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Biashara za Silaha unaolenga kudhibiti biashara ya silaha duniani.
Ahmadinejad ameyasema hayo Jumatano katika mazungumzo ya simu na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon. Rais Ahmadinejad amesema Iran ni muhanga wa ugaidi na hivyo inaunga mkono kikamilifu mkataba huo.
Rais wa Iran amesema kudhibiti usafirishaji silaha duniani ni jambo linaloweza kusaidia usalama wa kimataifa. Aidha ametaka hatua zichukuliwe kuboresha rasimu ya mkataba huo.
Kongamano la rasimu hiyo linaendelea leo Alkhamisi katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa ambapo kutafanyika juhudi za kudhibiti biashara ya silaha duniani inayokadiriwa kugharimu dola bilioni 70 kwa mwaka. Katika kikao cha Julai 2 hadi 27 mwaka uliopita, nchi wanachama hazikuweza kufikia mwafaka kuhusu rasimu hiyo. Mkataba huo unalenga kuweka viwango vipya vya uuzaji silaha kimataifa.

HAMAS YATOA TAHADHARI KWA ISRAEL JUU YA MASJIDUL AQSAA


Katika radiamali yake kuhusiana na wito uliotolewa na mwakilishi  mmoja wa Bunge la Israel (Knesset)  kwa Wazayuni wa kusherehekea sikukuu ya Kiyahudi katika msikiti wa al Aqsa, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imewatahadharisha viongozi wa utawala huo na kuwataka wajiepushe na hatua hiyo ya kishenzi.
Sambamba na kulaani wito huo wa Moshe Feiglin mwakilishi wa Bunge la Israel kwa Wazayuni wa kusherehekea sikukuu ya Kiyahudi ya 'Pasaka'  katika msikiti wa al Aqsa, Hamas imezitaka nchi za Kiislamu na taifa la Palestina kukabiliana na mpango  huo wa kidhulma wa adui Mzayuni wa kutaka kuhujumu msikiti huo. Hamas pia imetahadharisha kwamba Wazayuni ndio watakaobeba lawama na taathira mbaya za kusherehekea Pasaka katika Msikiti wa al Aqsa ambao ni kibla cha mwanzo cha Waislamu. Awali Taasisi ya Wakfu na Turathi ya al Aqsa pia ilitahadharisha juu ya athari mbaya za kusherehekea Pasaka katika msikiti huo na kutaka jamii ya kimataifa hasa nchi za Kiislamu na Kiarabu zichukuwe hatua za haraka na zenye taathira za kukabiliana na jinai na hujuma za Wazayuni dhidi ya msikiti huo zinazozidi kila uchao.
Hivi karibuni askari na walowezi wa Kizayuni wamekuwa wakijikusanya kwenye ua wa Masjidul Aqsa kwa lengo la kuingia kwenye msikiti huo mtukufu, ambapo Wapalestina walizima njama hizo. Walowezi wa Kizayuni na Wazayuni wenye misimamo mikali kwa visingizio tofauti kama kusherehekea sikukuu ya kidini ya Pasaka, siku zote wamekuwa wakitaka kuhujumu Msikiti wa al Aqsa na Baitul Muqaddas. Wazayuni wenye misimamo ya kufurutu ada wanaosaidiwa na askari wa Israel wanaendelea kuhujumu maeneo matakatifu ukiwemo Msikiti wa al Aqsa huku nchi za Kiarabu zikinyamazia jinai hiyo na kuishia tu kutoa maneno matupu. Kuhusu suala hilo viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu katika mkutano wao wa 24 uliofanyika Jumanne nchini Qatar, walichukuwa hatua ya kimaonyesho tu wakiitaka Israel iondoe vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina na kuacha kuhujumu Msikiti wa al Aqsa.
Nchi za Kiarabu zinanyamazia kimya hujuma za Wazayuni dhidi ya msikiti huo na kadhia nzima ya Palestina, katika hali ambayo hujuma zinazokaririwa na askari wa Kizayuni dhidi ya msikiti huo wa kihistoria, msikiti wa Qubbatus Swakhra na makanisa katika mji wa Quds Sharif zimekuwa zikilaaniwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO). Zaidi ya hayo vitongoji vya walowezi wa Kizayuni vilivyojengwa katika ardhi za Palestina vimekuwa vikipingwa na kukosolewa na jamii ya kimataifa. Kwa kuzingatia hayo inaonekana kuwa, njia pekee iliyobakia ni taasisi za kimataifa kutafuta suluhisho la kudumu litakalozuia kuendelea siasa za utawala wa Kizayuni za kupenda kujitanua katika ardhi za Palestina.

