Sunday, June 30, 2013

UMOJA WA ULAYA WATAKA UFAFANUZI TOKA MAREKANI

Rasi wa bunge la Ulaya Martin Schulz amesema anahitaji maelezo ya kina kutoka kwa Marekani baada ya shutuma mpya za kijasusi dhidi ya nchi hiyo. Martin Schulz amesema anawasi wasi mkubwa na kufadhaishwa juu ya madai ya Marekani kuzifanyia upepelezi ofisi za Umoja wa Ulaya.
Jarida la habari  nchini  Ujerumani, Der Spiegel, limeripoti Shirika la Usalama la Taifa nchini Marekani limekuwa likizitegesha taasisi za Umoja wa Ulaya ili kupata taarifa ya shughuli zake.
Katika ripoti yake iliyochapishwa jana kwenye mtandao, jarida hilo limesema kwamba majasusi wa Marekani walitumia virusi vya kompyuta na kunasa mazungumzo ya simu katika kupata taarifa kutoka taasisi za miji ya Washington, New York na Brussels.
Nyaraka hizo zilitolewa na Edward Snowden, mfanyakazi wa zamani wa Shirika hilo, ambaye katika siku za karibuni amevujisha nyaraka za siri kuhusiana na programu ya kuwafuatilia raia wa Marekani
Martin Schulz sasa amesema iwapo taarifa hizo zitakuwa ni za ukweli zitasababisha taathira kubwa katika uhusiano kati ya Umoja wa Ulaya na Marekani.

VIKOSI VYA SYRIA VYAZIDI KUPAMBANA NA WAASI

Watu watatu wameuwawa nchini Syria baada ya Jeshi la nchi hiyo kufanya mashambulizi ya angani mjini Homs. Kulingana na shirika la kutetea haki za binaadamu nchini humo, vikosi vya serikali bado vinaendelea na juhudi za kudhibiti mikoa ambayo inashikiliwa na waasi.
Mkurugenzi wa shirika hilo Rami Abdel Rahman  amesema watu hao waliouwawa ni mwanamke mmoja na watoto wawili na mamia ya watu wameachwa na majeraha tangu kuanza kwa mashambulizi ya angani kutoka kwa vikosi vya serikali hapo jana. Rami Abdel Rahman amesema jeshi kwa sasa linajaribu kuingia mjini Khaldiyeh lakini bado hawajafanikiwa.
Homs ambao ni mji wa tatu  kwa ukubwa nchini Syria ni miongoni mwa miji ya mwanzo kujiunga na uasi  dhidi ya Rais Bashar Al Assad zaidi ya miaka miwili iliopita.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa watoto 6000 ni miongoni mwa watu 93,000 waliouwawa hadi sasa.

PICHA ZA OBAMA ZACHOMWA MOTO AFRIKA KUSINI

Polisi nchini Afrika Kusini leo wamepambana na waandamanaji waliokuwa na hasira ambao wameteketeza moto picha za Rais Barack Obama wa Marekani ambaye yuko safarini nchini humo.
Waandamanaji hapo pia wameteketeza moto bendera za Marekani katika maandamano yaliyofanyika nje ya Chuo Kikuu cha Johannesburg, tawi la Soweto, sehemu ambayo Obama aliwahutubia wanafunzi.
Waandamanaji wamelaani vikali uungaji mkono wa Marekani kwa utawala haramu wa Israel na vile vile sera za Washington za kutumia ndege zisizo na rubani ambazo zimesababisha vifo vya watu wengi wasio na hatia hasa wanawake na watoto. Aidha wamemkosoa vikali Obama kwa kutotekeleza ahadi yake ya kufunga jela ya kuogofya ya Guantanamo inayosimamiwa na jeshi la Marekani. Wanaharakati walikuwa wamebeba mabango yaliyo kuwa na maandishi kama vile 'Obama acha kuunga mkono utawala wa ubaguzi wa rangi Israel'. Wanaharakati hao wanasema ni unafiki mkubwa kwa Obama kujaribu kujikurubisha kwa Shujaa Nelson Mandela aliyepinga utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika Kusini na wakati huo huo Washington inaendelea kuupa himaya kamili utawala haramu wa Israel unaowabagua Wapalestina.

MAANDAMANO MAKUBWA YAANZA MISRI LEO

Maandamano makubwa yameanza leo nchini Misri ambapo kuna wasi wasi wa kuibuka machafuko baina ya wafuasi na wapinzani wa Rais Mohammad Morsi.
Waandamanaji hasimu walianza kukusanyika Jumamosi usiku kwa ajili ya maandamano yanayofanyika katika kipindi hiki cha kuwadia mwaka mmoja tokea Morsi achaguliwe kuwa rais wa Misri. Watu watatu tayari wamesharipotiwa kupoteza maisha katika machafuko ya Jumamosi katika maeneo kadhaa ya Misri. Wapinzani wameitisha maandamano makubwa katika medani ya Tahrir mjini Cairo kwa lengo la kumtaka Rais Morsi ajiuzulu. Hata hivyo wafuasi wa Harakati ya Ikwanul Muslimin nao wameitisha maandamano yao wakimuunga mkono Rais Morsi. Hali hiyo imeibua wasi wasi wa uwezekano wa kuzuka machafuko na ghasia kote Misri katika maandamano ya leo. Wapinzani wanataka Rais Morsi ajiuzulu na uchaguzi wa mapema kuitishwa. Wanamlaumu kiongozi huyo kuwa amekengeuka mkondo wa mapinduzi yaliyomtimua madarakani dikteta Hosni Mubarak. Uamuzi wa Mursi wa kukata uhusiano na Syria na kuwaunga mkono magaidi nchini humo pia ni jambo ambalo limewakasirisha Wamisri.

OBAMA KUZURU GEREZA ALILOFUNGWA MANDELA

Rais Barack Obama wa Marekani ameendelea na ziara yake nchini Afrika Kusini na hii leo jumapili yeye pamoja na familia yake watatembelea kisiwa vya Robben na kuzuru gereza ambalo Rais wa zamani wa Taifa hilo na kinara wa vita dhidi ya ubaguzi wa rangi Nelson Mandela alitumikia kifungo cha miaka 18 kati ya miaka 27 aliyokaa gerezani.Akiwa nchini humo jana jumamosi kiongozi huyo alikutana na baadhi ya ndugu wa Mzee Mandela wakiwamo watoto na wajukuu zake huku akiahidi kuendelea kuwa karibu na familia hiyo katika kipindi hiki kigumu cha kumuuguza mpendwa wao ambaye bado hali ya ya afya yake imeendelea kuwa tata licha ya kukaa hospitalini kwa zaidi ya majuma matatu sasa.
Aidha Obama aliweka wazi sababu za yeye kutozuru Taifa la Kenya ambalo ni asili ya baba yake mzazi, miongoni mwa sababu zake ni pamoja na machafuko ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 inayomkabili Rais wa Taifa hilo Uhuru Kenyatta pamoja na naibu wake William Rutto katika mahakama ya kimataifa ya ICC. Hata hivyo kiongozi huyo ameahidi kuzuru Taifa hilo kabla ya kukamilika kwa muda wake wa Urais nchini Marekani. Akiwa katika siku ya mwisho ya ziara yake nchini Afrika Kusini Rais Obama anatarajiwa kutoa hotuba ihusuyo sera ya Marekani kwa Afrika katika chuo kikuu cha Cape Town.
Ziara ya Obama nchini Senegal, Afrika Kusini na Tanzania inalenga kubadilisha fikra zilizojengeka kuwa kiongozi huyo amekuwa akijiweka kando na maswala ya Afrika tangu kuanza kuliongoza Taifa tajiri la Marekani mwaka 2008.

Saturday, June 29, 2013

GHASIA ZAUA WAWILI MISRI

Watu wawili wameuwawa na wengine wengi wamejeruhiwa katika mji wa pili kwa ukubwa nchini Misri wa Alexandria kufuatia mapigano kati ya wafuasi na wapinzani wa rais mwenye msimamo wa itikadi kali za Kiislamu Mohammed Mursi.Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imethibitisha kwamba raia wa Marekani mwenye umri wa miaka 21 ni miongoni mwa waliouwawa.Katika mji wa Port Said pia kuna mtu mmoja aliyeuwawa na wengine wengi wakajeruhiwa baada ya kutokea mripuko katika maandamano.Polisi imesema bado haijafahamika ikiwa mripuko huo unahusiana na maandamano hayo.Maelfu ya watu wamekusanyika katika miji mbali mbali kote nchini Misri kushiriki maandamano ya kumpinga Rais Mursi huku ghasia zikiripotiwa pia katika mji mkuu wa nchi hiyo Cairo na katika mkoa wa Aga.Ghasia hizo zinashuhudiwa kabla ya  maandamano makubwa kabisa dhidi ya serikali yaliyopangwa kufanyika kesho Jumapili.Marekani imetowa tahadhari kwa raia wake kutosafiri nchini Misri wakati ikiwataka pia wafanyikazi wote katika ubalozi wake wasiokuwa na kazi za lazima kuondoka nchini humo.

FAMILIA YA MANDELA YAWAKOSOA WANAHABARI

Taarifa kutoka Ikulu ya Afrika Kusini zinasema kuwa hali ya kiafya ya rais mstaafu Nelson Mandela sio nzuri na kuwa imezorota katika saa 48 zilizopita. Baada ya kumtembelea hospitalini, mwanawe mkubwa wa kike Makaziwa, alisema hali inaonekana kuwa mbaya lakini akaongeza kuwa Mandela anaweza kuwasikia jamaa zake wanapomuita huku akijaribu kufungua macho yake. Makaziwe amesema “Nimekasirishwa sana. Kwa sababu Mandela ni kiongozi mashuhuri duniani, haimaanishi utu wake udhalilishwe pamoja na kuvuka mipaka kuingilia mambo yake binafsi Hapa naona kuna ubaguzi wa rangi, huku vyombo vingi vya kimataifa vikivuka mipaka, ni kama ndega aina ya Tai au Vulture wanaosubiri Simba kumla mnyama aliomuwinda kisha wakimbilie mzoga.
Wamevuka mipaka ya maadili. Wakati hayati Margaret Thatcher alipokuwa mgonjwa mbona sikuona, ukaribu wa vyombo vya habari kiasi ninachokiona kwa banangu? Ni kwa sababu hii ni nchi ya kiafrika. wanahisi kuwa hapa wanaweza kuvuka mipaka wanavyotaka, '' alisema Makaziwe Mapema leo, Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma alifutilia mbali ziara yake ya kwenda Musumbiji baada ya kumtembelea hospitalini aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela. Rais Zuma amesema kuwa Bwana Mandela yuko katika hali mbali ya afya. Msemaji wa Zuma Mac Maharaj alisema kuwa hali yake imedorora zaidi
Mandela ambaye, ni rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, amelazwa hospitalini tangu tarehe 8 mwezi Juni akiugua maradhi ya mapafu. Madaktari wanasemekana kufanya kila wawezalo kuhakikisha kuwa Mandela anapona. Vikundi vya watu wenye huzuni mkubwa kuhusu hali ya afya ya Mandela, walikusanyika nje ya hospitali alikolazwa, wakiwa na ujumbe wa ugua pole kwa Mandela.Wadadisi wanasema kuwa wananchi wa Afrika Kusini wanaonekana kuwa tayari kwa habari zozote sasa kuhusu hali ya Mandela.
"tutasikitika sana ikiwa tutapata habari za kifo chake, lakini pia tutakuwa tunasherehekea maisha yake. Amefanya mambo mengi zaidi kwa nchi yetu,'' alisema kijana John Ndlovu, mwenye umri wa miaka 25.
Zuma alitarajiwa kuhudhuria mkutano wa marais nchini Msumbiji, hii leo lakini akaamua kuakhirisha safari yake. Taarifa kutoka kwa ofisi yake ilisema kuwa anaendelea kuwapongeza wananchi wa Afrika Kusini wanaoendelea kuiombea familia ya Madiba. Uamuzi wa Rais Zuma kufutilia mbali ziara yake ambako alitarajiwa kuhudhuria mkutano wa kikanda kuhusu uekezaji anaonyesha wazi kuwa hali ya Mandela inaendelea kuzorota zaidi kulingana na mwandishi wa BBC mjini Johannesburg Mike Wooldridge.