RED CROSS YATUMA UJUMBE KWENDA JELA YA GUANTANAMO


Kamati ya Kimataifa ya shirika la Msalaba Mwekundu (ICRC) imetuma ujumbe katika jela ya Marekani ya Guantanamo Bay huko Cuba wiki moja kabla ya muda uliopangwa, kwa kuhofia kuendelea mgomo wa kula unaofanywa na mahubusu wanaoshikiliwa kwenye jela hiyo.
Msemaji wa ICRC Simon Schorno amesema, makumi ya wawakilishi wa jumuiya hiyo na daktari wameelekea kwenye jela hiyo ya kutisha ya Marekani. Taarifa zinasema kuwa, mgomo wa kula wa wafungwa wa jela ya Guantanamo umeingia siku ya 50, ambapo wafungwa 31 wanagoma kula kwenye jela hiyo. Maafisa wa jela hiyo wanasema kwamba, mahabusu watatu wanaogoma kula wamelazwa hospitali baada ya hali zao kuwa mbaya. Wafungwa wa jela hiyo walianza kugoma kula Februari 6 wakilalamikia uamuzi wa maafisa wa jela hiyo wa kuwanyang'anya baadhi ya vitu vyao binafsi kama barua, cd, picha na nakala za kitabu kitukufu cha Qur'ani.
Jela hiyo ya Marekani ina mahabusu 166 kutoka nchi mbalimbali duniani na watetezi wa haki za binadamu wamekuwa wakikosoa vikali Marekani kutokana na mateso na manyanyaso yanayofanywa dhidi ya wafungwa wa jela hiyo.

KIONGOZI WA WAASI WA JAMHURI YA KATI AJIPANGA KUTANGAZA SERIKALI YAKE


Kiongozi wa Waasi wa Kundi la Seleka ambaye amejitangaza Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Michel Djotodia anatarajiwa kutangaza serikali yake ambayo ameahidi itakaa madarakani kwa kipindi cha miaka mitatu kabla ya kuitisha uchaguzi mkuu. Serikali hiyo mpya inatarajiwa kushika nafasi ya ile iliyoangushwa ya Rais Francois Bozize ili kuongoza nchi hiyo ambayo imetengwa na Umoja wa Afrika AU pamoja na Umoja wa Mataifa UN ambao umelaani mapinduzi hayo. Djotodia amesema kuwa Serikali atakayoiunda itakuwa na jukumu la kuhakikisha inaimarisha usalama wa nchi hiyo pamoja na kuleta utangamano miongoni mwa wananchi ambao walikuwa wamegawanyika wakati wa utawala wa Bozize.
Kiongozi huyo ameongeza kuwa wakati huu ambapo aiunda Serikali, ameunda kikosi maalumu cha askari ambacho kitakuwa na jukumu la kuhakikisha kinawashughulikia wale wote ambao wanadaiwa kushiriki katika vitendo vya uvunjifu a amani ambapo wakati wanaingia kwenye mji huo wanajeshi wa Seleka waliripotiwa kupora mali. Jumuiya ya kimataifa imelaani matukio ambayo yamekuwa yakifanywa na wanajeshi wa Seleka wanaodaiwa kushiriki vitendo vya uvunjifu wa amani kwa kuwanyanyasa raia pamoja na kuwalazimisha kuchukua mali zao kwa nguvu.
Hali ya machafuko imesababisha madhara makubwa kwa vijana na hata wengine kujikuta wakiingia kwenye vitendo vya uporaji nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati jambo ambalo limeainishwa pia na shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na watoto UNICEF. Serikali ya Seleka imekumbana na ukosoaji mkubwa kutokana na kuiangusha serikali halali huku Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UNSC likiahidi kuchukua hatua madhubuti dhidi yao.

SERIKALI YA UINGEREZA YASHINDWA RUFAA YA SHEIKH ABU QATADA


Serikali ya Uingereza kwa mara nyingine imeshindwa kwenye mahakama kuu ya nchi hiyo kwenye rufaa waliyokuwa wamekata wakitaka kurejeshwa nchini Jordan kwa mtuhumiwa wa vitendo vya ugaidi Sheikh, Abu Qatada. Katika hukumu ambayo ilikuwa inasubiriwa kwa hamu kubwa na Serikali ya Uingereza, majaji watatu waliokuwa wakisikiliza rufaa hiyi walijiridhisha na upande wa utetezi ambao uliwasilisha nyaraka zinazoonesha kuwa Abu Qatada akirejeshwa nchini Jordan atafanyiwa vitendo vya unyanyasaji. Katika kufikia uamuzi wao majaji hao wamekataa ombi la Serikali ya Uingereza kutaka kumsafirisha kiongozi huyo wa kidini kwenda nchini Jordan kukabiliana na mashtaka ya ugaidi ambayo yanamkabili.

Ofisi ya wizara ya mambo ndani nchini humo kwenye taarifa iliyoichapisha kwenye mtandao wa Twitter, imesema kuwa bado haijakata tamaa dhidi ya kutaka kumrejesha nchini Jordan kiongozi huyo na kwamba wanajiandaa kuwasilisha ombi jingine la kwanini kiongozi huyo arejeshwe nchini Jordan. Abu Qatada alikamatwa hivi karibuni na maofisa uhamiaji kwenye mpaka wa nchi ya Uingereza na kudai kuwa kiongozi huyo alipanga kutoroka jambo ambalo mawakili wake walilikanusha. Hata hivyo kiongozi huyo kwa mara nyingine ameachiwa kwa dhamana licha ya kukiuka matakwa ya dhamana aliyokuwa amepatiwa hapo awali.