OBAMA AKUTANA NA ZUMA

Rais wa Marekani Barack Obama, amesema uvumilivu na ujasiri wa Nelson Mandela ni mfano mwema kwa dunia na upendo wa dhati wa rais huyo wa zamani wa taifa la Afrika Kusini inaonyesha ni kwa namna gani alivyo na utu wa kibinadamu. Bwana Obama ameongeza kuwa Mandela, alionyesha ukweli na ukakamavu ambao una maana kubwa katika utu wa kibinadamu ambao uliondoa tabaka la ubaguzi, udini na utaifa.
Rais huyo wa marekani ameyazungumza hayo mjini Pretoria baada ya mazungumzo na rais wa sasa wa Afrika kusini, Jacob Zuma.
Ziara hiyo ya bwana Obama ina lengo la kuongeza mauhusiano ya kibiashara lakini imetekwa na hisia za ugonjwa wa bwana Mandela ambaye amelazwa hospitalini kwa muda wiki tatu sasa kutokana na maradhi ya mapafu yanayosumbua mfumo wake wa kupumulia. Katika kikao hicho wawili hao walizungumza na vyombo vya habari kuhusu ushirikiano wa mataifa yao kibiashara mbali na kutafuta suluhu ya kudumu katika mataifa yaliokumbwa na ghasia mashariki ya kati. Ikulu ya White House imesema kuwa Obama pia atakutana na familia ya Mandela anayeugua maambukizi ya mapafu ili kuifariji. Awali Rais Obama, aliye ziarani barani afrika alitoa shukran za dhati kwa uongozi ulioonyeshwa na Mandela. Wakati wa ziara hiyo Obama pia atakutana na wanafunzi huko Soweto kabla ya kuelekea katika jela la Robben Island ambayo Mandela alihudumia kifungo chake cha miaka 27 wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi.

IRAN KUJENGA KITUO KIPYA CHA NYUKLIA

Dakta Fereydun Abbasi Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ina mpango wa kujenga kituo kipya cha nyuklia. Akizungumza na waandishi wa habari wa kigeni katika mji wa Saint Petersburg nchini Russia, Dakta Abbasi ameongeza kuwa, eneo la kujengwa kituo hicho kipya limeshatengwa, na hivi karibuni Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia IAEA utajulishwa juu ya mpango huo. Abbasi ambaye anahudhuria maonyesho ya kimataifa ya Atom - Expo 2013 na kikao cha nishati ya umeme wa nyuklia katika karne ya 21 mjini Saint Petersburg ameongeza kuwa, mikakati ya Iran ilikuwa ni kujenga tanuri la nyuklia lenye uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 1,000 hadi 1,200 huko Bushehr, ambapo moja kati ya miradi hiyo miwili tayari umeshaanza kufanya kazi. Akizungumzia uwezekano wa kubadilishwa siasa za nyuklia za Iran baada ya kuingia madarakani serikali ya Dakta Hassan Ruhani, Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran amesema kuwa, shughuli za nyuklia za Iran zinafanyika kwa malengo ya amani kwa minajili ya kudhamini nishati ya umeme na kuondoa mahitajio kwa wananchi na kwamba hakuna mabadiliko yoyote ya kimsingi yatakayofanyika.

UTAWALA WA ISRAEL WAWAHUDUMIA MAJERUHI TOKA SYRIA

Utawala wa Kizayuni wa Israel unatoa huduma za tiba kwa wapiganaji wa makundi ya waasi nchini Syria. Taarifa zinasema kuwa, mamia  ya waasi hao ambao wamejeruhiwa kwenye mapigano dhidi ya majeshi ya Syria wanahamishiwa kwenye hospitali za Israel kwa minajili ya kupata huduma za tiba. Taarifa hizo zinasema kuwa, tokea mwezi Februari  mwaka huu, madaktari na wafanyakazi wa hospitali za Israel wamepewa amri na makamanada wa jeshi la utawala huo kutoa huduma kwa  majeruhi wanaopelekwa kwenye hospitali za utawala huo ghasibu. Hii ni katika hali ambayo,  uingiliaji wa Marekani, Uingereza, Ufaransa, pamoja na nchi za eneo kama vile Saudi Arabia, Qatar, Uturuki na utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye mgogoro wa Syria, umesababisha mgogoro wa nchi hiyo kushadidi na kuwa tata zaidi.

IRAN NA RUSSIA KUFANYA MAZOEZI YA PAMOJA YA KIJESHI

Kamanda wa ngazi ya juu wa jeshi la majini la Russia amesema kuwa nchi yake na Iran zinachunguza mpango wa kufanya manuva ya pamoja katika bahari ya Caspian katika nusu ya pili ya mwaka huu. Iran na Russia mwaka 2009 zilifanya manuva ya kwanza ya pamoja ya baharini katika bahari ya Caspian iliyojumuisha meli za kivita 30. Katika manuva hayo yanayotarajiwa kufanywa katika nusu ya pili ya mwaka huu, maafisa wa jeshi la majini la Iran watavitembelea baadhi ya vituo vya kijeshi na bandari huko Russia na kufanya mikutano kadhaa na makamanda na viongozi wa ngazi za juu wa Russia. Tarehe 21 mwezi Aprili mwaka huu pia meli za kivita za Russia zilitia nanga katika bandari ya Bandar Abbas baada ya safari ndefu kutoka bahari ya Pacific.  

MKUU WA KITENGO CHA USALAMA AKAMATWA GUINEA

Mkuu wa kitengo cha usalama katika ofisi ya Rais wa Guinea Conakry ametiwa mbaroni kwa tuhuma za kushiriki kwenye mauaji dhidi ya wananchi wa nchi hiyo. Jean Claude alifikishwa mahakamani hapo jana kujibu shitaka la kushiriki kwenye mauaji ya wananchi wa nchi hiyo Septemba 28 mwaka 2009. Afisa mwandamizi kutoka shirikisho la kimataifa la mashirika ya haki za binadamu ameelezea kufurahishwa kwake na hatua ya kumtia mbaroni na kumfungulia mashtaka Jean Claude. Amesema kuwa hatua hiyo inaonyesha jinsi Guinea ilivyopiga hatua kuleta haki na usawa nchini humo. Inafaa kuashiria hapa kuwa, tarehe 28 Septemba 2009, maelfu ya wapinzani wa serikali ya Guinea walikusanyika katika uwanja mjini Conakry kupinga hatua ya Mousa Dadis Camara ambaye alikuwa Mkuu wa Baraza la Kijeshi linalotawala nchini humo kutaka kushiriki kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi wa rais mwaka 2010. Vikosi vya usalama vya nchi hiyo viliingia uwanjani hapo na kuwapiga, kuwafyatulia risasi na hata kuwabaka wanawake waliokuwepo uwanjani hapo. Machafuko hayo yalisababisha watu wasiopungua 157 kuuawa na wanawake zaidi ya 100 kubakwa na vikosi vya usalama vya nchini humo. 

WAFUASI WA MURSI WAANDAMANA KUMUUNGA MKONO

Makundi ya Kiislam nchini Misri yametowa wito kwa wafuasi wao kushiriki katika maandamao yasiokuwa na kikomo kuanzia leo Ijumaa, kumuunga mkono rais wa taifa hilo Mohamed Morsi, ikiwa ni siku mbili ya upinzani kukusanyika kuandamana wakimtaka rais huyo kujiuzulu baada ya kile wanachosema ameshindwa kuboresha maisha ya wananchi na kufikia malengo ya mapinduzi ya mwaka 2011 yaliomg'oa rais Hosni Mubarak Madarakani. Wafuasi wa rais Morsi wanaandamana leo siku ya Ijumaa, katika maandamano yatayo endelea na haijulikani itavyokuwa katika siku mbili zijazo kufuati upinzani nao kupanga kuandamana Juni 30. Jeshi la usalama nchini humo limeimarisha usalama jijini Cairo na miji mingine nchini humo kukabiliana na ghasia ambazo zaweza kuibuka.
Wapinzani nchini Misri wanasema wamechoka na uongozi wa rais Morsi na wanamtaka ajiuzulu baada ya mwaka mmoja wa kuwa uongozini huku wafuasi wa Morsi wakisema hawawezi kuruhusu kiongozi wao kutishwa na watu wachache. Siku ya Jumatano, maandamano yalifanyika mjini Mansoura na kusababisha vifo vya watu wawili na wengine zaidi ya mia moja kujeruhiwa. Wachambuzi wa Siasa wanasema tatizo kubwa linalochangia hali kuendelea kuwa mbaya nchini humo ni kwa sababu ya katiba ambayo imeegemea mno dini ya Kislamu.
Siku ya Jumatano rais Morsi aliadhimisha sherehe za mwaka mmoja tangu kuchukua hatamu ya uongozi nchini humo baada ya kuanguka kwa utawala wa Hosni Mubarak mwaka 2011. Rais Morsi amewaonya wananchi wa taifa hilo kuacha kuegemea mirengo ya kisiasa ili kuepuka nchi hiyo kugawanyika. Mwendelezo wa maandamano nchini humo unaelezwa na wachambuzi wa kiuchumi kuwa huenda pia ukachangia kuporomoka kwa uchumi nchini humo.

RAIS WA ECUADOR ATANGAZA KUFUTA MKATABA NA MAREKANI

Wakati Marekani ikiendesha vitisho na madhara kwa taifa litalo mpa hifadhi ya kisiasa mshauri wa zamani wa Kituo cha Usalama cha Marekani NSA, na mfanyakazi wa shirika la Ujasusi la Marekani Edward Snowden, Rais wa Ecuador Rafael Correa atangaza kusitisha mkataba wa mapendekezo ya ushuru uliotolewa na Marekani ikiwa ni sehemu ya mapambano dhidi ya biashara ya madawa ya kulevya. Rafael Correa ameiambia Marekani kwamba hawataki vitisho, na ndio sababu wameamuwa kufuta viwango vya ushuru vilivyo pendekezwa kwa upande wao na hawawezi kubadili hatuwa hii, hivyo kuiomba Marekani ibaki na mapendekezo yake.
Kiongozi huyo wa mrengo wa kisocialist aliechaguliwa februari iliopita kwa muhula wa miaka mitano amekuwa na uhusiano mbovu na Marekani. Makubaliano ya forodha baiba ya taifa hilo na Marekani yalianza kutumika mwaka 1991. Yalirahisisha mauzo ya mafuta Ekuador, maua, matunda kwenda kuuzwa nchini Marekani, ikiwa ni kiwango cha takriban dola za Marekani Milioni ishirini na tatu kwa mwaka. Tangu kuvijisha siri za Marekani kuwa imekuwa kwa muda mrefu ikiendesha uchunguzi wa mawasiliano ya ki elektroniki kwa mataifa mbalimbali duniani, Edward Snowden anatafutwa na serikali ya Marekani kwa kile kinacho daiwa na serikali hiyo kwamba ni uhaini.
Snowden amekwama kwenye uwanja wa ndege wa jijini Moscou akisubiri kupewa hifadhi na serikali ya Ecuador. Marekani imekuwa ikiomba Urusi kumsafirisha afisaa huyo nchini Marekani kwa ajili ya kuhojiwa na vyombo vya sheria, jambo ambalo Urusi imekuwa ikikanusha kuwepo katika ardhi yake na kuweka wazi kwamba amekwama kwenye eneo la Uwanja wa Ndege.

UFUJAJI WA MISAADA BARANI AFRIKA

Kamati ya Bunge la Uingereza limepokea taarifa kuwa zaidi ya dola milioni 650 pesa za msaada zilizotolewa na mataifa ya Ulaya kwa bara la Afrika zimetumiwa vibaya. Kamati ya bunge la malodi kuhusu maswala ya nje, inachunguza ambavyo dola bilioni 1.3 zilizotolewa kama msaada kwa miradi ya maji kusini mwa jangwa la Sahara miaka kumi iliyopita, zilivyotumiwa. Kamati hiyo iliarifiwa kuwa chini ya nusu ya miradi 23 iliyochunguzwa ilikuwa duni na wala haikutimiza mahitaji ya wananchi.
Matatizo yalitokana na mipango duni na hata wakati wa kuitekeleza miradi mipango haikuwa sawa. Mkaguzi mmoja wa matumizi ya pesa aliambia kamati hiyo kuwa utafiti wake ulionyesha wazi hali ya miradi mingine ambayo ilifanywa na Muungano wa Ulaya katika mwongo mmoja uliopita. Miradi ya maji hujumuisha utoaji wa huduma za maji safi, ujenzi wa vyoo hatua ambazo zinazuia kulipuka kwa magonjwa. Wakaguzi pia waligundua kuwa vifaa vilivyonunuliwa na mameneja wa miradi kama paipu vilikuwa vinahitajika. Matatizo yanatokana na ikiwa miradi hiyo inaweza kudumu au la.
Katika visa vingine, idadi ya wenyeji wanaopokea mafunzo ni ndogo sana kwa hivyo baada ya miradi kutekelezwa haiwezi kudumu. Lakini tatizo kubwa zaidi lilikuwa ufadhili au kuwepo mikataba ya kudumu kutoka kwa kamati na serikali za nchi maskini kuhusu namna ya kufadhili mfano hiyo miradi ya maji. Mwandishi wa BBC wa maswala ya ustawi Mark Doyle anasema kuwa ikiwa mikataba haiwezi kuwekwa basi itakuwa vigumu kwa matumizi mazuri ya pesa na pia kuna hatari ya pesa za maendeo kuendelea kufujwa.