Wednesday, March 27, 2013

KOREA KASKAZINI YAKATA MAWASILIANO NA KUSINI

Jeshi la Korea Kaskazini leo limekata mawasiliano ya simu na Korea Kusini, na kusitisha mawasiliano ya mwisho ya moja kwa moja baina ya nchi hizo mbili, katika wakati ambapo kuna hofu kubwa ya kijeshi. Hatua hiyo imechukuliwa sambamba na tangazo kwamba viongozi wakuu wa kisiasa wa Korea Kaskazini watakutana katika siku chache zijazo kujadili kuhusu "suala muhimu" na kufanya uamuzi wa kurudi nyuma. Hatua ya kukata mawasiliano ya simu imetangazwa na afisa wa ngazi ya juu wa jeshi la Kaskazini kwa mwenzake wa kusini muda mfupi kabla ya kukatwa laini hizo za simu. Wiki chache zilizopita, Korea Kaskazini ilikata laini za simu za Shirika la Msalaba Mwekundu ambazo zilikuwa zimetumiwa katika mawasiliano ya kiserikali bila kuwepo uhusiano wa kidiplomasia. Hatua hiyo ya kukatwa mawasiliano ya simu ndiyo ya karibuni katika msururu wa vitisho na hatua kutoka serikali ya Pyongyang na kuongeza hofu katika Rasi ya Korea tangu uzinduzi wa Korea Kaskazini wa kombora la masafa marefu mwezi Desemba na majaribio yake ya nyuklia mwezi uliopita.

WAPALESTINA WAZUILIWA KUSWALI KWENYE HARAM YA NABII IBRAHIM


Chuo Kikuu cha al Azhar nchini Misri kimelaani vikali hatua ya viongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuwazuia Waislamu kuingia na kufanya ibada kwenye Haram tukufu ya Nabii Ibrahim AS na badala yake wamefungua milango kwa walowezi wa Kizayuni kuingia kwenye eneo hilo takatifu. Viongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel kuanzia leo na kesho wamewazuia Waislamu kufanya ibada zao kwenye eneo hilo tukufu na badala yake wamewaruhusu walowezi wa Kizayuni kwa kisingizio cha kuadhimisha sikukuu za Kiyahudi.
Chuo Kikuu cha al Azhar kimesisitiza kuwa, Haram takatifu ya Nabii Ibrahim AS ni msikiti kamili na wala hauna mfungamano na Mayahudi na hali kadhalika haupasi kuvunjiwa heshima kwa namna yoyote ile. Taarifa hiyo imetahadharisha juu ya kuongezeka vitendo vya kulivunjia heshima eneo hilo, suala ambalo imesema linaziumiza nyoyo za zaidi ya Waislamu bilioni moja na nusu duniani. Taarifa hiyo pia imewataka Waislamu wote duniani na Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za kukomesha haraka uvamizi huo.

ALSHABAB WAHUSISHWA NA UBAKAJI SOMALIA


Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch (HRW) limewatuhumu wanajeshi wa serikali ya Somalia na kundi la wanamgambo wa Al Shabab kwa kuwabaka na kuwanajisi wakimbizi wanawake walioko kwenye kambi za wakimbizi pambizoni mwa Mogadishu, mji mkuu wa Somalia.
Taarifa iliyotolewa leo na shirika hilo imeeleza kuwa, wanawake ambao walikimbilia kwenye kambi hizo wakihofia mashambulizi ya makundi yanayobeba silaha na baa la njaa wamekuwa katika wakati mgumu baada ya kukabiliwa na vitendo vya kikatili vya kubakwa na kunajisiwa na wanamgambo wa kundi la al Shabab pamoja na baadhi ya wanajeshi wa serikali la Somalia. Taarifa hiyo imeeleza kuwa, hali ya wakimbizi hao bado haijaboreka ijapokuwa serikali mpya iliyochukua madarakani mwezi Septemba mwaka uliopita iliahidi kulishughulikia kikamilifu suala hilo. Kundi la al Shabab ambalo linafungamana na mtandao wa al Qaeda linadhibiti baadhi ya maeneo ya katikati na kusini mwa Somalia na limekuwa likivishambulia vikosi vya serikali na vile vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika AMISOM.

IRAN YALALAMIKIA MADAU YA SAUDI ARABIA


Iran imemuita balozi mdogo wa Saudi Arabia hapa Tehran na kumkabidhi malalamiko kuhusu madai ya Saudia kuwa Jamhuri ya Kiislamu inafungamana na mtandao wa kijasusi katika ufalme huo wa Kiarabu.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imembainishia mwanadipolmasia huyo wa Saudia malalamiko makali ya Iran kuhusu madai yasiyo na msingi na yanayokaririwa mara kwa mara na Saudia. Iran aidha imeitaka Saudi Arabia itoe maelezo rasmi kuhusu kadhia hiyo. Balozi wa Saudi Arabia nchini Iran hakuwepo na hivyo balozi mdogo ndiye aliyekabidhiwa malalamiko yao.
Wakati huo huo wanazuoni kadhaa wa Kiislamu nchini Saudi Arabia wameutaka utawala wa Riyadh kuwaachilia huru watu 18 waliotiwa mbaroni kwa madai ya kuwa na uhusiano na Iran. Watu hao 18 wamekanusha tuhuma dhidi yao na kusema utawala wa Saudia unajaribu kupotosha fikra za umma kuhusu matakwa ya wananchi wanaotaka marekebisho nchini humo. Kuna karibu wafungwa 30 elfu wa kisiasa kote Saudia ambao wanashikiliwa pasina kufunguliwa mashtaka au baada ya muhula wa vifungo vyao kumalizika.

LARIJANI ASIFU UWEZO JESHI LAKE


Ali Larijani Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran amesema vikosi vya kijeshi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndio vikosi bora katika kanda hii. Larijani ameyasema hayo leo Jumatano alipokutana na makamanda wa Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika eneo la Konarak, kusini mashariki mwa Iran. Larijani ameongeza kuwa harakati za nchi za Magharibi katika eneo la Ghuba ya Uajemi zinatokana na hofu yao kuhusu jeshi la Iran lenye nguvu na uzoefu.
Larijani ameongeza kuwa kundi la 5+1 linapofanya mazungumzo na Iran hubainisha masuala kinyume na inavyoashiriwa katika vyombo vya habari. Amesema kundi hilo linalojumuisha nchi za China, Russia, Ufaransa, Uingereza, Marekani na Ujurumani wakati zikiwa katika mazungumzo hukiri kuwa tatizo la nchi za Magharibi na Iran si kadhia ya nyuklia bali tatizo ni kuwa hivi sasa Iran inaibuka kama nchi yenye nguvu, yenye kujitegemea na iliyo na vikosi imara vya kijeshi. Larijani amesema Iran ndio nchi pekee katika eneo yenye utawala wa Kiislamu unaotegemea nguvu za wananchi. Ameongeza kuwa hakuna shaka kuwa mwamko wa Kiislamu katika eneo hili umepata ilhamu na mvuto kutoka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

IRAQ YAPINGA WAASI WA SYRIA KUPEWA UANACHAMA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq, Hoshyar Zebari amelaani hatua ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) ya kuwapa uanachama magaidi wa Syria kwenye jumuiya hiyo. Zebari amesema hatua hiyo inakiuka sheria na katiba ya Arab League. Akifafanua zaidi nukta hiyo, Hoshyar Zebari amesema wanachama wa jumuiya hiyo ni serikali za nchi za Kiarabu zilizochaguliwa kidemokrasia na wananchi na wala sio makundi yanayobeba silaha. Amesisitiza kwamba, magaidi wa Syria wanaungwa mkono zaidi na nchi za kigeni na hilo linakiuka vipengee muhimu vya mkataba wa kuundwa Jumuiya hiyo. Iraq ambayo kwa sasa ndiyo mwenyekiti wa kiduru wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imekuwa ikisisitiza kuwa njia pekee ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa Syria ni kupitia mazungumzo kati ya serikali na waasi. Radiamali ya Iraq inakuja siku moja baada ya Arab League kuchukua nafasi ya Syria katika jumuiya hiyo na kuwapa magaidi wanaopigana na serikali ya Rais Bashar Asad.  

JESHI LA ISRAEL LAWAKAMATA VIONGOZI WA HAMAS

Jeshi la utawala haramu wa kizayuni wa Israel limewatia nguvuni viongozi 3 waandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS baada ya kushambulia makaazi yao katika mji wa Khalil. Habari zinasema kuwa, wanajeshi wa Kizayuni wamemtia nguvuni Mohammad Jamal mwenye umri wa miaka 55 baada ya kumvurugia nyumba yake na kuchukua vitu vyake vya kibinafsi zikiwemo kompyuta na simu ya mkononi. Wazayuni hao maghasibu pia wamewakamata Amjad Hamouri na Abdul-Khaliq Natshe na kuwapeleka katika eneo lisilojulikana. HAMAS imelaani hujuma hiyo na kusema inakiuka makubaliano ya usitishaji vita yaliyomaliza mapigano ya siku 8 kati ya pande mbili hizo mwaka uliopita. Utawala haramu wa Israel umeendelea kukiuka haki za wapalestina sambamba na kukanyaga sheria za kimataifa huku Jamii ya kimataifa ikiendelea kuwa kimya. Uungaji mkono wa hali na mali wa Marekani ndio sababu ya kuendelea kuvimba kichwa  utawala huo haramu wa Kizayuni.