MAREKANI YAWAONYA RAIA WAKE WALIO MISRI

Serikali ya Marekani imetoa tahadhari kwa raia wake kutosafiri nchini Misri huku ikiwataka maafisa ambao hawajaajiriwa katika ubalozi wake nchini humo kuondoka mara moja kutokana na ghasia zinazoendelea . Baadhi ya raia wamefariki huku wengine wengi wakijeruhiwa vibaya kufuatia makabiliano kati ya wafuasi wa rais Mohammed Morsi na wale wa upinzani wakati ambapo rais huyo anatarajiwa kuadhimisha mwaka mmoja tangu achukue hatamu.
Maafisa nchini Misri wanasema kuwa kati ya waliouawa ni raia wa marekani mjini Alexandria. Tayari wananchi wa taifa hilo wameanza kununua chakula na mafuta kwa wingi ili kukihifadhi kwa hofu kwamba ghasia hizo huenda zikaenea. Wapinzani wa rais Morsi wanadai kuwa ameshindwa kutatua maswala nyeti nchini humo huku wafuasi wake wakisisitiza kuwa ni sharti apewe mda.

Friday, June 28, 2013

ZUMA AFUTA ZIARA ZAKE KUFATIA KUUMWA KWA MANDELA

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma amefuta safari yake katika nchi za nje ili kubaki nchini mwake wakati huu kinara wa ubaguzi wa rangi Nelson Mandela akiwa katika hali mahtuti jijini Pretoria, ambapo ametowa wito kwa wananchi kuendelea kumuombea. Hii ni mara ya kwanza rais wa taifa hilo anapangua ratiba tangu kulazwa hospitalini kwa kinara mtetezi wa ubaguzi wa rangi. Usiku mzima watu walijitokeza kwa wingi na mishumaa katika Hospitali ya Mediclinic Heart Hospital ambako amelazwa kinara huyo, ishara ya upendo dhidi ya kinara huyo.
Mandela ambaye tangu siku ya Jumapili hali yake imekuwa mbaya mno, kwa sasa anapumua kwa nguvu za machine, ambapo kiongozi wa jadi wa ukoo wa Mandela, Napilisi Mandela ambaye alikuwa kumuona jana, amethibtisha na kusema kwamba ni kweli anatumia machine kwa kupumua, inatia huruma sana lakini hawana njia nyingine ya kufanya. Rais Zuma upande wake alijizuia kuzungumzia lolote kuhusu taarifa hii baada ya kupewa maelezo na ma daktari wanaomshughulikia rais Mandela wakati alipo tembelea Hospitalini jana saa nne usiku majira ya Afrika kusini, na Afrika ya kati, ikiwa ni saa tano usiku majira ya Afrika Mashariki.
Katika taarifa iliotolewa na rais Zuma, alifahamisha tu kwamba Nelson Mandela bado yupo katika hali ngumu na kutangaza kufuta ziara yake iliotarajiwa kufanyika mapema leo asubuhi nchini Msumbuji. Rais Zuma alipewa taarifa ya hali inayoendelea na madaktari wanaofanya kila jitihada kuhakikisha hali inaboreka zaidi.
Msemaji wake Mac Maharaj amezungumza kupitia kituo cha televisheni ya taifa hilo SABC kuwa kwa saa 48 zilizopita hali ya afya ya rais Mandela imekuwa mbaya zaidi, na hivo kusababisha rais Zuma kuahirisha safari yake nchini Msumbuji. Muda mchache kabla ya hapo Rais Zuma akiwa mbele ya watetezi wa vyama vya wafanyakazi alisema kuwa na matumaini ya kusherehekea miaka 95 ya Mandela Julai 18 huku akiomba watu kuendelea kumuweka yeye na familia yake katika mawazo yetu na sala za kila dakika. 

EQUADOR YAAHIDI KUMPA UHURU SNOWDEN

Serikali ya Ecuador imempa pasi ya kusafiria afisaa wa zamani wa CIA Edward Snowden anaye tafutwa na serikali ya Marekani ambaye amekwama katika eneo la uwanja wa ndege wa Moscou ikiwa ni siku ya tano kwenye uwanja wa ndege wa Cheremetievo jijini Moscou akitokea Hong Kong Jumapili juma lililopita. Serikali ya Marekani ili sitisha kibali cha usafiri cha afisaa huyo wa zamani wa idara ya ujasusi nchini humo CIA na kudai kurejeshwa nyumbani kwa ajili ya kukabiliana na vyombo vya sheria kwa kosa la kuvujisha siri za taifa hilo kwenye nyanja ya ki elektroniki ambapi alisema Marekani imekuwa ikifanya uchunguzi wa mawasiliano ya ki elektroniki. Jambo ambalo lilizua tafrani kubwa.
Ubalozi mdogo wa Ecuador jijini London umetowa kibali cha usafiri kwa afisaa huyo wa zamani kitacho mrahisishia safari yake kuelekea nchini Ecuador ambako aliomba hifadhi ya kisiasa. Ubalozi huyo mdogo jijini London umezitaka nchi husika kumrahisishia afaisaa huyo na safari yake kuelekea katika nchi aliyo omba hifadhi. Kibali hicho chenye ukurasa mmoja chenye nembo ya Ecuador kimeaandika jina la Snwden, tarehe na mahali alipo zaliwa, rangi ya nywele zake na macho yake, urefu na hali ya familia na kutiwa sahihi na Fidel Narvaez Narvaez balozi mdogo wa Ecuador jijini London.
Hapo jana Ecuador ilikanisha taarifa za kutowa kibali cha usafiri kwa Edward Snowden afisaa wa samani wa idra ya ujasusi ya Marekani na kuweka ngumu kwenye ombi la ofisa huyo la kuomba hifadhi, na kutaja kuwa swala lake linaweza kuchukuwa siku au myezi. Ubalozi wa Ecuador jijini London ulimpa hifadhi pia Julian Assange, muasisi wa mtandao wa Wikileaks uliochapisha taarifa za siri mwaka 2010, kumlinda asisafirishwe kuelekea nchini Sweden ambako anakabiliwa na mashtaka ya ubakaji.

MORSI AONYA DHIDI YA MAANDAMANO

Rais wa Misri Mohammed Morsi ameonya kuwa vurugu za siasa zinaathiri demokrasia nchini humo. Katika hotuba ya taifa kupitia televisheni kuadhimisha mwaka mmoja tangu achukue uongozi, Bw Morsi alikiri kuwa amefanya makosa kadhaa. Kadhalika aliutaka upinzani kuwasilisha matakwa yake kupitia kura. Hata hivyo uongozi wake umekumbwa na changamoto si haba ambapo Misri imeshuhudia maandamano ya kila mara kati ya wafuasi na wapinzani wa Morsi.
Morsi pia amewonya wale wanaonekana kama wenye njama ya kutaabisha utawala wake na kujairbu kumwendea kichinichini pamoja na kusumbua demokrasia nchini humo. Wanajeshi wamepelekwa katika miji mikubwa kote nchini kabla ya kufanyika kwa maandamano yanayopangwa dhidi ya utawala wake mwishoni mwa wiki hii. Hotuba ya bwana Morsi imetolewa wakati makabiliano yakitokea Kaskazini mwa mji wa Mansoura.
Watu wawili waliuawa na wengine 170 kujeruhiwa kwenye mapigano kati ya wafuasi na wapinzani wa serikali, kwa mujibu wa afisaa wa afya. Morsi anayeongoza chama tawala cha Muslim Brotherhood, alikuwa rais wa kwanza wa taifa hilo kwa chama cha kiisilamu babada ya kushinda uchaguzi mwezi Juni mwaka jana. Uchaguzi huo ulisifiwa na wengi kuwa huru na wa haki. Mwaka wake wa kwanza mamlakani umekumbwa na maandamano ambayo hayaishi pamoja na uchumi unaodorora.

WANNAJESHI WANAILONDA MPAKA KATI YA SYRIA NA ISRAEL WAONGEZEWA MUDA

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeongeza muda wa miezi sita kwa majeshi ya kulinda amani ya  Umoja wa Mataifa katika eneo la Golan katika mpaka wa Israel na Syria. Jeshi hilo la kulinda amani sasa litamaliza muda wake mwisho wa mwaka huu  na litaongezeka kutoka wanajeshi 900 hadi 1,250.
Eneo la Golan limekuwa uwanja wa mapambano kati ya wanajeshi wa serikali ya rais Bashar Al Assad na waasi katika mgogoro unaoendela kwa mwaka wa pili sasa. Mark Lyall Grant Balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa amesema wanajeshi hao pia watapewa silaha nzito za kujilinda dhidi ya uvamizi kutoka kwa wanajeshi wa Syria au waasi. Majeshi ya kulinda amani yalitumwa katika eneo mapema miaka ya tisini baada ya baada ya kumalizika kwa vita kati ya Isreal na Syria kuhakikisha amani inadumu katika mpaka wa mataifa hayo mawili.
Kwingineko nchini Syria, Mashirika ya Kimataifa ya kutetea haki za binadamu yanasema kuwa miili ya watu 16 ya watu walioteswa na majeshi ya serikali imewasilishwa kwa jamaa zao siku ya Ijumaa. Mashirika hayo yanasema kuwa maelfu ya watu bado wanazuiliwa na kuteswa na jeshi la rais Bashar Assad baada ya kukamatwa katika maandamano ya kuiangusha serikali ya Assad. Takwimu za hivi karibu kutoka kwa umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa zaidi ya watu laki moja wameuliwa nchini Syria katika mapigano kati ya wapinzani na wanajeshi wa serikali kipindi hiki ambacho mataifa ya Magharibi yakipanga kuwapa silaha waasi huku serikali nayo ikipata usaidizi kutoka kwa Iran na kundi la Hezbollah kutoka Lebanon.

RAIA WAKESHA KUMUOMBEA MANDELA

Raia wa Afrika Kusini wakesha usiku kucha wakimuombea rais wa zamani wa nchi hiyo Nelson Mandela kinara wa zamani nje ya hospitali anakoendelea kupata matibabu mjini Pretoria. Mbali na maombi, raia hao wamekuwa wakiimba nje ya makaazi ya zamani ya kiongozi huyo wa zamani mtaani Soweto. Siku ya Alhamisi rais Jacob Zuma alisema kuwa afya ya Mandela ilionekana kuimarika lakini bado yuko katika hali mbaya.
Binti ya Mandela Makaziwe Mandela amesisitiza  kuwa licha ya baba yake kuwa katika hali mbaya, bado wana imani atapata nafuu na kuondoka hospitalini. Hata hivyo, Makaziwe amevishtumu vyombo vya habari vya kimataifa kuwapotosha watu duniani na halikadhalika kutoipa familia nafasi ya kuwa binafsi. Mbali na hayo rais wa Marekani Barrack Obama anatarajiwa kuwasili nchini humo hivi leo akitokea nchini Senegal ambako yupo kwenye ziara barani Afrika.
Jana rais Obama alikutana na Majaji wakuu wa Mahakama za juu barani Afrika jijini Dakar nchini Senegal na kujadiliana kuhusu haki barani Afrika. Aidha, Obama aliisifu nchi ya Senegal kama mojawapo ya nchi barani Afrika inayoimarika kidemokrasia na kufanya mabadiliko katika taasisi zake. Obama anatarajiwa kukutana na rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma pamoja na wafanyibiashara na viongozi wa vijana wakati huu rais wa kwanza mweusi wa taifa hilo Nelson Mandela akiendelea kupata matibabu hospitalini. Baada ya kuondoka Afrika Kusini Obama anatarajiwa kuzuru Tanzania siku ya Jumatatau juma lijalo.

RAIS WA SENEGAL APINGANA NA OBAMA KUHUSU USHOGA NA HAKI ZAO

Rais Macky Sall wa Senegal amesema nchi yake haiko tayari kuruhusu ushoga na maingiliano ya ngono kati ya watu wenye jinsia moja. Sall aliyasema hayo jana akijibu matamshi ya mgeni wake Rais Barack Obama wa Marekani aliyezitaka nchi za Kiafrika ziwape mashoga alichokiita haki sawa na makundi mengine ya kijamii. Rais Macky Sall amemjibu Obama akisema: Japo Senegal imeonyesha ustahamilivu mkubwa lakini haiko tayari kuruhusu maingiliano ya ngono kati ya watu wenye jinsia moja.
Obama alikuwa amezitaka nchi za Afrika kuwapa mabaradhuli haki sawa na makundi mengine ya kijamii bila ya kujali mbari, dini na jinsia zao.
Nchi nyingi za Afrika zinatambua maingiliano ya kingono kati ya watu wenye jinsia moja kuwa ni kosa la jinai.
katika miaka ya hivi karibuni nchi kama Burundi na Sudan Kusini zimepasisha sheria zinaotambua maingiliano kama hayo kuwa ni kosa la jinai na nchi kama Uganda, Nigeria na Liberia zinafanya mikakati ya kupasisha sheria zinazozidisha adhabu kwa wale wanaofanya vitendo hivyo vichafu.

WAZIRI WA ULINZI LIBYA AFUTWA KAZI

Waziri Mkuu wa Libya Ali Zeidan amemtimua kazi Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo Mohammed al Barghathi baada ya kutokea mapigano makali mjini Tipoli baina ya makundi mawili yenye silaha ambayo yamesababisha vifo vya watu watano na kujeruhi makumi ya wengine.
Ali Zeidan amesema baada ya yaliyojiri jana imeamuliwa kwamba Waziri wa Ulinzi ataachichwa kazi. Tutatanganza waziri mpya wa ulinzi hivi karibuni, amesisitiza Waziri Mkuu wa Libya.
Uamuzi huo wa kumfuta kazi Waziri wa Ulinzi wa Libya umechukuliwa huku nchi hiyo ikusumbuliwa na mapigano ya mara kwa mara kati ya makundi ya wanamgambo wanaobeba silaha.
Jumatano iliyopita watu wengine 5 waliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika mapigano makali yaliyotokea baina ya makundi hasimu kwenye wilaya ya Salahuddin. Mji wa pili kwa ukubwa nchini Libya wa Benghazi pia umekumbwa na machafuko makubwa ambapo vituo kadhaa vya polisi vimelipuliwa kwa mabomu.

KERRY ALAUMU MIPANGO YA UTAWALA WA ISRAEL

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry amesema utawala haramu wa Israel unavuka mipaka kwa kuidhinisha ujenzi wa vitongoji vipya vya walowezi wa Kizayuni.
Kerry alisema hayo baada ya kukutana na Waziri mkuu wa utawala huo ghasibu, Benjamin Netanyahu hapo jana. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amesema Tel Aviv inafuata mkondo mbaya ambao unaendelea kuzima matumaini ya kupatikana amani Mashariki ya Kati. Amesema kwamba, kwa hali ilivyo hivi sasa, uwezekano wa kuwa na mataifa mawili kama njia ya kutatua mgogoro wa Israel na Palestina unaendelea kufifia na kwamba itafika sehemu ambapo itakuwa vigumu kabisa kwa amani ya Mashariki kupatikana.
Hii ni katika hali ambayo, Umoja wa Mataifa umesisitiza mara kadhaa kwamba ujenzi wa vitongoji vya Wazayuni katika ardhi za Wapalestina ni kinyume cha sheria za kimataifa.

OBAMA KUKARIBISHWA NA MAANDAMANO YA WANANCHI KUMPINGA

Huku Rais Barack Obama wa Marekani akiwa amewasili nchini Senegal hii leo katika duru yake ya kwanza ya safari barani Afrika, safari yake hiyo inakabiliwa na upinzani mkubwa huko Afrika Kusini ambayo itakuwa nchi ya pili kuitembelea kabla ya kuelekea Tanzania.
Duru zinaarifu kuwa idadi kubwa ya mashirika ya wafanyakazi, wanafunzi wa vyuo vikuu, mawakili na watetezi wa haki za binaadamu wanapinga vikali safari ya Rais Obama nchini humo. Muungano wa Jumuiya za Wafanya Kazi Afrika Kusini COSATU umewataka wafanyakazi nchini humo kufanya maandamano ya kupinga safari hiyo. Katibu wa masuala ya kimataifa wa COSATU, Bongani Masuku amesema kuwa, siasa za Marekani zimejikita zaidi katika kuzalisha na kukithirisha silaha za nyuklia na kusambaza silaha ulimwenguni, jambo ambalo linavuruga amani, uadilifu, demokrasia na haki za binadamu.
Jumuiya ya Mawakili wa Kiislamu nchini Afrika Kusini imetaka Rais Barack Obama wa Marekani atiwe mbaroni kwa kutenda jinai za kivita. Jumuiya hiyo ya mawakili imetaka Obama afikishwe kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, (ICC) huko, The Hague, Uholanzi. Makundi ya kisiasa nchini Afrika Kusini yameitaja Marekani kuwa mporaji wa maliasili na utajiri wa nchi za Kiafrika.

MIGOGORO YA WAISLAM YAWANUFAISHA WAISRAEL NA MAREKANI

Waziri wa Ulinzi wa Iran Brigedia Jenerali Ahmad Vahidi ameonya kuwa Marekani na Utawala haramu wa Israel ndio zinazonufaika na migongano ya kimadhehebu miongoni mwa Waislamu.
Vahidi amelaani mauaji ya hivi karibuni ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Misri ambao waliuawa na Mawahabi wanaowakufurisha Waislamu. Vahidi amesema Mawahabi wanaowaua Mashia wanafanya hivyo kwa uchochezi wa Marekani na Israel na kuongeza kuwa, wale wote wanaojali maslahi ya Umma wa Kiislamu wamelaani kitendo hicho cha kinyama. Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema Mashia na Masuni ni ‘mbawa mbili za Uislamu. Ametoa wito kwa Waislamu wanaofuata madhehebu ya Shia na Suni kuungana na kutowaruhusu maadui kuwagawa.
Aghalabu ya wanazuoni wa Kiislamu akiwemo Mkuu wa Chuo Kikuu cha Al Azhar wamelaani vikali ukatili huo wa makundi ya wakufurishaji. Inafaa kuashiria hapa kuwa Mawahabi wakufurishaji wanaamini kuwa tafsiri yao ya Uislamu ndio sahihi na kwamba eti Waislamu wengine wote ni makafiri. Kwa karne nyingi sasa Waislamu wa madhehebu zote wamekuwa wakiishi kwa amani na maelewano nchini Misri na kote duniani.

WAPINZANI MISRI KUFANYA MAANDAMANO JUNI 30

Muungano wa wapinzani unaojulikana kwa jina la Kambi ya Wokozi wa Kitaifa nchini Misri umekosoa vikali hotuba ya Rais Muhammad Morsi wa nchi hiyo, aliyoitoa jana kwa mnasaba wa sherehe za kukumbuka mwaka mmoja tangu alipoingia madarakani. Wapinzani hao wamesisitiza juu ya kufanyika maandamano makubwa tarehe 30 mwezi huu dhidi ya rais huyo. Mbali na mrengo huo kusisitizia kufanya maandamano hayo ya siku ya Jumapili ijayo, pia umetaka kufanyika uchaguzi wa rais wa kabla ya wakati wake. Msemaji wa kambi hiyo Bwana Khalid Daud amekosoa tuhuma zilizotolewa na Rais Morsi na kusema kuwa hazina ushahidi wowote na kuongeza kuwa, ombi la rais huyo kwa mahakama ya katiba na kuitaka kufanya uchunguzi wa haraka wa sheria za uchaguzi wa bunge, kwa hakika ni uingiliaji wa wazi wa kiongozi huyo katika mambo ya mahakama. Daud ameongeza kuwa, viongozi wa kambi hiyo nao watashiriki katika maandamano ya tarehe 30 mwezi huu. Wakati huo huo jumuiya ya Waislamu wa madhehebu ya Kishia nchini Misri, imelaani vikali mauaji ya kikatili yaliyofanywa na Masalafi wenye misimamo mikali dhidi ya mwanazuoni maarufu wa Kishia Sheikh Hassan Shehata na wafuasi wake wengine wanne nchini Misri. Viongozi wa jumuiya hiyo waliyasema hayo hapo jana mjini Cairo mbele ya waandishi wa habari na kusema kuwa serikali iliyoshindwa kuwalinda raia wake hususan wafuasi wa madhehebu ya Kishia. Hii ni katika hali ambayo, kiongozi mmoja wa Kisalafi ametangaza hivi karibuni kuwa, mauaji hayo dhidi ya Waislamu hayo wa Kishia yalifanywa kwa idhini ya Rais Muhammad Morsi mwenyewe.

OBAMA AWASILI SENEGAL

Rais Barack Obama wa Marekani ambaye ameanza safari yake ya kulitembelea bara la Afrika leo amekutana na mwenzake wa Senegal Macky Sall. Katika mazungumzo hayo Obama amesifia hatua alizozitaja kuwa za kushangaza za kuimarisha demokrasia zilizopigwa na nchi za bara la Afrika. Ameongeza kuwa, Senegal ni moja ya waitifaki wenye nguvu zaidi wa Marekani barani humo na kwamba nchi hiyo inaelekea kuwa mfano mzuri wa utawala bora. Hii ni safari ya 3 ya Obama barani Afrika ambako atazitembelea pia nchi za Afrika Kusini na Tanzania. Obama amesema kuwa, ijapokuwa hali ya Mandela si nzuri lakini hatovunja safari yake ya Afrika Kusini na kuongeza kwamba lolote lile litakalotokea Mandela ataendelea kukumbukwa kama shujaa kutokana na mema aliyoyafanya. Katika ziara yake hiyo nchini Senegal pamoja na mambo mengine Obama na mkewe wanatarajiwa kutembelea kisiwa cha Goree, ambacho kilikuwa kituo cha kusafirishia watumbwa katika pwani ya mji mkuu Dakar.  

MAREKANI YAONYA KUTOKEA MASHAMBULIZI ZAIDI AFGHANISTAN

Marekani imeonya juu ya kutokea kwa mashambulizi zaidi ya wanamgambo wa kundi la taliban, licha kuanzishwa kwa mchakato wa amani tangu kufunguliwa kwa ofisi za kundi hilo nchini Qatar. Wanamgamba hao wa Taliban walishambulia hivi majuzi ofisi ya rais na ile ya shirika la ujasusi la Marekani CIA jijini Kaboul na kuwauwa walinzi watatu shambuli ambalo liliashiria uzaifu wa mchakato wa amani juma moja baada ya kuzunduliwa kwa ofisi za Talibans jijini Doha.
Shambulio hilo lilioendeshwa na wapiganaji watano waliovalia nguo za wanajeshi wa Kikosi cha kujihami cha majeshi ya nchi za magharibi nchini Afghanistan Nato, ni shambulio kubwa kuwahi kufanywa na wapiganaji hao tangu mwaka 2008 wakati wa jaribio la kutaka kumuuwa rais wa nchi hiyo Hamid Karzai. Mjumbe maalum wa Marekani nchini Afghanistan na Pakistan, James Dobbins amesema katika mkutano na vyombo vya habari jijini New Delhi, huenda wapiganaji wa Taliban wakaonyesha nia ya kuzungumza huku wakionyesha kwamba wako na nguvu. Dobblins amesema kuwa wanamgambo wa Talibans wanataka kuendeleza shinikizoili ionekana kwamba Marekani wameondoka nchini Afghanistan kufuatia shinikozo kutoka kwao.
Dobbins anazuru nchini India siku kadhaa baada ya ziara ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani nchini humo John Kerry, na kuweka wazi kwamba wamezungumza na viongozi wa Hew Delhi kuhusu kusua sua kwa mchakato wa mazungumzo ya amani nchini Afghanistan hali ambayo inazua hofu kwa viongozi wa India. Kiongozi huyo amesema viongozi wa India wanahofu, hofu ambayo watu wote wanayo, kwakuwa hakuna anaye juwa kitachotokea. Serikali ya New Delhi inahofia kurejea tena kwa utawala wa Talibans Kaboul baada ya kundoka kwa vikosi vya Nato mwaka 2014, na ambayo ilitowa dola za Marekani Bilioni mbili kama msaada kwa Afghanistan ili kukabiliana na ushawishi wa Pakistan katika kuwafadhili watu wenye msimamo mkali.

OBAMA HAJAZUNGUMZA NA CHINA WALA URUSI

Aliyekuwa mfanyakazi wa Shirika la Ujasusi la Marekani Edward Snowden hawezi kuondoka katika eneo alilojificha la uwanja wa ndege wa Moscow ili kusafiri kuelekea mahali kwingine kwa sababu stakabadhi zake sio halali. Chanzo cha habari kimeliambia shirika la habari la Urusi kuwa Snowden hatasafiri kuelekea Cuba au kwingineko kwa sababu hana vibali. Rais wa Marekani, Barack Obama, amesema leo kuwa hajazungumza na Rais wa China, Xi Jinping, au Rais wa Urusi, Vladmir Putin, kuhusiana na ombi la Marekani kuzitaka nchi hizo kusaidia kumrudisha nyumbani Marekani Snowden, kwa sababu hastahili kufanya hivyo. Akizungumza katika kikao cha waandishi habari nchini Senegal ambako ameanzia ziara yake ya mataifa matatu barani Afrika, Obama amesema njia za kawaida za kisheria zinatosha kutumika kuhusiana na ombi hilo la serikali ya Marekani. Amesema wana ushirikiano mkubwa na China na Marekani kuhusiana na masuala mengi na hivyo basi hawawezi kuangazia kisa cha mshukiwa mmoja tu ambaye wanajaribu kumsaka.