KOREA YASEMA VITA YA NYUKLIA INAKARIBIA

Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini imetoa taarifa kwa Umoja wa Mataifa ikisema vita vya nyuklia vinanukia katika Peninsula ya Korea. Taarifa ya Pyongyang kwa Umoja huo inasema kuwa, Marekani na Korea Kusini zinaendelea na chokochoko katika eneo hilo; jambo linalotishia kuanza kwa vita vya silaha za nyuklia. Taarifa hiyo pia imesisitiza kuwa, Korea Kaskazini itatumia kila njia kulinda ardhi na uhuru wake hata kama italazimika kutumia makombora ya nyuklia. Vitisho hivyo vimetajwa kuwa hatari zaidi kuwahi kutolewa na Pyongyang na kutokana na hali hiyo, Marekani imetangaza kuwa imeimarisha ngao zake dhidi ya makombora ili kukabiliana na vitisho hivyo. Majuma mawili yaliyopita, Korea Kaskazini ilitishia kuzishambulia Marekani na Korea Kusini kutokana na nchi mbili hizo kufanya maneva ya pamoja ya kijeshi katika Peninsula ya Korea. Pyongyang ilisema maneva hayo ni tangazo la moja kwa moja la vita dhidi yake. Tayari Korea Kaskazini imejiondoa kwenye mkataba wa usitishaji vita wa mwaka 1953 uliohitimisha vita kati yake na nchi jirani ya Korea Kusini.

RAIS WA SUDAN ATAKA WAASI KUSHIRIKI KATIBA MPYA

Makamu wa kwanza wa rais wa Sudan, Ali Osman Taha ametoa wito kwa makundi ya waasi kushiriki mchakato wa kuunda katiba mpya ya nchi hiyo. Katika hali isiyo ya kawaida, Taha amewakaribisha Malik Agar na Abdul-Aziz al-Hilu; viongozi wa kundi la waasi la SPLM-North na kusema kwamba, kushiriki kwao kwenye mchakatu wa kuandika katiba mpya utahitimisha fujo na tandabelua katika majimbo ya Blue Nile na Kordofan Kusini. Makamu wa kwanza wa rais wa Sudan aidha amesema katiba mpya itafungua milango ya kuelekea kwenye demokrasia halisi pamoja na kuleta amani na utulivu ndani na nje ya Sudan. Vita na rangaito katika mikoa ya Kordofan Kusini na Blue Nile vilianza punde baada ya Sudan Kusini kujitenga na Sudan mwezi Julai mwaka 2011 na nchi mbili hizo zimekuwa zikinyoosheana kidole cha lawama kuhusu uungaji mkono wa waasi katika majimbo hayo yaliyoko kwenye mpaka wao wa pamoja.

RUSSIA YAITAKA LEBANON KUTATUA MATATIZO YAKE WENYEWE

Serikali ya Russia imewataka Walebanon kuzuia uingiliaji wa aina yoyote ile wa madola ya kigeni katika mambo ya ndani ya nchi hiyo. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia Alexander Lukashevich ameyasema hayo leo na kusisitiza kuwa, nchi yake inaamini kwamba, Walebanon lazima watatue matatizo ya taifa lao wao wenyewe kwa njia za mazungumzo, likiwamo suala la uundwaji wa serikali mpya na kufanyika uchaguzi wa bunge na wasitoe mwanya kwa wageni kuingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo. Aidha ripoti hiyo imesisitiza kuwa, suala la usalama na utulivu nchini Lebanon ni jambo ambalo linapaswa kupewa kipaumbele na kwamba, taifa hilo la Kiarabu lazima lichukue hatua za lazima zitakazoiletea maslahi nchi hiyo na kusaidia demokrasia ya kweli na kuhakikisha usalama na ustawi unapatikana nchini humo. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia piaamesema kuwa, nchi yake inaunga mkono haki ya kujitawala, uhuru wa nchi na juhudi zote zinazofanywa na makundi ya kisiasa na kidini ya Lebanon katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili nchi hiyo hivi sasa. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, siku ya Jumamosi, Waziri Mkuu wa Lebanon, Mohammad Najib Mikati, alitangaza kujiuzulu na Rais Michel Suleiman wa nchi hiyo akakubali kujiuzulu kwake.

WAFUNGWA WA GUANTANAMO WAUNGWA MKONO

Wanaharakati wa haki za binaadamu katika pembe mbalimbali za dunia wameendelea kuunga mkono mgomo wa chakula wa wafungwa wa jela ya Guantanamo. Kwa mujibu wa ripoti iliyotangazwa na televisheni ya PRESS TV, mgomo wa wanaharakati hao wa haki za binaadamu katika pembe mbalimbali za dunia unafanyika kama ishara ya kuungana na wafungwa hao wanaoendelea kuzuiliwa katika jela ya kutisha ya Guantanamo. Mgomo huo ulianza tarehe 24 Machi na unatarajia kuendelea hadi tarehe 30 ya mwezi huu. Mbali na mgomo huo, wanaharakati hao wamepanga kufanya mikusanyiko kadhaa katika nchi kadhaa katika kuwaunga mkono wafungwa hao. Tarehe 14 mwezi huu mawakili 45 wanaowatetea baadhi ya wafungwa wanaoshikiliwa katika jela hiyo ya Guantanamo walimtumia barua ya wazi Waziri wa Ulinzi wa Marekani Chuck Hagel wakimtaarifu kuhusu suala hilo na kumtaka achukue hatua za haraka ili kumaliza mgomo huo. Wafungwa hao walianza mgomo huo tangu Februari 6 mwaka huu baada ya wafanyakazi wa jela hiyo ya Guantanamo kupora vitu vya wafungwa hao zikiwemo barua, picha na kuzivunjia heshima nakala za kitabu kitukufu cha Qu'rani wakati walipozikagua seli zao.