Thursday, June 27, 2013

KERO ZA UHARAMIA AFRIKA MAGHARIBI

Viongozi wa kanda ya Afrika Magharibi, wametoa wito wa kupelekwa kwa kikosi cha kimataifa cha jeshi la wanamaji kukabiliana na tishio la uharamia katika ghuba ya Guinea. Uharamia katika eneo hilo unahitaji kukabiliwa kwa ''mkono mkali wa kisheria ,'' alisema rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara kwenye mkutano wa viongozi wa kikanda. Wakati huu kuna mashambulizi zaidi yanayofanywa na maharamia katika ghuba ya kanda ya Afrika Magharibi kuliko kwenye fuo za Somalia. Taarifa hii ni kwa mujibu wa shirika la kimataifa la mabaharia. Ushikaji doria unaofanywa na wanajeshi wa kimataifa umepunguza visa vya uharamia. Takriban mabaharia 960, walishambuliwa Afrika Magharibi mwaka 2012 pekee ikilinganishwa na 851 waliokamatwa katika pwani ya Somalia. Hii ni mara ya kwanza kwa visa zaidi vya mashambulizi yanayofanywa na maharamia kuripotiwa katika fuo za Guinea kuliko hapo awali. Eneo linalokabiliwa na tisho zaidi ambako uharamia unatendwa Afrika Magharibi ni katika pwani ya Nigeria, nchi inayozalisha viwango vikubwa zaidi vya mafuta ghafi barani Afrika . Akihutubia mkutano wa viongozi wa Afrika Magharibi na Kati, mjini Yaounde, bwana Ouattara alitoa kauli hii,: "naitaka jamii ya kimataifa, kuweka sheria kudhibiti uharamia katika Ghuba ya Guinea kama walivyokuwa wakali kuhusu uharamia katika pwani ya Somalia, ambako uwepo wa wanajeshi wa kimataifa kumesaidia katika kupunguza visa vya uharamia.'' Naye rais wa Cameroon,Paul Biya, alisema kuwa ni muhimu kuchukua hatua kulinda, meli na mabaharia pamoja na maslahi ya kiuchumi katika kanda hiyo.
Maharamia katika kanda ya Afrika Magharibi, zaidi huiba mafuta pamoja na mali za wasafiri huku wakitumia mabavu kufanya vitendo vyao. Watano kati ya mahabaria 206 waliotekwa nyara mwaka jana , waliuawa katika ghuba ya Guinea. Hata hivyo ikilinganishwa na ambavyo maharamia wa kisomali huendesha shughuli zao, wao huwazuilia maharamia hadi wanapolipwa kikombozi ndio wanawaachilia.

MURSI KUHUTUBIA TAIFA

Rais wa Misri, Mohammed Mursi, anajiandaa kulihutubia taifa kupitia televisheni hii leo. Hotuba ya rais huyo inatazamiwa kutowa mwelekeo wa hatma yake kisiasa wakati mamilioni ya watu wa nchi hiyo wakijiandaa mwishoni mwa wiki hii kwa maandamano ya kumtaka aondoke madarakani. Inaarifiwa kwamba hofu za kuzuka vurugu kati ya wafuasi wa rais huyo na wapinzani wao kutoka vyama mbalimbali walioungana imewafanya wakaazi kununua vyakula na mafuta kwa wingi kuepuka adha itakayosababishwa na vurugu hizo. Jeshi pamoja na polisi wanajiandaa kukabiliana na hali yoyote ya vurugu itakayojitokeza. Tayari polisi imeongeza vifaa na askari katika maeneo kadhaa ya majengo muhimu ya serikali. Hotuba ya Mursi haijafahamika itazungumzia kitu gani lakini wasaidizi wake wameitaja hotuba hiyo kuwa muhimu kabisa. Baadhi wanahisi huenda akafanya mageuzi makubwa katika baraza lake la mawaziri ili kujaribu kuzimaliza hasira za wapinzani dhidi yake.

WABRAZIL WAZIDISHA MAANDAMANO YAO LICHA YA KAULI YA RAIS WAO

Waandamanaji nchini Brazil wameendelea na maandamano yao licha ya Rais wa taifa hilo, Dilma Rousseff kuahidi kufanya mabadiliko ili kuhakikisha anatii kiu ya wananchi wake kipindi hiki watu tisa wakitajwa kupoteza maisha kutokana na ghazi zinazo fuatia maandamano hayo. Maandamano makubwa yanaendelea kushuhudiwa nchini Brazil ambapo wananchi wanapiga kelele kufuatia kupanda kwa gharama ya maisha. Mamia ya waandamanaji wamejitokeza kwenye mitaa ya Rio De Janeiro na Sao Paoul na kufunga barabara wakionesha kuchukizwa na ahadi ambazo zimetolewa na Rais Rousseff ya kuhakikisha anaboresha huduma za usafiri, elimu na afya.
Jeshi la Polisi limelazimika kutumia nguvu kukabiliana na waandamanaji hao ambao wamesema hawapo tayari kuona fedha za umma zinatumika kwenye masuala ambayo hayana mchango kwenye maendeleo yao. Ghasia hizo zinaendelea kupindi hiki Rais Rousseff akiomba msaada kutoka katika Bunge kuhakikisha mabadiliko aliyoyatangaza yanaweza kufikiwa na hatimaye wananchi waweze kunufaika kupitia kodi zao. Waandamanaji hao wameweka bayana kabisa lengo lao ni kuzuia hata kufanyika kwa Kombe la Dunia lililopangwa kufanyika mwakani wakitaka fedha zinazotumiwa kwenye maandalizi hayo zitumike kuboresha maisha yao.

POLISI BRAZIL WAENDELEA KUKABILIANA NA MAANDAMANO

Jeshi la Polisi nchini Brazil linaendelea kukabiliwa na kibarua kigumu cha kupambana na waandamanaji ambao wameanza kutumia mbinu tofauti ikiwa ni pamoja na kufanya maandamano kwenye Kiwanja cha mpira kilichotumika kwa mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la Mabara. Ghasia kubwa zilizuka nje ya uwanja wa mpira wa miguu wa Belo Horizonte kutokana na waandamanaji kuanza kufanya fujo ikiwa ni sehemu ya shinikizo laokwa serikali iweze kusikiliza kilio chao cha kuboresha maisha ya wananchi.
Waandamanaji wapatao elfu arobaini wamejitokeza kwenye mitaa iliyokaribu na Uwanja wa Mpira wa Belo Horizonte na hivyo Jeshi la Polisi likalazimika kutumia mabomu ya machozi na risasi za mpira kuwasambaratisha watu hao. Takwimu zinaonesha watu milioni moja na laki mbili walijitokeza kwenye maandamano ya nchi nzima wakiendelea kushinikiza serikali ichukue hatua dhidi ya viongozi wala rushwa sanjari na kuboresha huduma za kijamii.
Maandamano hayo haya ya kulenga viwanja yanakuja kipindi hiki Rais Dilma Rousseff akitaka msaada kutoka kwa Bunge na Baraza la Seneti ili aweze kuharakisha mkakati wa kufanya mabadiliko yatakayosaidia kuboresha sekta za afya, elimu na usafiri.

JESHI LA NIGERIA LAKAMATA VIONGOZI WA BOKO HARAM

Msemaji wa Jeshi la Nigeria amethibitisha taarifa za kutiwa mbaroni viongozi kadhaa waandamizi wa kundi la Boko Haram katika maeneo ya kaskazini mwa Nigeria. Brigedia Chris Olukolade amesema leo kuwa, licha ya kutiwa mbaroni vinara waandamizi wa kundi hilo, jeshi la Nigeria limefanikiwa kugundua ghala la silaha mbalimbali la kundi hilo. Brigedia Olukolade ameongeza kuwa, miongoni mwa silaha na zana za kijeshi zilizokamatwa na jeshi la nchi hiyo ni maroketi ya aina mbalimbali, mada za milipuko, zana za mawasiliano na laptop kadhaa.
Msemaji wa jeshi la Nigeria amesema kuwa, tokea mwezi Mei mwaka huu, kikosi maalumu kimewekwa katika majimbo ya Borno na Yobe kaskazini mwa Nigeria na kimefanikiwa kuziangamiza kambi kadhaa za kundi hilo.

IRAN YAKAMATA MAJASUSI

Maafisa wa usalama wa taifa wa Iran wamefanikiwa kutambua na kusambaratisha mitandao hatari zaidi  ya ujasusi, ugaidi na uharibifu ambayo ilikuwa ikipata msaada wa mashirika ya ujasusi ya Marekani, utawala wa Kizayuni na baadhi ya nchi za eneo. Kwa mujibu wa Bw. Karimi, Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa katika mkoa wa Fars Kusini mwa Iran, mitandao hiyo ya kijasusi ilikuwa imepanga kutekeleza vitendo vya kikatili vya kigaidi kama vile kutega mabomu katika maeneo ya sala za Ijumaa, kushambulia maeneo ya kupiga kura na mikusanyiko ya wananchi katika siku za uchaguzi wa Juni 14. Bw. Karimi ameongeza kuwa maafisa wa usalama pia wamesambaratisha kundi linalofungamana na kijikundi cha kigaidi chenye misimamo mikali kinachopata himaya ya mashirika ya kijasusi ya nchi za Ulaya. Amesema kundi hilo lilikuwa limepanga pia kutekeleza hujuma za mabomu. Bw. Karimi ameendelea kusema kuwa maafisa wa usalama wa taifa pia wamewatambua na kuwatia mbaroni wanachama wa genge la kutayarisha na kusambaza silaha pamoja na zana za vita na kwamba genge hilo lilikuwa lina uhusiano na makundi yaliyo nje ya nchi. Amesema genge hilo pia lilikuwa linapanga kutekeleza hujuma wakati wa uchaguzi katika mkoa wa Fars, kusini mwa Iran.
Katika miaka ya hivi karibuni Iran imefanikiwa kusambaratisha makundi ya kijasusi na kigaidi yanayopata himaya ya mashirika ya kijasusi ya Marekani na utawala haramu wa Israel.

Wednesday, June 26, 2013

UJERUMANI YATAKA MAJIBU YA UJASUSI WA UINGEREZA

Waziri wa sheria wa Ujerumani, Sabine Leutheusser-Schnarrenberger, amewaandikia barua mawaziri wawili wa Uingereza akitaka kupewa maelezo kamili kuhusu kiwango cha hatua za kijasusi za shirika la ujasusi la nchi hiyo ya Uingereza katika Ujerumani. Kwa mujibu wa gazeti la Guardian waziri huyo wa Ujerumani ametaka majibu kutoka Uingereza kuhusu mpango wa nchi hiyo unaojulikana kama Tempora uliotumiwa kuzichunguza data zote za mawasiliano za raia nchini Ujerumani. Mpango huo uliofichuliwa na mfichua siri wa Kimarekani Edward Snowden umewashtuwa wanasiasa mjini Berlin. Ujerumani imewataka mawaziri wa sheria na mambo ya ndani nchini Uingereza kufafanua juu ya uhalali wa mpango huo wa Tempora na nani aliyeuidhinisha. Wizara ya mambo ya ndani ya Uingereza imesema itajibu barua hiyo katika wakati mwafaka lakini haikutowa maelezo zaidi. Katika mpango huo wa kijasusi inadaiwa barua pepe, ujumbe katika mitandao ya kijamii, mawasiliano ya simu na nyendo nyinginezo kwenye mitandao za wakaazi wa Ujerumani zimekuwa zikifuatiliwa.

RAIS OBAMA AELEKEA AFRIKA

Rais Barack Obama hii leo anaelekea barani Afrika katika ziara iiliyosubiriwa kwa muda mrefu. Hata hivyo ziara hiyo imegubikwa na suala la hali mbaya ya afya ya kiongozi wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela. Ziara hiyo ya wiki moja itamfikisha rais Obama nchini Senegal, Afrika Kusini na Tanzania. Ikulu ya Marekani imesema itashauriana na familia ya Mandela kuona ikiwa rais Obama anaweza kumtembelea mwanasiasa huyo mkongwe aliyelazwa katika hospitali ya mjini Pretoria kwa muda wa wiki tatu sasa. Mandela na Obama hawajawahi kukutana ana kwa ana tangu rais huyo wa Marekani alipochaguliwa kuingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 2008.

KIKOSI CHA UN KUANZA KAZI MALI JULAI MOSI

Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kitaanza operesheni zake nchini Mali ifikapo Julai Mosi mwaka huu baada ya Baraza la Usalama la umoja huo kutoa kibali hapo jana kwa kikosi hicho.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lenye nchi wanachama 15 mwezi Aprili liliafiki kutumwa kikosi hicho cha askari jeshi 12,600 kinachojulikana kwa jina la Minusma.
Wanajeshi wa Ufaransa watakisaidia kikosi hicho cha Umoja wa Mataifa katika kupambana na waasi wa kaskazini mwa Mali iwapo itahitajika. Ufaransa ikisaidiwa na wanajeshi elfu mbili wa Chad ilianzisha uvamizi wa kijeshi huko Mali kwa kile ilichokitaja kuwa mapambano ya kuwatokomeza waasi wa kaskazini mwa Mali.

WANAJESHI LIBYA WAULIWA NA WATU WENYE SILAHA

Wanajeshi wa Libya wasiopungua sita wameuawa baada ya watu wenye silaha wasiojulikana kukishambulia kituo cha upekuzi cha jeshi la nchi hiyo karibu na mji wa Sirte. Jeshi la Libya limeeleza kuwa askari jeshi hao wameuawa wakati watu kadhaa waliokuwa wamejizatiti kwa silaha walipokivamia kituo cha upekuzi cha kijeshi katika mji wa Sirte hapo jana. Jeshi la Libya limelizingira eneo hilo baada ya tukio hilo na tayari limeanzisha uchunguzi kuhusu shambulio hilo. Katika upande mwingine, wakazi wa mji wa Benghazi wameendelea kulalamikia kuzidi kuzorota hali ya usalama nchini Libya. Hadi kufikia sasa hakuna kundi wala mtu aliyekiri kuhusika nan shambulizi hilo la jana. Benghazi ambao ni mji wa pili kwa ukubwa nchini wa Libya katika wiki za hivi karibuni umeshuhudia wimbi la machafuko huku vituo kadhaa vya polisi vikiripuliwa kwa mabomu.

OFISI ZA CHAMA CHA MOSRI ZACHOMWA MOTO

Waandamanai wanaopinga serikali ya Rais Mohammad Morsi wa Misri wamechoma moto ofisi za chama chake cha Uhuru na Uadilifu ambacho ni tawi la kisiasa la harakati ya Ikhwanul Muslimin. Shirika la habari la al-Yaum Sub’h limeripoti kuwa, ofisi hiyo ilivamiwa na kuharibiwa kabla ya kuteketezwa katika mji wa Ibrahimia kaskazini mashariki mwa nchi. Habari zaidi zinasema kuwa, maafisa waandamizi wa chama hicho waliokuwa ofisini wakati wa tukio hilo walilazimika kukimbilia usalama wao katika msikiti uliokuwa karibu. Mali ya thamani kubwa imeharibiwa kwenye tukio hilo. Rais Morsi anakabiliwa na mashinikizo makubwa kutoka kwa wapinzani ambao wanadai uongozi wake wa mwaka mmoja haujaweza kutatua matatizo yanayowakabili Wamisri wa kipato cha chini. Wapinzani hao wakingozwa na shakhsia mashuhuri kama vile Mohammad el-Baradei na Amr Musa wamepanga kufanya maandamano makubwa Juni 30 ili kushinikiza kujiuzuu rais huyo.

GAZETI ANNUUR JUNI 21, 2013

POLISI UJERUMANI YAWASAKA MAGAIDI

Polisi wamefanya misako katika majimbo matatu ya Ujerumani ikiwa ni sehemu ya kinachoeleweka kuwa  uchunguzi wa mipango ya kufanyika mashambulio ya kigaidi.
Polisi hao walifanya misako katika majimbo ya Baden Württemberg,Bavaria na Saxony.
Kwa mujibu wa taarifa, watu wanaotuhumiwa kuwa    waislamu wenye itikadi kali,walipanga kufanya  mashambulio kwa kutumia ndege za sanamu zilizojazwa mabomu ambayo yangeliweza kufyatuliwa kutokea mbali.
Baadhi ya ripoti zimesema kuwa watuhumiwa hao wana nasaba ya Kitunisia na walikuwa wanasomea uhandisi kwenye chuo kikuu cha Stuttgart katika jimbo la kusini mwa Ujerumani ,la Baden Württemberg.
Misako ya polisi inafuatia tahadhari zilizotolewa na idara ya Ujerumani ya upelelezi wa ndani, kuwa  Ujerumani imekuwa lengo kuu la magaidi wa kiislamu wenye itikadi kali.

WATU WA4 WANYONGWA NIGERIA

Wafungwa wanne wamenyongwa kusini mwa Nigeria, katika kile maafisa wanasema kuwa hukumu ya kwanza ya kunyongwa kutekelezwa kwa miaka saba. Kamishna wa haki katika jimbo la Edo, Henry Idahagbon, aliambia waandishi wa habari kuwa wafungwa hao walinyongwa baada ya kuhukumiwa kifo kwa makosa ya wizi wa mabavu na mauaji. Shirika la Amnesty International lilisema kuwa hatua hiyo ya kuwanyonga wafungwa ni jambo la kuhuzunisha sana kwa watetezi wa haki za binadamu nchini Nigeria. Zaidi ya wafungwa 1,000 nchini Nigeria wanaaminika kuhukumiwa kifo .
Vyombo vya habari nchini humo vinasema kuwa Rais Goodluck Jonathan hivi karibuni aliwataka magavana wa majimbo kutia saini vibali vya hukumu ya kifo katika jitihada za serikali kupunguza visa vya uhalifu.
Bwana Idahagbon alisema kuwa wananume wanne walinyongwa katika gereza la Benin baada ya mahakama kuamuru wanyongwe siku ya Jumatatu. Alisema kesi zote za rufaa, hazikuweza kufua dafu na hukumu zao tayari zikuwa zimetiwa saini -mbili na magavana wa Edo Governor Adams Oshiomhole, huku nyingine zikitiwa saini na magavana wa majimbo mengine. Ikiwa itathibitishwa , hatua hii ya kunyongwa ni ishara ya kurejea kwa sheria kali ya hukumu ya kunyongwa nchini Nigeria. Wahudumu wa magereza ndio waliotekeleza hukumu ya kunyongwa , kitengo cha serikali wala sio jimbo la Edo. Kulikuwa na ripoti za kutatanisha kuhusu hali ya mfungwa wa tano. Chino Obiagwu wa kitengo cha sheria na mradi wa kuwasaidia wafungwa hao alisema kuwa mwanaume huyo alinyongwa.
Hukumu ilicheleweshwa kwa muda kwa sababu za kiufundi lakini baadaye wakapashwa habari kwa njia ya barua pepe, alisema bwana Obiagwu.  Lakini bwana Idahagbon alisema mwanaume huyo hakunyongwa kwa sababu hukumu yake ilisema kuwa auawe kwa kupigwa risasi. Hata hivyo shirika la Amnesty International limesema kuwa limepokea habari zinazoweza kuthibitisha kuwa wafungwa wanne walinyongwa mjini Benin.

RAIS WA BRAZIL AITISHA KURA YA MAOANI

Rais Dilma Rousseff wa Brazil ameelezea uamuzi wa serikali ya nchi hiyo wa kuitisha kura ya maoni juu ya marekebisho ya kisiasa nchini humo.
Rais Rousseff amesema kuwa, serikali ya Brazil imeamua kuitisha kura hiyo ya maoni kwa shabaha ya kukomesha maandamano dhidi ya serikali na machafuko ya kijamii yaliyoikumba nchi hiyo.
Mara baada ya kufanya mazungumzo na magavana, mawaziri na mameya wa miji yote nchini humo, Rais Rousseff ameongeza kuwa, suala la kufanyika marekebisho ya kisiasa limekuwa likipewa kipaumbele na serikali na kusisitiza kuwa, hivi karibuni watachaguliwa  wajumbe wa jopo litakalokuwa na jukumu la kutayarisha mchakato wa mabadiliko ya kisiasa nchini humo.
Wananchi wa Brazil wamekuwa wakiandamana wakipinga gharama kubwa za kuandaa fainali za kombe la dunia mwaka 2014 nchini humo, wa kunataka kwanza iboreshwe hali ya maisha na huduma za umma kwa wananchi.

BERLOSCONI AHUKUMIWA MIAKA SABA JELA

Mahakama ya mji wa Milan nchini Italia imemuhukumu kifungo cha miaka saba jela, Silvio Berlusconi Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo. Berlusconi ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Italia kwa vipindi vitatu tofauti, alipatikana na hatia ya kujihusisha na vitendo vya ngono na mabinti walio na umri wa chini ya miaka 18. Mahakama hiyo pia imemfungia Berlusconi mwenye umri wa miaka 76 kujishughulisha na masuala ya siasa kwa maisha yake yote baada ya kukumbwa na kashfa hiyo.
Hii ni mara ya tatu kwa Waziri Mkuu wa zamani wa Italia kuhukumiwa katika kipindi cha miezi tisa iliyopita. Mwezi Oktoba 2012 alihukumiwa kifungo cha miaka minne jela baada ya kupatikana na hatia ya kukwepa kodi na mwezi Disemba mwaka huohuo alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja kwa kosa la kutumia ushahidi wa kunasa mazungumzo ya simu kinyume cha sheria.
Mahakama ya Milan imetangaza kuwa, Berlusconi anayo haki ya kukata rufaa kwenye Mahakama ya Rufaa.

SUDAN YASEMA MATAMSHI YA MAREKANI NI YA KIPUUZI

Serikali ya Sudan imeyataja matamshi ya afisa mmoja wa Marekani aliyetoa wito wa kushambuliwa kijeshi viwanja vyote vya ndege za kijeshi vya nchi hiyo kuwa ni upuuzi na hayana maana. Hayo yamesemwa leo na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan Abubakar El-Saddiq na kuongeza kuwa mwito wa KenIsaacs, Naibu Katibu Mkuu wa Taasisi ya Kimataifa ya Mipango na Mendeleo 'Samaritan's Purse' ya kutaka kushambuliwa viwanja vyote vya ndege za kijeshi vya nchi hiyo kuwa hayana maana yoyote. El-Saddiq  amesema kuwa, madai hayo yanadhihirisha chuki na uadui wa baadhi ya watu wenye misimamo mikali dhidi ya watu na taifa la Sudan. Ameongeza kuwa, mienendo ya watu kama hao, haina nia nyengine ghairi ya kuficha jinai kubwa zinazofanywa na waasi wanaojiita 'Mrengo wa Mapinduzi' dhidi ya raia wasio na hatia wa miji miwili ya Abu Karshola na Um Rawaba. Aidha Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan ameyalaumu makundi ya watu wenye misimamo mikali nchini Marekani kwa kubadilisha ukweli halisi wa mambo kwa ajili ya kufikia malengo yao machafu. Hivi karibuni Ken aliitaka serikali ya Washington kufanya mashambulizi dhidi ya viwanja vya ndege za jeshi la Sudan kwa kile alichodai eti ni kujibu mashambulizi ya serikali ya Khartoum dhidi ya wakazi wa jimbo la Darfur na Blue Nile.

RAIS WA UFARANSA AAHIDI KUPAMBANA NA CHUKI DHIDI YA UISLAM

Rais Francois Hollande wa Ufaransa ameahidi kupambana na wimbi la uadui na chuki dhidi ya Uislamu katika nchi hiyo ya barani Ulaya. Rais Hollande amesema hayo mbele ya hadhara kubwa ya wawakilishi wa taasisi na asasi za kiserikali na kiraia pambizoni mwa mji mkuu Paris na kusisitiza kwamba, atapambana na wimbi la chuki dhidi ya Uislamu. Hollande anatoa ahadi hiyo katika hali ambayo, katika majuma ya hivi karibuni Waislamu wa Ufaransa hususan wanawake wanaovaa vazi tukufu la hijabu wamekabiliwa na wimbi kubwa la mashambulio ya watu waliofurutu ada na wenye chuki kubwa dhidi ya Uislamu. Miongoni mwa matukio ya chuki dhidi ya Uislamu nchini Ufaransa katika mwaka huu wa 2013 ni kushambuliwa wanawake kadhaa waliokuwa wamevaa hijabu katika kitongoji cha Val-d'Oise kaskazini mwa nchi hiyo. Viongozi wa Muungano wa Taasisi za Kiislamu nchini Ufaransa (UOIF) sanjari na kuonesha wasi wasi wao mkubwa kuhusiana na vitendo hivi ambavyo vimegeuka na kuwa jambo la kawaida, wamewataka viongozi wa serikali kuvunja kimya chao na kuchukua hatua kali za kuhitimisha vitendo hivyo vya kinyama dhidi ya Waislamu. Takwimu zinaonesha kuwa, vitendo vya mashambulio dhidi ya maeneo ya kidini ya Waislamu nchini Ufaransa vimeongezeka mno katika majuma ya hivi karibuni. Baraza la Kiutamaduni la Waislamu nchini Ufaransa (CFCM) limetangaza katika ripoti yake ya hivi karibuni kwamba, tangu kuanza mwaka huu wa 2013 zaidi ya misikiti 10 imeshambuliwa na kuvunjiwa heshima nchini humo. Nayo Kamati ya Kupambana na Kampeni za Kuuogopesha Uislamu nchini Ufaransa (CCIF) imetangaza kuwa, itafuatilia suala la kushambuliwa wanawake wa Kiislamu nchini humo. Katika hali ambayo vyombo vya habari vya Ufaransa vinafumbia macho mashambulio dhidi ya wanawake wa Kiislamu nchini humo, hivi karibuni wanawake wanne wa Kiislamu walishambuliwa na kupigwa vibaya katika viunga vya Paris. Mmoja wa wanawake wa Kiislamu ambaye alishambuliwa katika mji wa Argenteui aliumia vibaya na kusababaisha mimba yake kutoka.  Wataalamu wa mambo wanaamini kwamba, makundi yenye kufurutu ada na yenye chuki na Uislamu yameingiwa na wasi wasi na kihoro kikubwa kutokana na kuongezeka kwa kasi idadi ya Waislamu barani Ulaya hususan nchini Ufaransa. Hivi sasa malalamiko makubwa ya Waislamu wa Ufaransa ni hatua ya vyombo vya habari vya nchi hiyo ya kunyamazia kimya mashambulio na vitendo vya ubaguzi dhidi ya Waislamu. Ufaransa ina wakazi milioni 62.3 huku milioni 6 wakiwa ni Waislamu. Wataalamu wa mambo wanasema kuwa, Ufaransa inashikilia nafasi ya kwanza barani Ulaya kwa kuwa na idadi kubwa ya Waislamu na dini ya Kiislamu inahesabiwa kuwa ya pili kwa ukubwa nchini humo baada ya Ukristo. Hivyo basi kuongezeka vitendo vya chuki na mashambulio dhidi ya Waislamu vinaweza kutathminiwa katika fremu ya hofu na wasi wasi wa kupata nguvu Uislamu nchini Ufaransa.