SHAMBULIO LA BOMU LAUA MMOJA RWANDA


Mripuko wa guruneti uliotokea mjini Kigali Rwanda umeua mtu mmoja na kuwajeruhi wengine wanane. Msemaji wa polisi ya Rwanda ameeleza kuwa guruneti hilo liliripuka jana jioni katika sehemu iliyoko baina ya kituo cha basi na soko moja kwenye eneo la Kimironko katika mji mkuu Kigali. Baadae polisi ilisema kupitia ukurasa wake wa twitter kwamba watu wawili wametiwa mbaroni kwa kushukiwa kutekeleza shambulio hilo. Itakumbukwa kuwa milipuko mingine mitatu ya maguruneti ilitokea nchini Rwanda katika kipindi kama hiki mwaka jana yaani katika mwezi Machi. Mlipuko mmoja wa guruneti uliua mtu mmoja na kuwajeruhi wengine watano huko kaskazini mwa Rwanda na milipuko mingine miwili  iliwajeruhi watu sita huko Kigali. Rwanda imekuwa ikikabiliwa na milipuko ya guruneti tangu mwaka 2010 huku serikali ikiwanyooshea kidole cha tuhuma maafisa wawili wa ngazi za juu wa jeshi la nchi hiyo waliokimbilia uhamishoni.

MISIKITI NA NYUMBA KADHAA ZA WAISLAM ZACHOMWA MOTO MYANMAR


Misikti miwili na nyumba kadhaa za Waislamu zimeteketezwa kwa moto katika mashambulizi mapya dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar. Afisa wa polisi ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema kuwa mashambulizi hayo yametokea katika vijiji vya eneo la Bago kaskazini mwa mji wa Yangon siku ya Jumatatu.
Amesema hakuna habari zozote kuhusu mauaji katika mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya Waislamu walio wachache katika nchi hiyo ya kusini mashariki mwa Asia.
Mnamo Machi 20 Mabuddha wenye misimamo mikali waliteketeza kwa moto nyumba za Waislamu na misikiti katika mji wa Meiktila nchini Myanmar ambapo watu 40 waliuawa na wengine 12,000 kuachwa bila makao. Wakati huo huo mshauri wa Umoja wa Mataifa kuhusu Myanmar, Vijay Nambiar, ameitaka serikali ya nchi hiyo kuwaadhibu wanaofanya mashambulizi dhidi ya Waislamu.
Inafaa kukumbusha hapa kuwa, serikali ya Myanmar inawabagua, inawatesa na kuwakandamiza Waislamu wa Rohingya ambao idadi yao inafikia laki nane kwa madai kwamba, Waislamu hao ni wakimbizi waliokimbilia nchini humo wakitokea nchini Bangladesh.

Tuesday, March 26, 2013

KOREA KASKAZINI YAELEKEZA MIZINGA YAKE KWA VITUO VYA MAREKANI


Korea ya Kaskazini imeamuru mizinga yake iwekwe katika hali ya kivita, ikivilenga vituo vya  Marekani. Hayo yametangazwa na vyombo vya habari katika mji mkuu wa nchi hiyo, Pyongyang. Vikosi vya maroketi na mizinga ya masafa marefu vimetakiwa kuwa katika hali ya tahadhari, vikilenga Marekani na visiwa vyake vya Hawaii na Guam, ambako kuna kambi za jeshi la nchi hiyo. Shirika la habari la Korea KCNA limeripoti kuwa kiongozi wa Korea ya Kaskazini Kim Jong Un jana aliwatembelea wanajeshi walioko msitari wa mbele.
Korea ya Kaskazini imejenga zana za nyuklia, lakini haiaminiwi kuwa na uwezo wa kufyatua makombora ya masafa marefu. Utawala wa nchi hiyo ambao umetengwa na nchi nyingi duniani, siku za hivi karibuni umekuwa ukitoa vitisho kwa Korea Kusini na mshirika wake Marekani, baada ya nchi hizo kuanzisha mazoezi ya kijeshi pamoja katika eneo linalozunguka rasi ya Korea.

ISRAEL YAACHIA FEDHA ZA KODI KWA PALESTINA


Israel imesema itaanza tena kuipa mamlaka ya wapalestina fedha zinazotokana na kodi ambazo Israel huzikusanya kwa niaba ya mamlaka ya utawala wa Palestina. Fedha hizo zilisimamishwa baada ya Palestina kuomba na kupata hadhi ya mwanachama wa Umoja wa Mataifa asiye taifa huru.
Tangazo kuhusu kuachiwa kwa fedha hizo ambalo limetolewa na ofisi ya waziri mkuu Benjamin Netanyahu halikutoa maelezo zaidi kwa nini hatua imechukuliwa. Marekani na Israel zilipinga ombi la wapalestina kupandishwa hadhi na Umoja wa Mataifa na kuwa mwanachama asiye taifa.