JESHI LA afghanistan lazima shambulio dhidi ya ikulu

Wapiganaji wa kundi la wanamgambo wa Talibans, wameendesha shambulio dhidi ya Ikulu ya rais jijini Kaboul bila mafaanikio, baada ya majeshi ya serikali kufaulu kuzima shambulio hilo na kuwauawa washambuliaji wote. Tukio hili linajiri juma moja tu baada ya kuanzishwa kwa mchakato wa amani nchini humo na ambapo ofisi ya kisiasa ya kundi hilo, imefunguliwa jijini Doha. Mkuu wa polisi jijini Kaboul Mohammad Ayoub Salangi amesema takriban waasi wanne walioendesha shambulio hilo wameuawa, na hakuna wengine walioathirika.
Upande wake naibu mkuu wa polisi Mohammed Daud Amin amefahamisha kuwa Washambuliaji walikuwa ndani ya magari mawili tofauti huku wakibebelea mabomu ya kulipuka na kupita karibu na majengo ya Ikulu ya taifa na majengo ya shirika la kijasusi la nchini Marekani CIA, na walijaribu kujilinganisha na wanajeshi wa vikosi vya NATO nchini Afghanistani ISAF. Mohammad Daud Amin ameendelea kuwa wahalifu hao walikuwa katika magari mawili yanayo tumiwa na vikosi vya ISAF huku wakivalia sare za wanajeshi hao wakiwa na vifaa aina ya wanavyo tumia wanajeshi wa vikosi vya kujihami vya nchi za magharibi NATO nchini Afghanistani.
Magari hayo mawili yalijaribu kuvuka kituo cha uchunguzi, baada ya moja kufaulu kuvuka na nyingine kushindwa polisi ilitilia mashaka gari hilo na ndipo mapigano yakaanza na magari hayo yakalipuka. Duru kutoka ikulu ya rais nchini Afghanistani zaarifu kuwa rais wa nchi hiyo Hamid Karzai alikuwa amepanga kufanya kikao na vyombo vya habari mapema leo asubuhi. Kundi la wapiganaji wa Talibans limekiri na kujigamba kuhusika na mashambulzi hayo kupitia msemaji wake Zabihullah Mujahid ambaye amesema wanamgambo wa kundi hilo wameshambulia ofisi za CIA, ofisi za Ikulu ya rais pamoja na wizara ya ulinzi.

MAREKANI YAITAKA URUSI KUMRUDISHA ERDOWAN

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ameitolea wito serikali ya Marekani kuonyesha ushirikiano wake kwa kumrejesha nchini Marekani Edward Snowden anaetafutwa na taifa hilo kwa kosa la uhaini, na kudai kuwa serikali ya Washington haitaki mzozano wowote kuhusu swala hilo. Akiwa ziarani nchini Saudia Arabia, John Kerry amesema kwamba kurejeshwa nchini Marekani kwa afisa huyo wa zamani wa Idara ya Ujasusi ya Marekani CIA na Idara ya Usalama NSA, ni swala la kuheshimu sheria.
Hata hivyo serikali ya Urusi imesema afisa huyo wa zamani wa CIA hajakanyaga nchini humo, na kutupilia mbali madai ya serikali ya Marekani kwamba yupo nchini Urusi. serikali hiyo imeendelea kuituhumu Marekani kuhusika katika kutoroka kwa afiasa huyo. Inadaiwa kuwa Snowden aliwasili kwenye uwanja wa ndege wa Sheremetyevo jijini Moscou katika ndege iliokuwa ikitokea jijini Hong Hong siku ya Jumapili. Viongozi wa Urusi wao wanasisitiza kuwa afisa huyo hakutoka ndani ya ndege.
Hali inakuja kuhatarisha mvutano baina ya Urusi na Marekani, pamoja na China wakati mataifa hayo yakiangalia kijicho kibaya kwa kushindwa kuafikiana juu ya vita vinavyoendelea nchini Syria. akizungumza na vyombo vya habari waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema hawahusika kamwe na safari za Snowden na uhusinao wake na vyombo vya sheria nchini Marekeni. Hata hivyo waziri Lavrov hakukanusha aidha kuthibitisha kuwa afisa huyo wa zamani wa idara ya ujasusi nchini Marekani CIA na mataalamu wa idara ya Usalama NSA aliwasili kwenye uwanja wa ndege wa Sheremetyevo juzi Jumapili, bali amesisitiza kuwa  Snowden hajakanyaga ardhi ya Urusi na hakutoka kwenye Uwanja wa ndege.

TSVANGIRAI APINGANA NA MUGABE

Waziri mkuu nchini Zimbabwe Morgan Tsvangirai ametoa wito kwa mahakama ya kikatiba nchini humo kufutilia mbali agizo la rais wa taifa hilo Robert Mugabe kuandaa uchaguzi mwishoni mwa mwezi Julai. Tsvangirai ameonya kuwa huenda taifa hilo likakumbwa na hali ya switofahamu iwapo uchaguzi huo utafanyika.
Katika ombi lake waziri huyo anasema kuwa mda uliotolewa kuandaa shughuli ya usajili wa wapiga kura na uteuzi wa wagombea ni mchache mno. Hata hivyo Tsvangirai hakusema ni lini angependa uchaguzi huo ufanyike. Tayari uamuzi huo wa Mugabe kuitisha uchaguzi mapema kuliko ilivyotarajiwa, umekashifiwa na viongozi wengine wa mataifa ya Afrika Kusini.
Rais Mugabe alikwenda mahakamani mwezi jana kufuatia shinikizo kutoka kwa muungano wa nchi za Afrika Kusini (SADC) kubana hatua ya kuakhirisha shughuli nzima ya uchaguzi. Ikiwa Tsvangirai atashinda kesi hii, anasema mahakamana itakuwa imezuia jambo lisilo la kisheria kuweza kutumbukiza nchi katika hali ya switofahamu. Tsvangirai anataka uchaguzi ufanyike tu baada ya mageuzi ya sheria za uchaguzi ambayo yametokana na katiba mpya.

Tuesday, June 25, 2013

WHY THERE WAS NO UPDATES ON BLOG

Sorry kwa wote nilikuwa Bizee zaidi this week na nipo peke yangu na ninafanya kazi almost siku nzima na pia tunatofautiana majira.
So keep in touch with our blog na tutapashana as much as we can

Karibuni nyote

WAZIRI MKUU MISRI ATAHADHARISHA VITA YA KIMADHEHEBU

Waziri  mkuu  wa  Misri  ameshutumu  mauaji ya  Waislamu wanne  wa  madhehebu  ya  Shia  yaliyofanywa  na  kundi la  Wasunni  ambalo  linajumuisha  Wasalafi  wenye msimamo  mkali  katika  kijiji  karibu  na  mji  mkuu  Cairo. Taarifa  iliyotolewa  na  ofisi  ya  waziri  mkuu  Hesham Kandil leo imesema  kuwa  anafuatilia  kwa  karibu uchunguzi  kuhusu  tukio  hilo ili  kuhakikisha  kuwa wahusika  wanaadhibiwa.
Misri  ni  nchi  yenye  waumini  wengi  wa  madhehebbu  ya Sunni  ikiwa  na  idadi  ndogo  ya  Washia. Kiasi  ya asilimia  10  ya  wakaazi milioni  90  wa  nchi  hiyo  ni Wakristo. Shambulio  hilo  lililotokea  jana  Jumapili limekuja  wiki  moja  baada  ya  viongozi  kadha  wa  kundi la  Salafi  kuwakashifu  Washia  wakati  wa  mkutano uliohudhuriwa  na  rais  wa  nchi  hiyo Mohammed Mursi. Mmoja  wa  viongozi  hao  wa  kidini  Mohammed Hassan , amemtaka  Mursi  kutofungua  mpango  wa  Misri  kwa washia, akisema  kuwa  hawaingii mahali  bila  ya  kuleta ufisadi.

SERIKALI YA MALI YALALAMIKA KUBAKIA WANAJESHI WA UFARANSA

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Mali amekosoa vikali hatua ya Ufaransa ya kuendelea kuweko kijeshi katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.  Tieman Hubert Coulibaly amesema bayana kwamba, Mali haiwezi tena kuvumilia kuweko kwa wanajeshi takribani elfu moja katika ardhi ya nchi hiyo. Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Mali amesisitiza kwamba, Bamako haioni udharura wa kuendelea kuweko nchini humo majeshi ya Ufaransa ambayo yako katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo ya Kiafrika. Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Mali amesema, kuondoka majeshi ya Ufaransa nchini humo kutafungua haraka njia ya kupatikana amani katika ardhi ya nchi hiyo. Hayo yanajiri katika hali ambayo, hivi karibuni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon alikaribisha makubaliano ya amani yaliyotiwa saini kati ya serikali ya Mali na waasi wa Tuareg. Ban alisema katika ujumbe wake kwamba, pande mbili hizo zinafaa kuhakikisha kwamba makubaliano hayo yanatekelezwa kikamilifu.

SILAHA TOKA ISRAEL ZAWASILI SYRIA

Shehena ya kwanza ya silaha za kisasa zilizoundwa Israel imetumwa kwa magaidi wa Syria. Mtandao wa Intaneti ya gazeti la al Manar la Palestina umeripoti kuwa hatua ya Israel ya kutuma ya shehena ya kwanza ya silaha za kisasa kwa makundi ya kigaidi huko Syria imekuja kufuatia ombi la Washington la kuutaka utawala wa Kizayuni ufanye hivyo.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa, ndege kadhaa za kijeshi za Israel zimesafirisha silaha hizo hadi nchini Uturuki kwa nyakati mbili tofauti na baadae silaha hizo zitapelekwa kwenye maghala maalumu ya silaha kwenye mpaka ya Uturuki na Syria na baadaye kutumwa kwa magaidi wanaofanya mauaji ndani ya ardhi ya Syria. Utawala wa Kizayuni wa Israel umetoa misaada hiyo ya kijeshi kwa magaidi wa Syria huku mfalme wa Saudi Arabia akiutaka utawala wa Kizayuni ufanye mashambulizi mengine ya anga ndani ya ardhi ya Syria.

ASKARI 57 WA MAREKANI WAINGIA SYRIA

Duru za habari zinaarifu kuingia nchini Syria askari 57 waliostaafu wa Marekani kwa ajili ya kuwasaidia magaidi wanaotekeleza mauaji na uharibifu nchini humo. Shirika la Habari la Fars limeripoti kuwa maafisa hao 57 waliwasili nchini Uturuki na ndege ya Kimarekani ya C-130 na kuingia Syria kupitia njia ya mkoa wa mpakani wa Reyhanlı. Aidha ndege hiyo ilikuwa imebeba pia zana za kijasusi kwa ajili ya kuwasaidia magaidi. Wakati hayo yakiripotiwa, kikao cha siku ya Jumamosi cha nchi zinazojiita eti marafiki wa Syria kilichofanyika mjini Doha, Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi ikiwemo Uturuki, Qatar na Saudia, zilikubaliana kuongeza misaada yao kwa wapinzani wa Syria na makundi ya kigaidi yenye mafungamano na kundi la kigaidi la Al-Qaida. Wakati huo huo, magaidi ambao wanaonekana kushindwa na jeshi la serikali halali ya Rais Bashar al-Assad wa nchi hiyo, wameanzisha wimbi jipya la kuwashambulia ovyo raia wasio na hatia wa nchi hiyo, ili kwa njia hiyo waweze kuishinikiza serikali ya Damascus. Weledi wa masuala ya kisiasa wa Mashariki ya Kati wanaamini kuwa, kikao cha Doha, Qatar hakikufanikiwa na kwamba, ni mwanzo wa kushindwa.

UJUMBE WA KIDIPLOMASIA TOKA ETHIOPIA WAWASILI MISRI

Ujumbe wa kidiplomasia unaoongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia ambaye pia ni  mkuu wa Kituo cha Amani cha nchi hiyo umewasili mjini Cairo Misri kwa ziara ya siku tatu kwa lengo la kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo.
Baada ya Ethiopia kuchukua uamuzi wa kujenga bwawa la Renaissance au ambalo mara nyingine linajulikana kwa jila la Millennium Dam, kwenye Mto Nile na hivyo kuzusha mvutano katika uhusiano wa nchi hizo, hii ni mara ya kwanza kwa ujumbe wa kidiplomasia wa Ethiopia kufanya safari nchini Misri. Kamati ya Wataalamu wa Kimataifa inasema kuwa uamuzi wa Ethiopia wa kujenga bwawa hilo katika mto uliotajwa unahatarisha maslahi ya nchi mbili za Misri na Sudan zinazonufaika kwa sehemu kubwa na maji ya mto huo. Kamati hiyo ambayo inajumuisha wataalamu kutoka nchi za Ethiopia, Sudan, Misri, Afrika Kusini, Ufaransa, Ujerumani na Uingereza, ilibuniwa sambamba na kuanza shughuli za ujenzi wa bwala la Renaissance ili kutathmini manufaa ya nchi tatu za Ethiopia, Misri na Sudan kutokana na maji ya Mto Nile. Kamati hiyo imetayarisha ripoti ya kurasa 800 na kuiwasilisha kwa serikali za nchi hizo tatu ili zipate kuifanyia kazi. Mwishoni mwa mwezi Mei uliopita serikali ya Ethiopia ilianza kubadilisha mkondo wa maji ya Mto Blue Nile ambao unachangia sehemu kubwa ya maji ya Mto Nile na kuyaelekeza kwenye mradi wa bwawa hilo ambalo linatathminiwa kugharimu dola bilioni 4 na milioni 700. Mto wa Blue Nile huungana na wa White Nile katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum na kuunda Mto Nile na kupitia ardhi ya Misri kabla ya kumwaga maji yake kwenye bahari ya Mediterranean. Kwa msingi huo, kujengwa bwawa la Renaissance kwenye mto huo kumeitia wasiwasi mkubwa Misri ambayo inahofia kwamba huenda ikapoteza hisa kubwa ya maji ya mto huo. Licha ya makelele mengi yaliyopigwa na Misri kuhusiana na suala hilo lakini mazungumzo ya hivi karibuni ya ujumbe wa kidiplomasia wa nchi hiyo huko mjini Addis Ababa Ethiopia, yalikuwa na mafanikio. Licha ya upinzani wa Misri wa kujengwa bwawa hilo kwenye Mto Nile lakini Rais Yoweri Museveni wa Uganda ameunga mkono mradi huo muhimu wa Ethiopia na kusema kuwa umeme utakaozalishwa na bwawa hilo utazifaidi nchi nyingi zinazopakana au kuchangia maji ya Mto huo.
Katika upande wa pili Ban Ki-moo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezitaka nchi mbili za Misri na Ethiopia kutatua kwa amani hitilafu zao kuhusiana na suala hilo. Amemtaka Rais Muhammad Mursi wa Misri ambaye ametishia kuingia kwenye vita ili kutetea maslahi ya nchi yake kuhusiana na maji ya Mto Nile kuketi pamoja na  Waziri  Mkuu Hailemariam Desalegn wa Ethiopia kwenye meza ya mazungumzo ili kutatua kwa njia za kidiplomasia matatizo yaliyopo. Wakati huohuo hivi karibuni bunge la Ethiopia lilipasisha mswada mpya ambao utachukua nafasi ya mkataba wa kikoloni ambao inazipa nchi za Sudan na Misri fursa ya kunufaika na maji ya Mto Nile. Mkataba huo pia ulitiwa saini na nchi sita zinazopakana na mto huo. Kwa mujibu wa mswada huo, nchi zote zinazochangia maji ya mto huo sasa zinaruhusiwa kunufaika na maji hayo katika kuanzisha miradi ya maendeleo.

UHUSIANO WA RUSSIA NA MAREKANI WAZIDI KUKOROGEKA

Uhusiano kati ya Russia na Marekani umezidi kuvurugika baada ya Moscow kushindwa kumkamata afisa wa zamani wa CIA aliyeanika hadharani siri za Washington wiki mbili zilizopita. Edward Snowden, hivi majuzi alifichua kwamba Marekani imekuwa ikidukua mitandao ya intaneti kama vile Google, Facecook, Youtube na Yahoo na kukusanya taarifa za siri za watu kote duniani; jambo ambalo ni kinyume na sheria za kimataifa. Snowden pia alifichua kwamba mashirika ya kijasusi ya Marekani ya CIA na NSA yamekuwa yakinasa mazungumzo ya simu ya watu kote duniani. Ufichuzi huo uliamsha hasira za watu hususan huko Marekani ambako katiba ya nchi imesisitiza kuheshimiwa faragha ya mtu. Snowden alikimbilia Hongkong baada ya ufichuzi huo na hapo jana aliondoka na kuelekea Russia akiwa njiani kwenda Ecuador. Washington ilikuwa imeiomba Moscow kumkamata afisa huyo wa zamani wa CIA na kumrudisha nyumbani lakini hilo halikufanyika. Kwa sasa Snowden ameelekea Ecuador anakotarajiwa kupata hifadhi ya kisiasa. Wachambuzi wa mambo wanasema kwa kuzingatia jinsi mgogoro wa Syria ulivyozigawa Marekani na Russia, kadhia ya Snowden inatarajiwa kupanua zaidi ufa wa kidiplomasia ulioko kati ya nchi mbili hizo.

WAPINZANI WA MURSI WAPANGA MAANDAMANO YA KUMNG'OA

Kiongozi mmoja nchini Misri Mahmoud Badr muasisi wa kampeni za kutaka kumg'oa rais Misri madarakani amesema Wananchi wa Misri wameoneka kugawanyika katika makundi mawili, yale ya wafuasi wa chama tawala cha Muslim bradhardhood pamoja na wale wa upinzani wanaomtaka rais Mohamed Morsi kuondoka madarakani, hali ambayo wachambuzi wa siasa wanaona kuwa inatishia kuzuka kwa machafuko nchini humo. Harakati zinaendelea nchini humo ambapo kapmeni ya Tamarod, ikimaanisha Uasi kwa kiarabu na tayari sahihi elfu kumi na tano zimekusanywa kuhakikisha wanapata idadi inayokubaliwa na sheria ili kuitisha uchaguzi mwingine kabla ya wakati.
Vyama kadhaa vya upinzani nchini humo vimejiunga na harakati za kuandamana kwa wingi mbele ya ikulu ya taifa hili Juni 30, ikiw ani tarehe ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu kuchaguliwa kwa rais Mohamed Morsi hali tete ya uchumi wa taifa hilo, uhaba wa mafuta, kukatika kwa umeme na kupandishwa kwa bei ya bidhaa mbalimbali nchini humo ndio imekuwa sababu ya kuwakusanya pamoja wananchi wa Misri chini ya kauli mbiu, kuuangusha utawala wa Muslim Bradherhood unaotuhumiwa kutaka kimabavu.
Hata hivyo swala hili limewagawa wananchi wa Misri ambao baadhi wanaumuunga Mkono rais na ambao wanahofia kuzuka kwa machafuko.Mohammed Hamed mkuu wa zamani wa baraza la kitaifa amesema kukusanya sahihi juu ya kumpinga raia au la haina athari yoyote kisheria, hili ni shinikizo la kisiasa.Mahmoud Badr yeye anasema kuwa kuanzisha kampeni Tamarod ni baada ya kuona kwamba rais Morsi ameshindwa, kisiasa, kiuchumi, kijamii na ameshindwa kutekeleza malengo ya mapinduzi ya mwanzoni mwa mwaka 2011 yaliompindua rais Hosni Moubarak.
Jumalililopita wafuasi wa chama tawala walijitokeza kwa wingi katika barabara za jijini Cairo kumuunga mkono rais Morsi huku wakidai kuwa rais haondolewi madarakani kwa maandamano. hii ni baada ya upinzani kuitisha maandamano makubwa Juni 30 wakati wa sherehe za kuadhimisha mwaka mmoja tangu kuchaguliwa kwa rais Morsi.

RAIS WA UFARANSA AWASILI QATAR KUIJADILI SYRIA

Raisi wa Ufaransa Francois Hollande amewasili nchini Qatar tayari kwa mazungumzo juu ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yanayoendelea nchini Syria na kujadili mahusiano ya kiuchumi na taifa hilo lenye utajiri wa gesi.Raisi Hollande amejumuika nchini humo kufuatia mkutano wa mataifa rafiki za Syria katika siku iliyoamuliwa kutolewa haraka kwa msaada wa kijeshi kuwasaidia waasi wa Syria.
Aidha raisi Hollande alizungumza katika mkutano wake na wafaransa waishio Qatar na kusema kuwa amekaribisha maamuzi ambayo yataruhusu kuunga mkono upinzani nchini Syria ili kufikiwa lengo la kupatikana suluhu ya kisiasa.
Mawaziri kutoka uingereza, misri, ufaransa, Ujerumani, Italia, Jordan, Qatar, Saudi Arabia, Uturuki na marekani kwa pamoja walihudhuria mazungumzo hayo. Tamko la mwisho lilikuwa ni kwa kila nchi kwa namna yake ingetoa haraka mahitaji na vifaa vyote muhimu ili kuwawezesha waasi kuwalinda watu wa Syria pia kukabiliana na mashambulizi ya kikatili yanayofanywa na majeshi ya serikali na washirika wake.

JESHI LA LEBANON LAAPA KUWASAKA WASUASI WA KISUNNI

Jeshi nchini Lebanoni, limesema litaendelea na operesheni ya kuwasaka wafuasi wa kiongozi wa kidini dhehebu la Sunni mwenye msimamo mkali waliotekeleza mauaji ya wanajeshi 12 kusini mwa taifa hilo. Viongozi wa kijeshi wamethibitisha baada ya kikao cha dharura kilichofanyika mapema leo asubuhi na kuwashirikisha maafisa wote wa Usalama. Katika taarifa iliotolewa baada ya kikao cha dharura cha maafisa wa kijeshi na usalama, wameamuwa kuwasaka waasi na kuwasambaratisha hadi kwenye ngome yao ya cheikh Ahmad al Assir na kuwatia nguvuni wale wote walioleta choko choko kwa jeshi.
Kikao hicho cha dharura kiliongozwa na rais wa taifa hilo Michel Sleimane na kiliitishwa ili kutathimini muendelezo wa uperesheni ya kijeshi dhidi ya waasi waliohusika na mauaji ya wanajeshi 12 katika shambulio lililotokea jana katika mji wa Abra katika kitongoji cha mji wa bandari wa Saida.Katika taarifa iliotolewa na jeshi imewataka waasi walioshambulia wanajeshi na raia, kujisalimisha ili kuepusha umwagaji wa damu, na kwamba jeshi litaendelea na operesheni ya kuwafyeka wanaomiliki silaha katika mji wa Saida hadi pale usalama utaimarika.
Wakati huo huo vyombo vya sheria nchini humo vimemfungulia mashtaka Cheikh Al Assir na wafuasi wake 123.Mapambano yalianza jana Jumapili baada ya shambulio dhidi ya kituo cha wanajeshi ambapo wafuasi wa Cheikh Assir mwenye msimamo mkali wa kidini anaepingana na kundi la Hezbollah kundi la Kishia linalo pambano bega kwa bega kuusaidia utawala wa rais Bashar Al Assad.Kiongozi huyo wa kidini amejipatina umaarufu baada ya  msimao wake wa kuikosoa ya serikali ya Damascus na vikosi vya Hezbollah.
Hivi karibuni alilituhumu jeshi nchini humo kusalia kimya dhidi ya kundi la uasi lenye nguvu nchini humo la Hezbollah.Serikali ya Lebanoni, inaendelea na msimamo wake wa kutoegemea upande wowote katika mzozo wa Syria licha ya tuhuma ambazo zimeanza kutolewa tangu pale wapiganaji wa kundi la Hezbollah walipojiunga na majeshi ya Syria kuusaidia utawala wa rais Assad dhidi ya waasi ambao kwa asilimia kubwa ni wasuni, jambo ambalo laonekana kuzua mvutano kwa saaa nchini Liban