IRAN YAITAKA UN IZUIE MATUMIZI YA KEMIKALI SYRIA

Dk Ali Akbar Salehi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameutaka Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za kuzuia kukaririwa tena utumiaji wa silaha za kemikali uliofanywa na makudi ya kigaidi nchini Syria. Salehi amemuandikia barua Ban Ki-Moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambapo sanjari na kulaani kitendo cha magaidi wa Syria cha kutumia silaha za kemikali ameutaka umoja huo ufanye uchunguzi kuhusiana na jinai hizo za waasi na kuchukua hatua za lazima za kuzuia kukaririwa tena kitendo kama hicho. Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesisitiza katika barua yake kwa Ban Ki-Moon kwamba, kuna haja kwa Umoja wa Mataifa kutuma timu ya wachunguzi huko Syria ili kufanya uchunguzi kuhusiana na jinai zilizofanywa na waasi hao wanaofanya mauaji kila leo dhidi ya raia katika nchi hiyo ya Kiarabu. Aidha Ali Akbar Salehi amesisitiza kwamba, hatua ya waasi wa Syria ya kutumia silaha za kemikali katika mji wa Halab ni tishio la wazi kabisa dhidi ya amani na usalama na kwamba, hatua hiyo inakiuka wazi sheria za kimataifa na mikataba ya kimataifa hususan mkataba wa silaha za kemikali.

NAFASI YA CIA KATIKA KUYAPA SILAHA WAASI WA SYRIA

Gazeti la New York Times la nchini Marekani limeandika kuwa, serikali za nchi za Kiarabu na Uturuki kwa kusaidiwa na Shirika la Kijasusi la Marekani CIA mwaka jana ziliyapelekea tani 3500 za silaha makundi ya kigaidi yanayofanya mauaji nchini Syria. Gazeti hilo limetegemea taarifa za minara ya kuongozea ndege, mahojiano na viongozi wa nchi mbalimbali na matamshi ya makamanda wa makundi ya waasi nchini Syria na kuandika kuwa, serikali za nchi za Kiarabu na Uturuki katika miezi ya hivi karibuni pia zimeongeza misaada yao ya kijeshi kwa makundi ya kigaidi nchini Syria. Taarifa za kijasusi zinasema kuwa, jambo hilo lilianza mwanzoni mwa mwaka 2012 kwa kutumwa shehena ndogo nadogo na likaendelea mtawalia hadi mwishoni mwa msimu uliopita wa mapukutiko na kuongezeka mno katika miezi ya mwishoni mwa mwaka jana. Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya New York Times, shehena hizo za silaha zinajumuisha zaidi ya shehena 160 za kijeshi zilizotoka kwa serikali za Jordan, Saudi Arabia na Qatar na kupelekwa katika viwanja vya ndege kadhaa vya Urutuki na baadaye kutumiwa magenge ya kigaidi nchini Syria. Gazeti hilo la Marekani limekiri pia kuwa, kutumwa shehena hizo za silaha kulileta mabadiliko katika vita vya ndani vya Syria. Limeandika kuwa, katika hali ambayo Rais Barack Obama wa Marekani alikuwa anadai kwamba anapinga kutumwa msaada wowote ule kwa waasi wa Syria isipokuwa wa kiraia, Shirika la Kijasusi la Marekani CIA lilitoa mchango mkubwa wa kutumwa silaha kwa magenge ya waasi ya Syria jambo ambalo linaonesha kuwa Marekani ina hamu ya kuona machafuko nchini Syria yanaendelea kupitia kuwaunga mkono waitifaki wake wa Kiarabu. Maafisa waandamizi wa Marekani ambao hawakutaka majina yao yatajwe nao wamesema kuwa, maajenti wa CIA wamezisaidia nchi za Kiarabu kununua silaha hizo na kuzituma kwa makundi ya kigaidi huko Syria. Serikali ya Uturuki nayo imekuwa na mchango mkubwa sana katika jambo hilo. Wachambuzi wa masuala ya kudhibiti silaha za magendo wanasema kuwa, tani 3500 za silaha ni shehena kubwa sana na hili linaonesha ni kiasi gani taifa la Syria lilivyoshikamana na serikali yao pamoja na uimara wa utawala wa Rais Bashar al Assad kiasi kwamba umeweza kukabiliana vilivyo na ugaidi huo unaoiandama Syria kutoka kila mahala. Baada ya kuchaguliwa tena Obama kuwa Rais wa Marekani, viongozi wa Washington wamejitokeza na mikakati mipya ya kuzidi kushirikiana na Ufaransa, Uingereza, Uturuki, Saudia na Qatar kuyasheheneza silaha hatari hata za kemikali, makundi ya kigaidi huko Syria. Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, ni kichekesho kuzisikia Marekani na waitifaki wake hasa Uingereza, Ufaransa, Uturuki, Saudia na Qatar zikidai kuwa zinataka kuutatua mgogoro wa Syria wakati ndizo zinazochochea mauaji na ukatili wa makundi ya waasi yasiyo na chembe ya ubinaadamu huko Syria.

12 WAUAWA SHAMBULIO LA TALIBAN

Kwa akali watu 12 wameripotiwa kuuawa nchini Afghanistan kufuatia shambulio la wanamgambo wa Taliban mashariki mwa nchi hiyo. Duru za usalama zinaripoti kwamba, wanamgambo wa Taliban wamefanya shambulio katika kituo kimoja cha polisi mashariki mwa nchi hiyo na kupelekea watu 12 kuuawa wakiwemo polisi watano. Taarifa zaidi zinasema kuwa, kituo kimoja cha polisi katika mji wa Jalal-Abad kimeshambuliwa kwa mabomu yasiyopungua saba. Kundi la wanamgambo wa Taliban limetangaza kuhusika na shambulio hilo ambalo limepelekea pia makumi ya watu kujeruhiwa. Nchi ya Afghanistan inaendelea kushuhudia hali ya mchafukoge na ukosefu wa amani, licha ya kuweko vikosi vya kigeni vinavyoongozwa na Marekani ambavyo vinadai viko katika nchi hiyo kwa ajili ya kurejesha amani na utulivu.

CHRISTIAN RONALDO AKATAA KUBADILISHANA JEZI NA MUISRAEL


Christiano Ronaldo nahodha na mshambuliaji machachari wa timu ya taifa ya Ureno na klabu ya Real Madrid ya Uhispania amekataa kubadilishana jezi na mchezaji mwenzake wa utawala wa Kizayuni wa Israel, mara baada ya kumalizika mechi kati ya timu hizo mbili za kuwania tiketi ya kucheza fainali ya kombe la dunia mwaka 2014 nchini Brazil iliyochezwa hivi karibuni huko Tel Aviv, Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Takwa la mchezaji wa Israel la kubadilishana jezi na Ronaldo lilikataliwa katika hali ambayo, wachezaji wote waliobakia wa Ureno walikubali kubadilishana jezi na wale wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Kitendo cha kubadilishana jezi ni cha kawaida, na hasa kinaonyesha upendo na kinabaki kuwa kumbukumbu kwa wachezaji hao.
Aidha pambano hilo la kundi F, lilimalizika kwa timu hizo mbili kutoshana kwa  sare ya kufungana mabao 3-3. Ureno ilitangulia kupachika bao katika dakika ya 2 lililofungwa na Bruno Alves, na baada ya hapo Israel ilichachamaa na kusawazisha katika dakika ya 40, na kupachika mabao mengine mawili katika dakika za 40 na 70 yaliyofungwa na Ben Basat na Gershon. Ureno nusura iumbuke ugenini, lakini Fabio Coentrao anayechezea Real Madrid ya Uhispania alisawazisha katika dakika za majeruhi 90+3. Ronaldo aliulizwa swali la kichokozi  na lenye mtazamo wa kisiasa na mwandishi mmoja wa habari juu ya suala la nchi ya Israel na kujibu; anachojua yeye ni kwamba amecheza mechi hiyo nchini Palestina, na wala siyo Israel.
Inafaa kuashiria hapa kuwa, mara baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel kushambulia eneo la Ukanda wa Gaza mwishoni mwa mwaka 2012, Ronaldo alitoa msaada wa kiasi cha euro milioni moja na nusu kwa ajili ya ukarabati wa shule ilizobomolewa kwa makombora ya ndege za utawala wa Israel. Aidha mwaka 2011 aliwahi kutoa viatu vyake na kupigwa mnada na fedha zilizopatikana alizikabidhi kwa Wapalestina kwa minajili ya kujenga na kukarabati shule za eneo la Ukanda wa Gaza.

WAISLAM WA UFARANSA WASHIKAMANA ZAIDI NA UISLAM


Uchunguzi wa maoni uliofanywa na Taasisi ya Sociovision nchini Ufaransa unaonesha kuwa, Waislamu nchini humo wanafungamana zaidi na misingi na thamani za kidini kuliko wafuasi wa dini nyingine za mbinguni.
Uchunguzi huo uliotolewa na taasisi hiyo hivi karibuni unaonesha kuwa, asilimia 68 ya Waislamu wa Ufaransa wanashikamana zaidi na thamani na misingi ya dini tukufu ya Kiislamu kuliko wafuasi wa dini nyinginezo. Uchunguzi uliofanywa mwezi Februari baina ya Waislamu, Wakristo na Mayahudi nchini humo unaonesha kuwa, asilimia 40 ya Mayahudi wanafungamana na thamani za kidini na asilimia 60 wanafungamana na thamani za kitaifa. Uchunguzi huo umeonesha kuwa, asilimia 63 ya Wakristo wanafungamana na thamani za kiutaifa na asilimia 37 tu ndiyo inashikamana na misingi na thamani za kidini. Kwa upande mwingine ripoti iliyochapishwa hivi karibuni na gazeti la New York Time la nchini Marekani inaonyesha kuwa, kasi ya kuongezeka wafuasi wa dini ya Kiislamu nchini Ufaransa imeongezeka maradufu katika kipindi cha miaka 25 iliyopita.